1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DW yamtunuku Jimmy Lai kwa kutetea uhuru wa habari

24 Juni 2026

Mwanawe anasema wanaopigania uhuru wa wengine hawako peke yao. Kauli hiyo imepewa uzito mpya baada ya Jimmy Lai kutunukiwa Tuzo ya DW ya Uhuru wa Kujieleza akiwa bado gerezani.

https://p.dw.com/p/5G027
Mashtaka dhidi ya mchapishaji Jimmy Lai mjini Hongkong
Akiwa amefungwa gerezani kwa zaidi ya miaka mitano, Jimmy Lai bado anaendelea kuonekana na wengi kama ishara ya upinzani dhidi ya kubanwa kwa uhuru wa habari na demokrasia Hong KongPicha: Anthony Wallace/AFP

Mjasiriamali wa vyombo vya habari na mtetezi wa demokrasia wa Hong Kong Jimmy Lai ametunukiwa Tuzo ya Uhuru wa Kujieleza ya Deutsche Welle (DW) mwaka huu kwa mchango wake katika kutetea uhuru wa habari na haki ya kujieleza.

Lai, mwenye umri wa miaka 78, kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 20 jela mjini Hong Kong baada ya kukutwa na hatia ya kile mamlaka zilichokiita "kushirikiana na nguvu za kigeni." Kesi yake imekuwa alama ya hali inayozidi kuzua wasiwasi kuhusu uhuru wa vyombo vya habari katika eneo hilo.

Tuzo hiyo ilitolewa Jumanne katika Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari la Deutsche Welle - Global Media Forum, linalofanyika mjini Bonn, Ujerumani.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Jodie Ginsberg, Mkurugenzi Mkuu wa Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ), alisema Lai amekuwa mfano wa mtu aliyesimama kidete kutetea vyombo vya habari huru licha ya gharama kubwa binafsi.

Alisema mashambulizi dhidi ya gazeti la Apple Daily na vyombo vingine vya habari vya Hong Kong yalitangulia hatua kubwa zaidi za kubana uhuru wa kiraia zilizofuata katika miaka ya karibuni.

China Hongkong 2020 | Kukamatwa kwa mmiliki wa vyombo vya habari na mwanaharakati wa uhuru Jimmy Lai
Jimmy Lai alikamatawa na maafisa wa Polisi kutoka nyumbani kwake mjini Hong Kong, Aprili 18, 2020Picha: Vincent Yu/AP Photo/picture alliance

Kutoka mhamiaji maskini hadi tajiri wa vyombo vya habari

Safari ya Jimmy Lai ilianza akiwa mtoto wa miaka 12 aliyekimbia kutoka Guangzhou kusini mwa China kuelekea Hong Kong, iliyokuwa koloni la Uingereza wakati huo.

Akiwa hana chochote, Lai alijijengea utajiri kupitia biashara ya nguo na mwaka 1981 akaanzisha chapa maarufu ya Giordano, ambayo ilimfanya kuwa mmoja wa wafanyabiashara wenye mafanikio makubwa Hong Kong.

Hata hivyo, tukio la mauaji ya waandamanaji waliokuwa wanadai demokrasia katika Uwanja wa Tiananmen mjini Beijing mwaka 1989 lilibadilisha kabisa mtazamo wake kuhusu siasa na uhuru.

Baada ya hapo, aliamua kutumia sehemu ya utajiri wake kuunga mkono harakati za demokrasia na kuingia katika sekta ya vyombo vya habari.

Alianzisha Jarida la Next na baadaye gazeti la Apple Daily, ambalo lilijulikana kwa uchunguzi wa kina, ukosoaji wa serikali na kuunga mkono waziwazi harakati za demokrasia Hong Kong.

China Hongkong 2021 | Kiwanda cha gazeti la Apple Daily baada ya uvamizi wa maafisa usalama
Gazeti la Apple Daily, lililoanzishwa na Jimmy Lai lilikuwa na jukumu kubwa katika kupigania uhuru Hong KongPicha: Kin Cheung/AP Photo/picture alliance

Sauti ya demokrasia Hong Kong

Kwa miaka mingi, Apple Daily lilikuwa moja ya vyombo vya habari vyenye ushawishi mkubwa Hong Kong.

Gazeti hilo lilichanganya habari za uchunguzi, biashara, burudani na siasa, huku likibaki kuwa jukwaa muhimu kwa sauti zinazoikosoa Beijing.

Lai mwenyewe alishiriki katika maandamano makubwa ya harakati za Vuguvugu la Miavuli la mwaka 2014 na maandamano ya kupinga sheria ya kurejesha washukiwa China mwaka 2019.

Baada ya Beijing kuweka Sheria ya Usalama wa Taifa mwaka 2020, Lai alikamatwa na Apple Daily kulazimika kusitisha shughuli zake mwaka mmoja baadaye.

Tangu wakati huo, vyombo vingine kadhaa vya habari vinavyojitegemea pia vimefungwa au kusitisha shughuli kutokana na mazingira yanayozidi kuwa magumu kwa uhuru wa habari.

Ujerumani Bonn | Claire Lai kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Vyombo vya Habari
Binti wa Jimmy Lai, Claire Lai alisema tuzo ya DW inamaanisha wanaopiganiaa uhuru wa wengine kama baba yake kamwe hawako pekee yaoPicha: DW

Miaka zaidi ya mitano gerezani

Jimmy Lai amekuwa gerezani tangu Desemba mwaka 2020 na amekaa zaidi ya siku 2,000 katika mazingira ya kutengwa.

Mnamo Februari mwaka huu alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, adhabu inayochukuliwa kuwa mojawapo ya kali zaidi kutolewa chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa.

Mahakama ilisema Lai alitumia ushawishi wake na gazeti la Apple Daily kupinga mamlaka ya Chama cha Kikomunisti cha China na serikali ya Hong Kong.

Lai alikana mashtaka yote dhidi yake, lakini timu yake ya wanasheria imesema hatakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Familia yake imeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu afya yake, ikisema ana ugonjwa wa kisukari na amepungua uzito kwa kiasi kikubwa akiwa gerezani.

Hong Kong 2025 | Watu wakisubiri nje ya Mahakama ya West Kowloon kabla ya kutolewa kwa hukumu dhidi ya tajiri wa vyombo vya habari Jimmy Lai
Watu wakisubiri nje ya Mahakama ya West Kowloon kabla ya kutolewa kwa hukumu dhidi ya tajiri wa vyombo vya habari Jimmy LaiPicha: Vernon Yuen/Nexpher Images/Sipa USA/picture alliance

Tuzo yenye ujumbe wa mshikamano

Mwanawe, Claire Lai, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kampeni za kutaka aachiliwe huru, amesema tuzo hiyo ina umuhimu mkubwa kwa familia yao.

Kulingana naye, tuzo hiyo inathibitisha kuwa wale wanaopigania uhuru wa wengine hawasahauliki hata wanapokabiliwa na mateso.

"Watu wanaopigania uhuru, na wale wanaopigania uhuru wa wengine, kamwe hawako peke yao," alisema katika mahojiano na DW.

Claire alisema anaamini baba yake angefurahi sana kujua kwamba ametunukiwa tuzo hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa DW Barbara Massing alisema taasisi hiyo inamtambua Jimmy Lai kwa kujitolea kwake kusikoyumba katika kutetea maadili ya kidemokrasia na uhuru wa habari.

Je, kuna siku ataachiwa huru?

Swali kubwa linalobaki ni kama Jimmy Lai ataweza kutoka gerezani akiwa hai. Familia yake inasema imepita miaka mitano tangu wamwone ana kwa ana, huku mawasiliano yao yakifanyika kwa njia ya barua pekee.

Sebastien Lai alisema mojawapo ya ndoto zake kubwa ni siku ambayo baba yake atarudi nyumbani na familia yote kukaa pamoja mezani kwa mara nyingine.

Hata hivyo, matumaini hayo yanaendelea kufifia kadiri miaka inavyosonga mbele.

Kwa wengi, Jimmy Lai amekuwa zaidi ya mfungwa wa kisiasa; amegeuka kuwa ishara ya mapambano ya uhuru wa habari, demokrasia na haki ya wananchi kupata taarifa bila hofu ya ukandamizaji.