Jeshi la Israel lasema limewaua ‘magaidi’ wanne Rafah
30 Novemba 2025
Jeshi la Israel limesema Jumapili (30.11.2025) kuwa limewaua Wapalestina wanne iliowataja kuwa magaidi baada ya kutoka kwenye handaki katika mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Operesheni hiyo ilifanywa kwa mwongozo wa Jeshi la Anga la Israel.
Wakati huo huo, Wizara ya Afya ya Gaza imetangaza kuwa idadi ya vifo kutokana na mashambulizi ya Israel imevuka 70,000, baada ya watu 301 kuongezwa kwenye hesabu tangu siku ya Alhamisi.
Taarifa hiyo imesema watu wawili waliuawa katika mashambulizi ya hivi karibuni, wengine wakitambuliwa kutoka kwenye mabaki yaliyokuwa chini ya kifusi.
Huku mashambulizi yakiendelea, Misri inawapa mafunzo mamia ya maafisa wa polisi wa Kipalestina kwa lengo la kuunda kikosi cha usalama baada ya vita. Zaidi ya maafisa 500 wamehitimu mafunzo mjini Cairo, na mafunzo ya miezi miwili yanaendelea kwa mamia zaidi.