Familia za mateka: Amani isitishwe hadi Hamas iwajibike
16 Oktoba 2025
Katika taarifa, Kundi la Familia za Mateka na waliotoweka, limeitaka serikali ya Israel kusitisha mara moja utekelezwaji wa hatua zozote zaidi za makubaliano ikiwa Hamas itaendelea kukiuka waziwazi wajibu wake wa kurejeshwa kwa mateka wote na miili ya waliofariki.
Miili miwili zaidi ya mateka wa Israel yatambuliwa
Taarifa ya jeshi la Israel imesema miili miwili zaidi imetambuliwa kuwa ya mateka wa Israel waliouawa, baada ya kukabidhiwa miili hiyo na kundi la wanamgambo wa Hamas jana usiku.
Miili hiyo ilitambuliwa kuwa ya Inbar Hayman mwenye umri wa miaka 27, mateka wa mwisho wa kike kushikiliwa huko Gaza tangu alipotekwa nyara kutoka kwa tamasha la muziki wakati wa shambulio lililoongozwa na Hamas kusini mwa Israel mnamo Oktoba 7, 2023.
Mwili wa pili ulitambuliwa kuwa wa Sajenti Muhammad Al-Atarash mwenye umri wa miaka 39, ambaye aliuawa wakati wa vita na kundi hilo la Hamas Oktoba 7, 2023 na mwili wake kuchukuliwa mateka hadi Gaza.
Chini ya mapatano yaliyosimamiwa na Marekani kati ya Israel na Hamas, yaliolenga kumaliza vita vya miaka miwili huko Gaza, Hamas ilikuwa iwaachie mateka 20 waliosalia na 28 waliokufa kwa kubadilishana na takriban wafungwa 2,000 wa Kipalestina kutoka jela la Israel.
Israel kutangaza baadaye kufunguliwa kwa kivuko cha Rafah
Katika hatua nyingine mamlaka ya Israel inayosimamia masuala ya kiraia katika maeneo ya Palestina, COGAT imesema tarehe ya kufunguliwa kwa kivuko cha Rafah kuwezesha kuvuka kwa watu itatangazwa baadaye, mara tu upande wa Israel, pamoja na wa Misri, utakapokamilisha maandalizi muhimu ya ufunguzi wa kivuko hicho.
Mratibu wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), Hani Isleem amesema wao kama shirika, wameshuhudia wagonjwa 19 kati ya 200 kwenye orodha yao wakifariki dunia.
Merz autaka Umoja wa Ulaya kujifunza kutoka mpango wa amani wa Trump
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz anaamini Umoja wa Ulaya lazima ujifunze kutoka kwa mpango wa amani wa Gaza wa Rais wa Marekani Donald Trump kuchukua hatua thabiti katika jukwaa la kimataifa.
Akitoa hotuba ya sera za kigeni jana katika baraza la chini la bunge la Ujerumani, Merz amesema katika ulimwengu unaokuwa na ambao umekuwa mbaya zaidi nguvu pekee ndizo zinazohifadhi amani.
Pia ameongeza kuwa udhaifu husababisha amani kudorora.