Israel imewaita wanajeshi zaidi Gaza | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Israel imewaita wanajeshi zaidi Gaza

Wiki mbili baada ya kuanza mashambulizi ya ardhini katika Ukanda wa Gaza, Israel imewaita wanajeshi wengine wa ziada 16,000 kuendelea na mapambano hayo, huku idadi ya waliofariki Palestina ikiongezeka na kufikia 1,363.

Baadhi ya wanajeshi wa Israel

Baadhi ya wanajeshi wa Israel

Afisa mkuu wa jeshi la Israel amesema wanajeshi hao watabadilishana majukumu na wale ambao wako katika uwanja wa mapambano kwa sasa. Afisa huyo amesema idadi ya wanajeshi wa ziada ambao hadi sasa wameshaitwa jeshini imefikia 86,000.

Kwa upande wa Baraza la mawaziri la Israel linaloshughulika na usalama limetoa maelekezo kwa jeshi la nchi hiyo kupanua zaidi mashambulizi yao ndani ya Ukanda wa Gaza, huku baraza kamili la mawaziri likikutana leo kuzungumzia oparesheni hiyo.

Katika Mkutano huo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema wanajeshi wataendelea kuharibu mahandaki yanayotumiwa na wanamgambo wa Gaza kuishambulia Israel hata mapigano yakisitishwa.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Netanyahu amesema mpaka sasa wameyaharibu mahandaki kadhaa na kwamba Israel ina nia ya kumaliza oparesheni yake hiyo.

Wakati huo huo msemaji wa wizara ya afya mjini Gaza Ashraf al-Qedra amesema idadi ya waliouwawa hapo jana pekee imepanda hadi 119 kutokana na idadi ya waliouwawa katika shambulizi kwenye shule ya Umoja wa Mataifa iliokuwa inatumiwa kama eneo la hifadhi kwa wakimbizi kupanda.

Ashraf al-Qedra amesema kwa sasa idadi jumla ya waliouwawa imefikia 1,363 huku wengine 7,680 wakijeruhiwa na kuongeza kwamba asilimia 40 ya wale waliouwawa ni watoto. Nayo Israel inayosema inapambana na wanamgambo walio na itikadi kali wa Hamas, imepoteza wanajeshi wake 56 katika vita hivyo.

Umoja wa Mataifa wasema ni wakati wa kusema imetosha kwa mashambulizi

Naibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson amesema kwa sasa imefikia wakati wa kusema tosha katika mapigano yanayoendelea. "Tuna hali ya hatari sana kwa mtazamo wa kibinadamu. Kwangu mimi huu ni wakati ambapo kwa kweli unapaswa kusema imetosha," alisema Eliasson

Nembo ya Umoja wa Mataifa

Nembo ya Umoja wa Mataifa

Hii leo asubuhi mapambano yalianza tena karibu na shule nyengine ya Umoja wa Mataifa mjini Beit Hanoun, Kaskazini mwa Gaza. Takriban watu 15 walijeruhiwa wakati wanajeshi wa Israel walipofyatuliana risasi na wanamgambo wa Palestina.

Marekani kwa upande wake imelaani shambulizi katika shule ya Umoja wa Mataifa, lakini imeendelea kutoa msaada wake wa kijeshi kwa jeshi la Israel huku ikiidhinisha nchi hiyo kupokea silaha ambazo bila shaka zitatumika katika mashambulizi yanayoendelea.

Kwa upande mwengine Marekani pia imelaani hatua ya wanamgambo wa Hamas kuficha baadhi ya makombora yao katika shule hizo. Hii ni baada ya afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa kukiri kupata roketi katika moja ya majengo yake kwa mara ya pili.

Mwandishi Amina Abubakar/dpa/AFP

Mhariri Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com