Iraq yasifika katika kikao cha Kuwait | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.04.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Iraq yasifika katika kikao cha Kuwait

Kikao cha nne cha nchi za kiarabu na zile za magharibi zenye uwezo mkubwa kitafanyika mjini Baghdad

Waziri mkuu wa Iraq Nouri al-Maliki akihutubu

Waziri mkuu wa Iraq Nouri al-Maliki akihutubu

Kikao cha nne kitakachokutanisha Iraq, na nchi zingine za kiarabu pamoja na mataifa yenye nguvu duniani kitafanyika Baghdad kwa mara ya kwanza baada ya cha tatu kumalizika leo Kuwait.


Waziri wa nchi za nje wa Kuwait Sheikh Mohamed al-Sabah amesema hayo baada ya kikao cha Kuwait kumalizika lakini hakutaja tarehe ya kikao hicho cha nne.


Katika ripoti iliyotolewa baada ya kikao cha Kuwait mataifa yaliyohudhuria yameipongeza Iraq kwa juhudi zake za kukabiliana na wanamgambo wanaovuruga amani.


Nchi jirani za kiarabu zenye utawala wa kisunni zimeanza kuukaribisha utawala wa kishia wa Iraq. Kulingana na waziri wa nchi wa Iraq Hoshyar Zebari Iraq itaendelea kuwa na subira inapoitisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kutoka kwa jirani zake.


Zebari ametamka hayo alipokutana na waziri wa nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice ambaye anazishawishi nchi za kiarabu ziunge mkono juhudi za waziri mkuu wa Iraq Nuri al Maliki za kukabiliana na wanamgambo wa kishia alizoanza mwezi uliopita.


Rice anaamini kwamba Iraq imepiga hatua kubwa za kisiasa. Anasema "Ama kwa kweli ni wakati muhimu kwa Irak shukrani kuu ni kwa maamuzi ya makubwa aliyofanya waziri mkuu na utawala wa Iraq uliyoshikamana"


Tangu wanajeshi wa Marekani walipoongoza kug'atuliwa mamlakani kwa kiongozi wa kisunni saddam Hussein mwaka wa 2003 nchi za kiarabu zimekuwa na hofu sio tu ya mashambulio ya mara kwa mara nchini humo bali pia ya uhusiano wa Iraq na Iran ambayo sio taifa la kiarabu.


Lakini katika hotuba yake waziri mkuu wa Iraq al Maliki aliondoa hofu hiyo akisema Iraq imefaulu kumaliza tofauti miongoni mwa wananchi wake na sasa matakwa ya watu wake yameuganishwa.


Katika taarifa iliyosomwa baada ya kikao cha Kuwait, Majeshi ya Iraq na walinda usalama nchini humo wamepongezwa kwa kuendelea kukabiliana na wanamgambo na pia kusimama wima dhidi ya vitisho vya hivi karibuni vilivyotolewa na wapiganaji nchini humo.


Kikao hicho kimeukaribisha mpango wa Iraq wa kuwafanya wapiganaji wote wasalimishe silaha zao na kulinda sheria.


Marekani imekuwa ikishawishi nchi za kiarabu zenye utawala wa wasunni ziunge mkono serikali ya waziri mkuu Nuri al Maliki wa Iraq.


Akihutubia kikao cha Kuwait leo al Maliki amezilaumu nchi za kiarabu kwa kutoshirikiana vyema na Iraq na kufuta madeni zinazodai nchi hiyo akisema utawala wa Saddam Hussein umekwisha na nchi hiyo sio tisho tena katika eneo la ghuba.


Maliki hakutaja nchi yoyote lakini matamko yake yanaonekana kana kwamba yalikuwa yanalenga nchi za kiarabu zinazoongozwa na wasunni ambazo zinaushirikano duni na serikali yake ya washia.


Iraq imetoa wito kwa mataifa ya ghuba kuondoa deni la mabilioni ya dola ambalo linaikabili nchi hiyo kufuatia uvamizi wake nchini Kuwait mwaka wa 1990.


Waziri huyo mkuu ametoa wito kwa nchi jirani kufungua balozi zake mjini Baghdad akisema kwamba nchi nyingine nyingi zimeendelea na shughuli zake mjini humo bila kujali hali ya usalama.


Hakuna balozi kutoka nchi ya kiarabu inayoongozwa na wasunni iliyowekwa rasmi mjini Baghdad tangu balozi wa Misri alipotekwa nyara na kuuawa mda mfupi tuu baada ya kuwasili mwaka wa 2005.


Saudi Arabia na Bahrai zimeahidi kufungua balozi zake mjini Baghdad; jambo ambalo kulingana na Marekani linaongeza matumaini ya nchi zingine za kiarabu kufuata mkondo huo huo.


Ziara za viongozi wakuu kutoka nchi za kiarabu nchini humo pia zimekuwa chache.


Lakini ihusiano wa nchi hiyo na Iran unaonekana ukinawiri.


Waziri wa nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice ambaye amekuwa akizishawishi nchi za kiarabu ziwajibike katika kurejesha uhusiano mwema na Iraq na pia zisahau madeni zinazoidai nchi hiyo amesema Iraq imeanza kukubaliwa tena katika jimbo la ghuba akidai kwamba baadhi ya nchi tayari zimependekeza kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Iraq.


Iraq inatakikana kulipa asilimia tano ya pato lake la mafuta katika mfuko maalum uliotengwa na baraza la usalama la umoja wa mataifa kama malipo kwa hasara iliyotokana na vita vya mwaka wa 1990 vilivyoongozwa na Saddam Hussein.


Kikao cha Kuwait kinafuatia vikao vilivyofanyika Uturuki na Misri.


Kulingana na waziri wa nchi za nje wa Kuwait Iraq itaandaa kikao cha nne cha nchi hizo za kiarabu pamoja na nchi za magharibi mjini Baghdad kwa mara ya kwanza.

 • Tarehe 22.04.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DmrD
 • Tarehe 22.04.2008
 • Mwandishi Mwakideu, Alex
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DmrD
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com