Iran yailaumu Ulaya kwa kusambaratika mkataba wa nyuklia | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.09.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Iran yailaumu Ulaya kwa kusambaratika mkataba wa nyuklia

Mkuu wa shirika la atomik nchini Iran amesema, nchi za Ulaya zilizofikia makubaliano na Iran mnamo mwaka 2015  zimeshindwa kutimiza mipango waliyodhamiria chini ya makubaliano hayo.

Mkuu huyo ameyasema haya siku moja baada ya Iran kutangaza kwamba itakiuka zaidi viwango vya kurutubisha madini ya Urani ilivyowekewa chini ya makubaliano hayo.

Ali Akbar Salehi ameyasema haya katika kikao na waandishi wa habari pamoja na kaimu mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kawi ya Nyuklia IAEA Cornel Feruta ambaye alikuwa katika ziara ya siku moja nchini Iran. Hatua ya Iran kusema kuwa inaongeza viwango vya madini ya urani ni pigo jipya kwa makubaliano hayo ya mwaka 2015.

Ufaransa, Ujerumani na Uingereza wamejaribu kuilinda Iran

Mkataba huo wa nyuklia ulihakikisha kwamba Iran inasitisha mpango wake wa nyuklia kwa ajili ya kupunguziwa vikwazo, ingawa umesambaratika tangu Marekani ijiondoe mwaka jana na kuiwekea vikwazo Iran kuuza mafuta yake katika nchi za nje.

Iran Atomprogramm

Mfanyakazi katika kituo cha kuyabadilisha madini ya Urani

Ufaransa, Ujerumani na Uingereza wamejaribu mfumo wa biashara ya kubadilishana bidhaa na Iran ili kuilinda kutokana na vikwazo vya Marekani ingawa wamekuwa na wakati mgumu kuanzisha biashara hiyo. Wiki iliyopita Iran iliweka muda wa mwisho wa siku sitini kwa nchi za Ulaya kuchukua hatua mwafaka.

Ali Akbar Salehi ni mkuu wa mpango wa nyuklia wa Iran.

"Kuhusiana na jukumu la Umoja wa Ulaya kuichukua nafasi ya Marekani katika mkataba wa nyuklia, kwa bahati mbaya walishindwa kutimiza waliyoahidi. Fauka ya hayo tumesikia kwamba msemaji wa Umoja wa Ulaya amesema wataendelea kuushikilia ule mpango wa JCPOA. Nimeshangazwa sana na jambo hili," alisema Salehi.

Majadiliano yanayoendelea yanahitaji ushirikiano mkubwa

Kulingana na taarifa ya shirika la IAEA lililo na makao yake huko Geneva Uswisi,katika ziara Cornel Feruta amefahamishwa kuhusu hatua za hivi karibuni ilizochukua Iran.

Cornel Feruta

Kaimu mkuu wa IAEA Cornel Feruta

Shirika hilo linasema kuwa majadiliano yanayoendelea sasa yanahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa Iran jambo ambalo wanadiplomasia wanasema huenda likaleta suala la wasiwasi kuhusiana na utoaji wa taarifa.

"Na sote tunajua kuwa IAEA ina jukumu muhimu katika masuala kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran. Kwa upande mmoja tunaangalia na kuthibitisha uetekelezwaji wa maazimio chini ya makubaliano hayo na kwa upande mwengine tunahusika katika utekelezaji wa makubaliano hayo na itifaki nyenginezo," alisema Feruta.

Ufaransa ambayo imekuwa ikiongoza juhudi za Ulaya kuunusuru mkataba huo, hapo jana iliitaka Iran isitishe hatua zake za kukiuka makubaliano hayo ya nyuklia.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com