1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya waliokufa mafuriko Afrika Kusini yakaribia 400

Iddi Ssessanga
16 Aprili 2022

Eneo lililokumbwa na mafuriko mashariki mwa Afrika Kusini limepigwa na mvua zaidi Jumamosi, baada ya dhoruba mbaya zaidi nchini humu kuua takribani watu 400 na kuwaacha maelfu bila makaazi.

https://p.dw.com/p/4A1hm
Überschwemmung in Südafrika
Picha: AP/picture alliance

Idara ya huduma za dharura katika jimbo la kusini mashariki la KwaZulu-Natal (KZN), ulipo mji wa Durban, ilikuwa katika hali ya tahadhari huku watabiri wa hali ya hewa wakitabiri mvua zaidi wikendi ya Pasaka.  

"Mvua tayari inanyesha katika baadhi ya maeneo ya KZN lakini haitakuwa kubwa kama ilivyokuwa katika siku chache zilizopita," Puseletso Mofokeng, mtabiri mkuu katika idara ya huduma ya hali ya hewa ya Afrika Kusini aliliambia shirika la habari la AFP.

Soma pia: Waliokufa katika mafuriko Afrika Kusini wafikia 259

"Lakini kwa sababu ya udongo kujaa maji kupita kiasi, bado tunaweza kupata mafuriko makubwa," alionya.

BG Südafrika | Erdrutsch Überflutung
Usafi ukifanyika katika eneo la Marianridge, Durban, kufuatia mvua kubwa zilizosababisha mafuriko, Aprili 12, 2022.Picha: ROGAN WARD/REUTERS

Serikali ya mkoa ilisema siku ya Ijumaa kuwa timu za usimamizi wa maafa ziko kwenye "tahadhari ya juu kuzishughulikia haraka jamii zinazojulikana kuwa katika hatari kubwa, kuepusha au kupunguza athari za maafa".

Wanajeshi, polisi na waokoaji wa kujitolea wanafanya kazi kutokea uwanja mdogo wa ndege wa kiraia ambao kawaida hutumika kwa maonyesho ya anga na kwa mafunzo kwa marubani.

"Tumejitayarisha kikamilifu," amesema Dave Steyn, afisa mkuu wa polisi anayeratibu shughuli za uokoaji na ufufuaji katika uwanja huo wa ndege.

Shawn Herbst wa kampuni ya uitikiaji wa kwanza ya Netcare 911 ameiambia AFP: "Cha kusikitisha bado kuna miili inayopatikana kwenye makaazi, hasa kutoka maeneo ya vijijini."

"Bado kuna uharibifu unaoendelea hasa kutokana na mvua inayonyesha leo ambayo inazidisha hali mbaya katika maeneo ambayo tayari yameharibika”.

Soma pia: Idadi ya waliokufa Afrika Kusini kufuatia mafuriko yakaribia 60

Mafuriko hayo yameharibu zaidi ya nyumba 13,000 na kuziharibu kabisa nyingine takribani 4,000.

Janga lisilo kifani

Mamlaka zimewataka watu walio katika maeneo hatarishi kuhamia katika vituo vya kijamii kama vile kumbi na shule. Maji safi yamekuwa haba na mamlaka zimeahidi kupeleka matenki ya maji.

Südafrika Überschwemmungen nach Unwettern
Watu wakikusanyika kwenye gari kupata maji safi na salaama katika kitongoji cha Bhambayi.Picha: PHILL MAGAKOE/AFP

Serikali imetangaza randi bilioni moja (dola milioni 68) katika ufadhili wa misaada ya dharura.

"Wakati tukifikiria kuwa ni salama sasa kutoka katika janga la (Covid), tumekubwa na janga jengine, janga la asili linaloikumba nchi yetu," Rais Cyril Ramaphosa alisema katika hotuba ya Ijumaa Kuu.

Mafuriko hayo ni "janga kubwa lisilowahi kushuhudiwa nchini hapo kabla nchini mwetu."

Soma pia:UN: Afrika kuathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabia nchi

Zaidi ya askari polisi 4,000 wamepelekwa katika maeneo yalioathiriwa kusaidia juhudi za misaada na kulinda sheria na utaratibu.

"Tuko karibu na hospitali ikiwa tutahitajika," amesema Garrith Jamieson, mkurugenzi wa kampuni ya huduma za afya ya ALS Paramedics, yenye makao yake mjini Durban.

Chanzo: AFPE