1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Niederlande Chefanklägerin beim Internationalen Strafgerichtshof in Den Haag | Fatou Bensouda
Picha: Getty Images/AFP/E. Plevier

ICC kuchunguza uhalifu maeneo yanayokaliwa na Israel

Mohammed Khelef
6 Februari 2021

Majaji mjini The Hague wanasema kuwa mahakama hiyo inaweza kuchunguza kesi za Gaza, Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, huku Israel ikisema uamuzi huo ni wa kisiasa na Wapalestina wakiuita 'ushindi kwa ukweli.'

https://p.dw.com/p/3oyVT

Kwenye hukumu iliyotolewa Ijumaa (6 Februari), Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imeamuliwa kwamba inayo mamlaka ya kisheria kwenye maeneo ya Palestina yanayokaliwa kimabavu na Israel tangu vita vya mwaka 1967. 

Uamuzi huo uliofikiwa na majaji wawili kati ya watatu wa Mahakama hiyo unasema kwamba ICC inazo nguvu za kuhukumu kesi zinazohusiana na Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ikiwemo Jerusalem Mashariki."

Uamuzi huo sasa unaweza kufunguwa njia kwa mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama hiyo mwenye makao yake makuu mjini The Hague kufunguwa uchunguzi wa uhalifu wa kivita dhidi ya vitendo vya jeshi la Israel.

Bensouda asema jeshi la Israel, makundi ya Wapalestina wanahusika uhalifu wa kivita

Palästina Wutprotest in Gaza
Waandamanaji wa Kipalestina kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS/Y. Masoud

Mnamo mwaka 2019, mwendesha mashitaka huyo, Fatou Bensouda, alisema kwamba kulikuwa na sababu za kutosha kufunguwa uchunguzi huo dhidi ya vitendo vya jeshi la Israel kwenye Ukanda wa Gaza mwaka 2014.

Alivitaja vikosi vya Jeshi la Ulinzi na Israel na makundi yenye silaha ya Palestina, kama vile Hamas, kuwa wanaweza kuhusika na vitendo hivyo. 

Mapigano hayo ya mwaka 2014 yaliangamiza maisha ya Wapalestina wakaribiao 2,000 na zaidi ya Waisraeli 60. 

Mwanasheria huyo mwenye asili ya Gambia pia alitaka kuchunguza makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kwenye Ukingo wa Magharibi, lakini kwanza aliiomba Mahakama hiyo kuamuwa endapo anayo mamlaka ya kisheria ya kuendelea na kesi hiyo.

Israel yapinga, Palestina yapongeza

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameulaani uamuzi huo, akiita Mahakama hiyo kuwa "chombo cha kisiasa na sio taasisi ya kisheria."

"ICC inapuuzia uhalifu wa kweli wa kivira na badala yake inaiandama Dola la Israel, dola ambalo lina serikali imara ya kidemokrasia inayoenzi utawala wa sheria," alisema Netanyahu.

Israel | Premierminister Netanjahu Rede Knesset Likud
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu asema uamuzi huo ni wa kisiasa na si kisheria.Picha: Yonatan Sindel/REUTERS

Waziri wa Masuala ya Kiraia wa Palestina, Hussein al-Sheikh, aliupongeza uamuzi huo kama "ushindi kwa ukweli, haki, uhuru na maadili ulimwenguni."

Israel, ambayo si mwanachama wa ICC, imekuwa ikihoji kwamba Mahakama hiyo haina mamlaka yoyote ya kisheria, ikidai kuwa hakuna dola la Palestina lenye mamlaka ambalo linaweza kwenda mahakamani juu ya mamlaka ya mipaka yake na raia wake.

Lakini ICC inaweza kutoa hati za kukamatwa ambazo zinaweza kuwafanya maafisa wa Israel kupata wakati mgumu kwenye safari zao nje ya nchi.

Jamii ya kimataifa kwa kiasi kikubwa inayachukulia makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kwenye ardhi za Wapalestina kuwa haramu chini ya sheria za kimataifa.

Israel iliziteka Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa Gaza na Jerusalem Mashariki kwenye vita vya mwaka 1967, maeneo ambayo Wapalestina wanayataka kuanzisha dola lao wenyewe.

Kiasi cha Waisraili 700,000 wanaishi kwenye makaazi ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki, ambao Wapalestina wanasema ni kikwazo kwa amani.