1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hezbollah wapambana na wanajeshi wa Israel Lebanon kusini

Josephat Charo
5 Mei 2026

Kundi la Hezbollah limesema vikosi vyake vilipambana na wanajeshi wa Israeli Jumatatu kusini mwa Lebanon.

https://p.dw.com/p/5DH7C
Moshi ukipaa angani kufuatia shambulizi la Israel huko Zawtar al-Sharqiyah kusini mwa Lebanon
Moshi ukipaa angani kufuatia shambulizi la Israel huko Zawtar al-Sharqiyah kusini mwa LebanonPicha: AFP

Kundi la Hezbollah limesema vikosi vyake vilipambana na wanajeshi wa Israeli Jumatatu kusini mwa Lebanon karibu na mpaka ambapo wanajeshi hao bado wanaendesha shughuli zao licha ya usitishaji mapigano dhaifu tangu Aprili 17.

Kundi hilo linaloungwa mkono na Iran lilisema katika taarifa kwamba baada ya wanajeshi wa Israeli kujaribu kusonga mbele karibu na mji wa Deir Seryan, wapiganaji wake walifyatulia risasi jeshi la adui na kupambana nao katika mapigano makali.

Jeshi la Israeli lilithibitisha kulikuwa na mapigano na wapiganaji wa Hezbollah kusini mwa Lebanon ambapo wanajeshi wake wawili walijeruhiwa na kupelekwa hospitali kupata matibabu.

Hezbollah pia walidai kufanya mfululizo wa mashambulizi mengine dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Israeli kusini mwa Lebanon ambayo walisema yalikuwa ni ya kujibu ukiukaji wa usitishaji mapigano uliofanywa na Israel.