1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatima ya Georg Maaßen magazetini

Oumilkheir Hamidou
10 Septemba 2018

Mjadala kuhusu matamshi ya mkuu wa idara ya upelelezi Georg Maaßen aliyeshuku yaliyotokea Chemnitz ,na suala kama kisa cha Chemnitz kitashuhudiwa pia Köthen ni miongoni mwa mada magazetini .

https://p.dw.com/p/34bUl
Deutschland Horst Seehofer und Hans-Georg Maaßen
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Tunaanzia Chemnitz ambako matukio ya kutimuliwa wageni na wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia yanatiliwa shaka na mkuu wa idara ya upelelezi Georg Maaßen. Matamshi yake yanayokinzana na yale ya kansela Merkel na wanasiasa kadhaa wa Ujerumani yamezusha mjadala kama Maaßen anastahili kuendelea na wadhifa wake. Gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linaandika: "Shaka shaka za mkuu wa idara zote za upelelezi anaeshuku kisa kilichotokea bila ya kutoa ushahidi zinamfanya mtu aamini kwamba Georg Maaßen, mpinzani mmojawapo wa sera ya wakimbizi ya Angela Merkel amelenga kumshambulia Merkel tu. Pengine amesikilizana hivyo na kiongozi wake Horst Seehofer ambae kama waziri wa mambo ya ndani amehindwa kubuni utaratibu wa kazi.

Wote wawili wanachochea mashaka wakitumia suala la usalama. Merkel akitaka kumfukuza kazi kiongozi wa idara ya upelelezi, itamaanisha na waziri wake wa mambo ya ndani atakwenda zake. Na Seehofer akenda zake, itamaanisha na chama cha CSU pia kitajitoa katika serikali kuu ya muungano. SPD wanawatia kishindo sasa wana CDU/CSU. Suala watu wanalojiuliza, eti kweli SPD wanataka serikali kuu ya muungano ivunjike?"

 

Eti yaliyotokea Chemnitz yanaweza kutokea Köthen?

Kisa kama kile kichoshuhudiwa Chemnitz kimetokea pia mwishoni mwa wiki katika mji wa Köthen. Makundi mawili ya vijana wamezozana, mmoja ameanguka na kupiga kichwa chini na kufariki. Vijana wawili wenye asili ya Afghanistan wamekamatwa. Makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia wameitisha maandamano siku hiyo hiyo na wito wao kuitikwa. Mhariri wa gazeti la "Volkstimme" anajibu hofu kama yaliyotokea Chemnitz yanaweza kutokea pia Köthen akisema: "Kinyume na Chemnitz ambako wanasiasa na maafisa wa polisi walikawia kuingilia kati, katika kisa cha Köthen, wanasiasa, wakuu wa makanisa na mashirika  ya kiraia hawajakawia kuingilia kati na kuwasihi watu watulie.

Hawakuwaachia upenu wa kuingilia kati si wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia na wala si wafanyafujo wa siasa kali za mrengo wa kushoto. Kinyume na Chemnitz, Polisi pia waliwekwa kwa wingi kuzuwia machafuko ya aina yoyote ile yasitokee. Kilichosalia hivi sasa ni kujua chanzo cha yaliyotokea Köthen na kutangaza ukweli. Chochote kile chengine kitawapa nguvu wafanya fujo tu tena wa pande zote mbili."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman