Hali ilivyo kuhusu Corona duniani | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.03.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Balaa la Corona laendelea kuitikisa dunia

Hali ilivyo kuhusu Corona duniani

Itali inaendelea kushikilia namba barani Ulaya na duniani katika maambukizi na vifo vinavyotokana na Corona

Zaidi ya watu 337,000 wameambukizwa virusi hivyo hatari duniani na wengine 14,651 wamekufa kutokana na ugonjwa wa Covid19.

Kufikia sasa ripoti zinaeleza kwamba nchi 192 nje ya China zimerekodi visa vya watu walioambukizwa virusi vya Corona na Italia ndio nchi inayoongoza kwa sasa kwa idadi ya waliokufa kutokana na ugonjwa unaosababishwa na virusi hivyo vipya. Idadi ya waliokufa Italia imeipiku ile iliyorekodiwa China nchi ambayo ndio kitovu cha virusi vya Corona.

Taarifa zinasema China bara ambako ndiko ulikoanzia mripuko wa virusi hivyo kuna visa vipya 39 vilivyothibitishwa jana Jumapili na wagonjwa wote hao ni watu waliowasili China wakitokea nchi za nje. Hapa barani Ulaya, Uingereza huenda ikalazimika kutangaza sheria ya watu kutotembea nje wala kusafiri ili kuzuia kuendelea kusambaa kwa virusi hivyo.

Hatua hiyo huenda ikachukuliwa ikiwa wananchi hawatozingatia ushauri uliotolewa na serikali kujiepusha kukaa kwenye mikusanyiko, onyo hilo limetolewa Jumapili na waziri mkuu Boris Johnson. Nchini Ugiriki nako serikali imeshatangaza sheria ya kuwataka watu wabakie majumbani kuanzia leo Jumatatu.

Uhispania kwa upande wake imeamua kuongeza muda wa hali ya dharura ya kuwazuia watu kutotembea mitaani hadi Aprili 11. Uhispania ni nchi ya pili barani Ulaya inayoshudia hali mbaya kabisa ya maambukizi ya virusi vya Corona ambapo kufikia Jumapili waliokufa nchini humo ni zaidi ya 1,700.

Hapa nchini Ujerumani idadi ya waliothibitishwa kuambukizwa virusi hivyo imeongezeka hadi watu 22,672 na 86 wamefariki, hiyo ni takwimu iliyotangazwa leo Jumatatu na taasisi ya afya ya umma nchini  ya Robert Koch.

Ama nchini Marekani rais Donald Trump ameagiza kuandaliwe maelfu ya vitanda vya dharura vya hospitali katika vituo maalumu vya kupokea walioambukizwa virusi vya Corona lakini mpango wa uokozi wa kiuchumi wa dolla trilioni umegonga mwamba wakati vifo vinavyosababishwa na janga hili vikiongezeka duniani. 

Baraza la Seneti liliupiga chini mpango huo jana ingawa bado mazungumzo yanaendelea. Katika eneo la Mashariki ya Kati Iran ambayo ndiyo iliyoko katika hali mbaya zaidi imeitaka Marekani kuiondolea vikwazo ili iweze kukabiliana na kusambaa kwa virusi hivyo. Rais  Hassan Rouhani leo ametowa ujumbe huo akisema Iran haina nia ya kupokea msaada wowote wa kibinadamu kutoka Marekani. Iran ina mashaka na Marekani na kiongozi wake wa juu Ayatollah Ali Khamenei akisisitiza kilichosemwa na rais Rouhani amesema.

"Sijui kuna ukweli kiasi gani, lakini ikiwa kuna madai hayo je mtu mwenye akili zake anaweza kuwaamini? mnaweza kutoa dawa za kusambaza zaidi virusi au kusababisha virusi visiondoke. Uzoefu wetu unaonesha hamuwezi kuaminika na mnavifanya vitu hivyo.''

Ikumbukwe kwamba siku ya Alhamisi katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutteres alionya kwamba maisha ya mamilioni ya watu yako hatarini ikiwa jumuiya ya kimataifa haitoonesha mshikamano hasa na nchi masikini kufuatia janga hili.