Guterres asema hali ya Gaza "inatisha na haikubaliki"
17 Septemba 2025
Hilo ni baada ya hapo jana Jumanne Israel kuanza operesheni ya ardhini ndani ya mji mkubwa wa ardhi hiyo ya Wapalestina.
Guterres amesema kile kinachoendelea Gaza "kinatisha" akitolea mfano wa uharibifu mkubwa wa makaazi ya Wapalestina na kuongeza kwamba "matendo ya Israel kwenye eneo hilo hayana uhalali na hayavumiliki."
Matamshi hayo ameyatoa wakati jopo huru la uchunguzi la Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limetoa ripoti jana Jumanne iliyohitimisha kuwa Israel inafanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina.
Ripoti hiyo yenye kurasa 72 imeorodhesha ushahidi unaoihusisha moja kwa moja serikali ya Israel na jeshi la nchi hiyo kuwa dhamira ya "kuwaangamiza Wapalestina".
Israel imepuuzilia mbali ripoti hiyo na kuitaja kuwa sehemu ya kampeni chafu ya kulipaka tope taifa hilo la kiyahudi.