George H.W. Bush afariki dunia: Rais aliyeongoza nyakati za kutisha | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.12.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

George H.W. Bush afariki dunia: Rais aliyeongoza nyakati za kutisha

Rais wa zamani wa Marekani George H.W. Bush (94) amefariki dunia. Mwanasiasa huyo aliyeiongoza Marekani mwishoni mwa kipindi cha Vita Baridi atakumbukwa Ujerumani kwa juhudi zake za kuliunganisha bara la Ulaya.

Rais wa zamani wa Marekani George H.W. Bush amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 94, kulingana na taarifa rasmi iliyotolewa Jumamosi.

George H.W. Bush alishika hatamu ya urais mnamo mwaka 1989, baada ya kutumika kama makamu wa rais wakati wa uongozi wa Ronald Reagan. Nchini Ujerumani, atakumbukwa kwa juhudi zake za kuziunganisha Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi mnamo mwkaa 1990. Mwanawe wa kiume George W. Bush pia aliwahi kuwa rais wa Marekani na kutumikia mihula miwili kati ya mwaka 2001 na 2009.

Shujaa wa vita

Alizaliwa mwaka 1924 katika jimbo la Massachusetts. George H.W. Bush alijiandikisha katika Jeshi la Angani la Marekani siku aliyotimiza miaka 18, na baadae aliweka rekodi ya kuwa rubani mdogo zaidi katika jeshi hilo la angani.

Bush alioana na Barbara Pierce mwaka 1945, na baadae mwaka huohuo alimaliza kutumikia jeshi la angani la Marekani na kujiunga na Chuo Kikuu cha Yale. Baada ya kuhitimu masomo yake, yeye na familia yake walihamia katika jimbo la Texas. Kwa msaada wa Rais Richard Nixon, Bush aliteuliwa katika Baraza la Wawakilishi la Marekani mwaka 1966 na mwaka 1971 Nixon alimteua kama balozi wa Marekani kwa Umoja wa Mataifa.

USA: Das ehemalige Präsidentenpaar Barbara und George Bush (picture-alliance/AP Photo/D. J. Phillip)

Rais wa zamani wa Marekani George H.W. Bush akiwa na mke wake Barbara Bush.

Pia aliwahi kuwa mwakilishi wa kwanza wa kidiplomasia wa Marekani nchini China na mkuu wa Shirika la Upelelezi wa Marekani (CIA), kabla ya kuchaguliwa makamu wa rais na hatimaye, mwaka 1988, alichaguliwa kama rais wa 41 wa Marekani.

Aliibuka kutoka katika kivuli cha Reagan

Bush alijaribu kugombea urais kupitia tiketi ya chama cha Republic mwaka 1980. Licha ya kushindwa katika kinyang'anyiro hicho, mwanasiasa mwenzake wa chama cha Republican Ronald Reagan alimchagua kuwa mgombea wake mwenza. Uzoefu wake wa sera za kigeni wakati wa Vita Baridi dhidi ya Umoja wa Kisovyeti ulimsaidia katika kuteuliwa huko.

Baada ya miaka minane kama makamu wa rais wa Reagan, Bush alijaribu kwa mara nyingine tena kugombea urais mwaka 1989, na kushinda uteuzi wa chama cha Republican na baadae kushinda katika uchaguzi wa rais wa Marekani - na kuwa rais wa kwanza katika miaka 152 kuteuliwa baada ya kushika wadhifa wa makamu wa rais. Bush alimshinda mpinzani wake, Gavana wa jimbo la Massachusetts Michael Dukakis kwa asilimia 54 ya kura zote zilizopigwa.

Mtetezi wa umoja wa Ujerumani

Bush aliapishwa kama rais wa Marekani Januari 20, 1989. Katika hotuba yake, alitangaza kwamba "Siku ya dikteta imefikia mwisho" - na baadaye mwaka huo utawala wa Kikomunisti katika nchi tofauti za Ulaya ulipinduliwa na harakati za kidemokrasia, na ndio ukawa mwisho wa Vita Baridi. Umoja wa Kisovyeti tu ndiyo ulisalia - nao pia ukaondolewa kwenye ramani ya dunia miaka miwili baadaye - na kutokana na uwezo wake wa kidiplomasia Bush aliweza kumshawishi kiongozi wa Kisovyeti Mikhail Gorbachev.

Germany Berlin Wall (AP)

George H.W. Bush akiwa na kiongozi wa mwisho wa Kisovyeti Mikhail Gorbachev na Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl.

Hatua hiyo ilikuwa muhimu sana katika kulishughulikia suala la kuungana kwa Ujerumani, ambalo lilikuwa na uwezekano baada kufunguliwa kwa Ukuta wa Berlin mwezi Novemba. Bush ambae alikuwa miongoni mwa watu wa awali waliounga mkono muungano wa Ujerumani, alifanikiwa kutuliza hofu za Gorbachev juu ya suala la muungano wa Ujerumani Mashariki na Magharibi. Matokeo yake, makubaliano yakasainiwa mwaka 1990 kati ya pande mbili za Ujerumani na washindi wa Vita vya Pili vya Dunia ambao ni Uingereza, Ufaransa, Umoja wa Kisovyeti na Marekani. Makubaliano hayo yalisafisha njia na pande mbili za Ujerumani zikaweza kuungana, kurejeshwa kwa uhuru kamili wa Ujerumani, kubaki kama mwanachama wa NATO na kuondolewa kwa wanajeshi wa Kisovyeti nchini humo.

Baada ya kuungana tena kwa Ujerumani Mashariki na Magharibi mnamo Oktoba 3, 1990, Bush alisema, "Ninampongeza Kansela Kohl na watu wa Ujerumani Mashariki na Magharibi pamoja na watu wa mji wa Berlin, waliogawanywa kwa muda mrefu, na kwa kuweza kufanikisha ndoto yao ya kuwa na uhuru wa kitaifa."

Vita vya Iraq 1991

Bush alitumia nguvu ya kijeshi na kuamuru uvamizi wa Panama na kumtia mbaroni kiongozi wake aliedaiwa kuhusika na madawa ya kulevya, Manuel Noriega, Desemba 1989. Mwaka uliofuata, baada ya Iraq kuivamia Kuwait, Bush aliunda muungano wa Umoja wa Mataifa chini ya uongozi wa Marekani ambao haukuwahi kushuhudiwa uliojumuisha mataifa kadhaa ya Kiarabu. Saddam Hussein alipokataa kuondoa wanajeshi wake Kuwait, Vita vya Ghuba, vilivyopewa jina la 'Operation Desert Storm', vilianza Januari 1991.

Licha ya kupata umaarufu wa asilimia 90 miongoni mwa raia baada ya kumalizika kwa Vita vya Ghuba, umaarufu huo ulipotea haraka baada ya Bush kushindwa kushughulikia masuala mazito ya ndani ya nchi huku uchumi ukiwa unaporomoka nchini humo.

Jan 20 1989 Washington DC United States of America U S President George H W Bush takes the (imago/ZUMA Press)

Januari 20, 1989 Washington DC Rais wa Marekani George H.W. Bush akiapishwa urais.

Kushindwa na Clinton

Bush alishindwa na Bill Clinton katika uchaguzi wa rais wa mwaka 1992,  kwa sababu alikubali kuongezwa kwa kodi ya petroli, kuongezewa kodi watu wa kipato cha juu pamoja na kupandishwa viwango vya ushuru kwenye vitu vya anasa licha ya ahadi yake ya wakati wa uchaguzi ya "kutoongeza kodi mpya." Clinton alimlaumu kwa kuanguka kwa uchumi wa nchi, kukua kwa pengo kati ya matajiri na maskini pamoja na deni la kitaifa.

Baada ya kushindwa na Clinton, Bush alijitoa kutoka katika siasa na kuhamia mjini Houston na mke wake Barbara, ambako aliishi hadi kifo chake. Mara kwa mara alisema hakuwa akitamani kurudi katika siasa wala kuandikwa katika vyombo vya habari. Mtoto wake wa kiume George W. Bush, mmoja wa watoto wake sita, aliwahi kuwa gavana katika jimbo la Texas na kuchaguliwa kama rais wa Marekani katika uchaguzi wa mwaka 2000. Mtoto wake mwengine, Jeb Bush, pia aligombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican mwaka 2015, lakini alishindwa na Donald Trump.

George H.W. Bush, George W. Bush und Jeb Bush (picture-alliance/dpa/M. Cavanaugh)

George H.W. Bush, akiwa na watoto wake George W. Bush na Jeb Bush

Kutambuliwa kimataifa

Hata baada ya miaka kadhaa tokea kuwa rais, Bush alitunukiwa tuzo kadhaa. Mwaka 2008, alitunukiwa tuzo ya Henry Kissinger mjini Berlin kwa mchango wake katika makubaliano ya kibiashara ya trans-Atlantic. Mwaka 2011, Rais Barack Obama alimtunukia Medali ya Rais ya Uhuru - ambayo ni tuzo ya heshima kubwa zaidi nchi Marekani anayopewa raia wa kawaida.

Mwandishi: Simon Bone, Daniel Scheschkewitz, Stephanie Höppner/DW

Tafsiri: Yusra Buwayhid

Mhariri: Sylvia Mwehozi

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com