1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

EU yakubaliana kutoa euro bil. 5 kuinunulia silaha Ukraine

Iddi Ssessanga
14 Machi 2024

Mataifa wanachama ya Umoja wa Ulaya yamekubaliana kuongeza euro bilioni 5.5 kwenye mfuko wa pamoja ili kulipia silaha zinazotumwa Ukraine. Mataifa ya Ulaya yametoa ufadhili wa jumla wa euro bilioni 28 kwa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4dVGv
Brussels | Halmashauri Kuu ya EU| Bendera za EU na Ukraine
Ukraine imesogea zaidi upande wa Umoja wa Ulaya tangu uvamizi wa Urusi, ikipewa hadhi ya mwanachama mgombea.Picha: Lukasz Kobus/European Commission

Hatua hiyo inaiimarisha Kyiv wakati ambapo msaada kutoka mfadhili wake mkuu Marekani ikiyumba na vikosi vyake vikipambana kuizuwia Urusi.

Ubelgiji, ambayo ndiyo inashikilia urais wa mzunguko wa Umoja wa Ulaya, imesema mabalozi kutoka mataifa 27 wanachama walikuwa wamekubaliana kimsingi juu ya mpango wa kuifadhili Kyiv mwaka huu wa 2024 kwa kiasi cha euro bilioni tano.

Hii ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Ulaya kukubali kufadhili ununuzi wa silaha kwa ajili ya taifa lililoko vitani.

Soma pia: Vita vya Urusi na Ukraine vimeingia mwaka wa tatu sasa

Tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi mwaka 2022, jumuiya hiyo imetoa euro bilioni 6.1 kutoka mfuko wake wa amani kurejesha gharama za silaha zilizotumwa na wanachama kwa Ukraine.

Bunge la Ulaya likijadili juu ya watoto wa Ukraine waliohamishiwa nchini Urusi.
Bunge la Ulaya likijadili juu ya watoto wa Ukraine waliohamishiwa nchini Urusi.Picha: Alexis HAULOT/European Union 2024

Kwa ujumla tangu kuanza kwa vita vya Urusi nchini Ukraine, Brussels inasema takribani euro bilioni 28 zimetumika kutoka mataifa wanachama na hazina ya EU kulisaidia jeshi la Ukraine.

Tangazo hilo la ufadhili wa karibuni zaidi kwa ajili ya Ukraine limekuja wakati ambapo vikosi vya Kyiv vinakabiliwa na shinikizo kwenye kwenye uwanja wa vita kutokana na uhaba wa risasi na makombora.

Urusi yazidisha mashambulizi kote Ukraine

Usiku wa kuamkia Alhamisi, vikosi vya Urusi vimefanya mashambulizi kadhaa ya droni dhidi ya mikoa ya nchi hiyo ambayo mamlaka zimesema yalilenga miundombinu ya kiraia.

Gavana wa mkoa wa mashariki wa Kharkiv Oleh Synehubov, amesema kupitia chaneli ya Telegram kwamba ukarabati ulikuwa unaendelea baada ya miundombinu ya televisheni kushambuliwa, lakini hakutoa ufafanuzi.

Soma pia:Vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwa Urusi vinatekelezwa?

Mamlaka katika mkoa jirani wa Sumy zimesema miundombinu katika miji minne ilishambuliwa kwa droni zilizotengenezwa Iran. Jeshi la Ukraine limesema liliangusha droni 22 kati ya 36 zilizotumwa na Urusi usiku.

Kurutu wa jeshi la Ukraine akiwa mazoezini
Kurutu wa jeshi la Ukraine akiwa mazoeziniPicha: Viacheslav Ratynskyi/REUTERS

Akizungumzia mashambulizi hayo ya Urusi, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alisema katika hotuba yake ya usiku, kwamba kila mmoja anapaswa kufanya juhudi kuhakikisha watu wanaoteseka hawaachwi peke yao na maumivu.

"Na haijalishi nini kitatokea, kutakuwa na msaada katika kila kona ya nchi yetu. Hiki ndicho hasa kinachohitajika," alisema Zelenskiy.

Wakati huo huo, mamlaka ya usimamizi wa mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia inayodhibitiwa na Urusi imesema jeshi la Urusi limeshambulia miundombinu nyeti katika mtambo huo.

Soma pia: Vita Ukraine: Uchumi wa Urusi wasalia imara licha ya vikwazo

Kiwanda hicho kimeripoti kuwa kifaa cha mlipuko kilidondoshwa karibu na ukuta yaliko matenki ya mafuta, na kuongeza kuwa mashambulizi kama hayo hayakubaliki. Hata hivyo haikuwa wazi lini hasa shambulio hilo lilitokea.

Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la nishati ya atomiki Rafael Grossi, amekuwa akionya mara kwa mara juu ya hatari za mashambulizi dhidi ya kiwanda hicho cha nyuklia, ambacho ndiyo kikubwa zaidi barani Ulaya.

Chanzo: Mashirika