China yatishia kuilipizia kisasi Marekani kuiunga mkono Hong Kong | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.11.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

China yatishia kuilipizia kisasi Marekani kuiunga mkono Hong Kong

China Alhamisi imetishia kulipiza kisasi baada ya Marekani kupitisha sheria ya kuunga mkono vuguvugu la kupigania demokrasia mjini Hong Kong, katika wakati mataifa hayo yakiwa na mzozo wa kibiashara.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China amemuita balozi wa Marekani nchini China, Terry Branstad, kuwasilisha malalamiko rasmi, saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusaini miswada miwili na kuwa sheria ambayo inaunga mkono waandamanaji wanaopigania demokrasia Hong Kong. Serikali ya Hong Kong kwa upande wake imesema imesikitishwa sana na hatua ya Trump.

Akisaini miswada hiyo miwili hapo jana, Trump amesema ameamua kuchukua hatua hiyo kwa kuwa anamheshimu Rais Xi Jinping, China na watu wa Hong Kong.

Mwanaharakati anayepigania demokrasia katika vuguvugu hilo la Hong Kong Joshua Wong amesema sheria hiyo ya kuiunga mkono Hong Kong iliyotiwa saini na Rais Donald Trump inatoa ujumbe wazi kwa serikali ya China.

"Rais Donald Trump amesaini muswada huo ili kuwaongozea nguvu ya mapatano wakazi wa  Hong Kong. Hatujali.. mimi sio chombo cha kutumiwa na kiongozi yoyote wa ulimwengu. Na sijali kabisa ikiwa kweli, kwenye mioyo yao, wanataka kuisaidia Hong Kong. Tunataka tu mambo yafanyike," amesema Wong.

Hong Kong | Proteste | Polytechnic University (Getty Images/AFP/D. de la Rey)

Wakazi wa Hong Kong wakiandamana Novemba 25

China yaitaka Marekani kutoingilia mambo yake 

Sheria hiyo ambayo iliungwa mkono kwa sauti moja bungeni, inahitaji Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kuthibitisha angalau kila mwaka kwamba uhuru wa Hong Kong haukutatizwa.

Bunge la Marekani pia limepitisha muswada wa pili - ambao Rais Trump pia ameusaini - unaopiga marufuku usafirishaji na uuzaji wa silaha za kudhibiti maandamano ya umma kwa vikosi vya usalama vya Hong Kong kama vile, mabomu ya kutoa machozi, dawa ya pilipili, risasi za mpira pamoja na bunduki za kutoa mshtuko wa umeme.

China ilimuonya Trump wiki iliyopita kuwa itachukua hatua za kulipiza kisasi iwapo atasaini miswada hiyo na kuwa sheria.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China Le Yucheng ameitaka Marekani kujizuia kutekeleza sheria hiyo kwa vitendo na kuacha kuingilia kati mambo ya ndani ya Hong Kong na China.

China na Marekani zinavutana katika mgogoro wa kibiashara, bila ya kupatikana suluhisho la maana katika siku za usoni. Miswada hiyo miwili ya kuiunga mkono Hong Kong inaweza kuikasirisha zaidi China.

Vyanzo: (dpa,afp)

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com