1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cameron aanza kuwakera wanachama wa EU

30 Desemba 2014

Mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya EU, yanaonekana kuanza kuchoshwa na vitisho vya Uingereza kujitoa katika umoja huo, kutokana na madai ya waziri mkuu David Cameron kutaka kubadilisha kanuni za msingi wa umoja huo.

https://p.dw.com/p/1ECGF
Waziri mkuu Cameron alipotoa hotuba yake kuhusu EU katika kiwanda cha mitambo mikubwa cha JCB World mjini Rocester, 28.11.2014.
Waziri mkuu Cameron alipotoa hotuba yake kuhusu EU katika kiwanda cha mitambo mikubwa cha JCB World mjini Rocester, 28.11.2014.Picha: Reuters/O. Scarff

Wakati king'ora cha kuashiria moto kilivyokatiza hotuba kubwa ya waziri mkuu David Cameron kuhusu Ulaya katika kiwanda kikubwa cha kutengeneza mitambo mwezi Novemba 2014, alitania kuwa hadhira yake ilikuwa ikisikia kengele zikilia mjini Brussels kuhusiana na uwezekano wa Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya.

Ukosoaji wa Umoja wa Ulaya ni jambo linalopokelewa vyema nchini Uingereza, ambako chama kinachoupinga umoja huo cha UK Independent UKIP, kilijizolea ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge la Ulaya mapema mwaka 2014.

Shinikizo la kisiasa

Akikabiliwa na shinikizo kutoka kwa wapinzani wa Umoja wa Ulaya ndani na nje ya chama chake, waziri mkuu Cameron ameahidi kura ya maoni kuamua ama kubakia au kutoka ndani ya umoja huo mwaka 2017, ikiwa atachaguliwa tena kuliongoza taifa hilo mwezi Mei mwaka 2015. Wakati akisema angependa kuona Uingereza ikibakia katika umoja wa Ulaya, Cameron amedokeza pia kwamba anaweza kubadilisha msimamo wake ikiwa matakwa muhimu hayatatekelezwa.

Viongozi wa EU wakiwa katika mkutano wao wa kilele mjini Brussels.
Viongozi wa EU wakiwa katika mkutano wao wa kilele mjini Brussels.Picha: picture alliance/AA/D.Aydemir

Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa Waingereza hawana ari ya kuwa katika Umoja wa Ulaya, licha ya nchi hiyo kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo ya kisiasa na kiuchumi kwa miaka 40. Hata uongozi wa chama cha upinzani cha Labour, ambacho hakiahidi kura ya maoni, kinapambana kutoonyesha hisia kali kuhusu umoja huo wenye wanachama 28.

Suala moja muhimu na linalozua tafrani ni kuhusu uhamiaji, na hasa kushindwa kwa Uingereza kuwazuwia wahamiaji wa EU kuingia nchini humo kutokana na kanuni ya umoja huo inayowapa raia wake uhuru wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila kuwekewa vikwazo.

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa raia 228,000 wa Umoja wa Ulaya wamewasili nchini Uingereza kufikia Julai mwaka huu -- hii ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya shabaha ya wahamiaji 100,000 aliyoiahidi Cameron kufikia Mei 2015.

Msimamo usiyoeleweka

Lakini Cameron anatuma ujumbe mchanganyiko kuhusu uanachama wa Umoja wa Ulaya. Wakati chama chake cha Wahafidhina kikipoteza umaarufu kwa chama cha UKIP, wafanyabiashara wengi wanasisitiza umuhimu wa kubaki katika Umoja wa Ulaya, ambao unatoa fursa makhsusi za kuwafikia walaji wake milioni 500.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anataka UK ibakie katika EU lakini hakubaliani na madai ya Cameron kubadilisha kanuni za msingi za umoja huo.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anataka UK ibakie katika EU lakini hakubaliani na madai ya Cameron kubadilisha kanuni za msingi za umoja huo.Picha: AFP/Getty Images/T. Charlier

Michael Rake, kiongozi wa shirikisho la viwanda la Uingereza, alionya kuwa kuondoka katika Umoja wa Ulaya kutaifanya Uingereza kujifungia nje ya ulimwengu katika wakati ambapo dunia inapitia mabadiliko yasiyozuwilika.

Jambo la muhimu ni kwamba Cameron aliamua kutoa hotuba yake kuhusu Ulaya katika kiwanda cha mitambo mikubwa cha JBC, ambacho pengine hakingekuwepo bila faida za soko la pamoja linalotokana na uanachama wa Umoja wa Ulaya.

Na licha ya kupendekeza kupunguzwa kwa mafao ya kijamii kwa wahamiaji wa EU, Cameron anasisitiza kuwa hataki kuharibu kanuni ya uhuru ya kutoka sehemu moja kwenda nyingine, ambayo Waingereza zaidi ya milioni 1.3 wamenufaika nayo.

Badala yake, mkwara wa Cameron unalenga kuilainisha Brussels kwa kutishia kuiondoa Uingereza katika EU ikiwa hakutakuwa na makubaliano kuhusu masuala muhimu kama vile uhamiaji. Lakini Umoja wa Ulaya umesisitiza msimamo wa kupinga jitihada zozote za kubadili kanuni yake hiyo ya uasisi kuhusu uhuru wa watu kutoka nchi moja kwenda nyingine.

Chini ya uongozi wa Cameron, Uingereza imejikuta ikizidi kukwaruzana na wanachama wengine, kuhusiana na masuala kuanzia uteuzi wa rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claud Juncker, na kura ya turufu ya Uingereza mwaka 2011 kupinga hatua zilizonuwiwa kushughulikia mgogoro wa kiuchumi wa umoja huo. Lakini tabia hii inaonekana kuwachosha wanachama wengine.

Waziri Cameron akiwa na rais wa Halmashauri ya EU Jean-Claud Juncker, ambaye alipinga uteuzi wake bila mafanikio.
Waziri Cameron akiwa na rais wa Halmashauri ya EU Jean-Claud Juncker, ambaye alipinga uteuzi wake bila mafanikio.Picha: picture-alliance/dpa/EU/Creemers

'Cameron anachezea moto'

Mwezi Oktoba, aliyekuwa rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso alionya kuwa Cameron anachezea moto kwa kuchochea hisia za chuki dhidi ya Umoja wa Ulaya, akisema katika mahojiano na televisheni ya France 24 kuwa "huwezi kuikosoa EU kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi, na kuwaomba watu kuipigia kura EU siku ya Jumapili.

Mrithi wake Jean-Claud Juncker, ameahidi kufanya kazi kuibakiza Uingereza katika Umoja wa Ulaya, lakini mataifa mengi hayako tayari kubadili mikataba ya EU kwa lengo la kubadili sheria za msingi za uanachama, yakihofia kuwa kufanya hivyo kunaweza kusababisha matatizo mengine yasiyotarajiwa. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aliripotiwa kukosa uvumilivu pale Cameron alipozungumzia kuanzisha ukomo wa wahamiaji - hatua ambayo aliamua kutoichukuwa wakati akibainisha mipango yake ya kupunguza uhamiaji.

Wengine wanaona katika mtazamo wa Uingereza, ukaida wa kudumu wa kuachana na historia yake ya zamani, ilipokuwa taifa lenye nguvu kubwa duniani, lenye mahusiano maalumu na Marekani, na pia njozi ya ufahari wa utamaduni wake ulioanzishwa karibu miaka 2000 iliyopita, na ambao sasa unatishiwa na wale wanaowachukulia kuwa ni washenzi wanaomiminika nchini mwao.

Mwandishi: Iddi Sessanga/dpae
Mhariri: Jopsephat Nyiro Charo