1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bendera ya Palestina Yapepea Umoja wa Mataifa

Admin.WagnerD11 Septemba 2015

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinisha hatua ya kuruhusu bendera ya Mamlaka ya Wapalestina kupeperushwa mbele ya makao makuu ya umoja huo kama ishara ya kukubalika kwa ombi la kuwepo dola la Wapalestina.

https://p.dw.com/p/1GUyW
Bendera ya Palestina
Bendera ya PalestinaPicha: Getty Images/C. Furlong

Nchi 119 zimepika kura ya kuunga mkono hatua hiyo ya kuiruhusu bendera ya wapalestina kupeperushwa mbele ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani huku nchi 45 zikijizuia kupiga kura yoyote. Azimio hilo la jana linatoa nafasi ya nchi waangalizi katika Umoja wa Mataifa kupeperusha bendera zao sambamba na nchi 193 wanachama wa Umoja huo.

Na kwa hivyo hatua hiyo ya kuidhinishwa kwa azimio hilo imezifanya Palestina pamoja na makao makuu ya Kanisa Katoliki - Vatican ambazo sio wanachama wa Umoja wa Mataifa bali waangalizi kwa mara ya kwanza kupata nafasi hiyo ya kupeperusha bendera zao katika Umoja huo.

Vatican yasubiri ziara ya Papa

Hata hivyo Vatican kwa upande wake imekataa hapo jana kupeperusha bendera yake mbele ya makao makuu hayo ya Umoja wa Mataifa ikisema haiwezi kuchukua hatua hiyo hadi pale kiongozi wa kanisa hilo Papa Francis atakapozuru Umoja wa Mataifa mwezi huu. Lakini kwa wapalestina licha ya kukwama kwa mazungumzo ya kutafuta amani na waisraeli ili ipatikane suluhusu ya kuundwa dola lao, hatimae wamefanikiwa kupata alau heshima ya kutambulika kama dola mbele ya Umoja huo wa Mataifa.

Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas akihutubia katika Umoja wa Mataifa
Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas akihutubia katika Umoja wa MataifaPicha: AFP/Getty Images

Ikumbukwe kwamba baraza kuu la Umoja huo wa Mataifa liliidhinisha mwaka 2012 kuipandisha hadhi Palestina kutoka kuwa taifa mwangalizi hadi kuwa taifa muangalizi lisilokuwa mwanachama wa Umoja huo.Hatua hiyo ilifikiwa baada ya nchi 138 kupiga kura kuunga mkono azimio hilo na nchi 9 kulipinga.

Hatua ya kihistoria

Kufuatia hatua hiyo hatimae Wapalestina wakapata nafasi ya kujiunga na mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo lile la elimu sayansi na utamaduni UNESCO pamoja na mikataba chungu nzima ikiwemo ule wa Roma uliounda mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita mjini The Hague, ICC. Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour ameipongeza hatua ya kihistoria iliyochukuliwa na baraza kuu la Umoja huo akisema ni hatua nyingine kuelekea kutimia kwa ahadi waliyopewa wapalestina kiasi miongo saba iliyopita ya kupata uhuru wao.

Balozi huyo alisema wiki iliyopita kwamba wapalestina wangependa kumuona rais wao Mahmoud Abbas akipeperusha bendera yao baada ya kukihutubia kikao cha hadhara kuu ya Umoja huo mnamo septemba 30, kikao ambacho kimsingi kinafanyika kila mwaka mjini New York kikiwakutanisha viongozi wa dunia. Balozi wa Israel katika Umoja huo wa Mataifa Ron Prosor amelitaja lengo la azimio hilo kuwa ni kichekesho akisema halitofanikisha malengo ya kupatikana amani katika eneo hilo ingawa anataraji kuona hilo linatokea.

Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/dpa/P. Foley

Marekani na Israel zinapinga hatua ya kutambuliwa kwa dola la wapalestina zikidai kwamba ni hali inayohujumu juhudi za mazungumzo ya kutafuta makubaliano ya amani. Nchi nyingine zilizopinga azimio hilo ni Canada, Australia na nchi nyingine za visiwa vidogo, wakati Ulaya ikiwa imegawika, Ufaransa, Italia, Uhispania Sweden na Poland ni miongoni mwa zilizounga mkono wakati Ujerumani Uingereza na mataifa ya Baltic yakijizuia kupiga kura.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Daniel Gakuba.