Ban Ki-Moon asema ″hana matumaini″ | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ban Ki-Moon asema "hana matumaini"

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ametoa tathmini kuhusu matarajio ya kutuliza ghasia kati ya Waisrael na Wapalestina, akisema hana matumaini, baada ya kukutana na viongozi wakuu wa pande zote.

Katibu Mkuu Ban alikiambia kikao cha dharura cha baraza la usalama kwa njia ya video kutoka mjii mkuu wa Jordan Amman, kwamba kuna pengo kubwa sana kati ya pande mbili kuhusu upunguzaji wa mgogoro katika kipindi cha muda mfupi, na kurudi tena kwenye meza ya mazungumzo katika kipindi cha muda mrefu.

Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Matthew Rycroft alisema katibu mkuu Ban alielezea haja kwa wote wenye ushawishi kuutumia kutuliza hali inayozidi kuwa mbaya kila uchao, na kuongeza kuwa ni muhimu kwa jamii ya kimataifa na hasa baraza la usalama kutumia kila lililomo ndani ya uwezo wake kukomesha vurugu hizo.

Katibu Mkuu Ban Ki-Moon akiwa na rais wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas mjini Ramallah.

Katibu Mkuu Ban Ki-Moon akiwa na rais wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas mjini Ramallah.

Maelezo ya Ban yalitolewa sambamba na uamuzi wake wa kutuma waraka wenye kurasa 42 kwa Umoja wa Mataifa, kuhusu matukio ya kihistoria katika ulinzi wa watu, ambao uliandaliwa nasekriteriate ya Umoja wa Mataifa, katika kujibu barua ya Julai 21, 2014 kutoka kwa Rais wa Palestina mahmoud Abbas, akiomba kuwa ardhi ya taifa la Palestina iwekwe chini ya mfumo wa ulinzi wa kimataifa na Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kuhakikisha ulinzi wa Wapalestina.

Merkel asisitiza suluhisho la mataifa mawili

Machafuko ya sasa yalianza mwezi uliyopita kufuatia makabiliano katika eneo takatifu mjini Jerusalem linalojulikana kama Haram Sharif kwa Waislamu na Temple Mount kwa Wayahudi. Katika mkutano na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu jana Jumatano, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, alisisitza umuhimu kwa pande zote kuchangia kutuliza hali.

"Kwa mtazamo wangu, na nimelisema hili mara nyingi kwamba kuhusiana na suala la mataifa mawili, tunachukulia ujenzi wa makaazi ya walowezi kuwa kinyume na matarajio. Tunahitaji kufanya kila kitu kutuliza hali, na katika moyo huo nadhani kila upande unapaswa kutoa mchango," alisema Merkel.

Hadi sasa Netanyahu hajaonyesha nia hasa ya kufikia muafaka. Alipokutana na katibu mkuu Ban siku ya Jumanne, alimkosoa vikali rais Abbas kwa kile alichodai anachochea mgogoro, na kukanusha madai kuwa Israel inatumia nguvu iliyopitiliza.

Mashirika ya haki za binaadamu yanasema wanajeshi wa Israel na walowezi wa Kiyahudi wamewauwa watoto wa Kipalestina.

Mashirika ya haki za binaadamu yanasema wanajeshi wa Israel na walowezi wa Kiyahudi wamewauwa watoto wa Kipalestina.

Alirejea madai hayo mjini Berlin katika mazungumzo yake na Kansela Merkel akisema, "ikiwa tunataka amani, tunapaswa kukomesha ugaidi. Na ili tukomeshe ugaidi tunapaswa kuacha ucochezi."

Israel yauwa watoto

Lakini makundi ya haki za binaadamu yamesisitiza katika ripoti yao iliyotolewa leo, kuwa Israel inatumia nguvu iliyopitiliza hata dhidi ya watoto wa Kipalestina, ambapo katika mgogoro wa sasa watoto wasiopungua 10 wameuawa.

Kulingana na ofisi ya kuratibu shughuli za haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa, kati ya Oktoba 6 na 12, watoto 201 wa Kipalestina wamejeruhiwa na wanajeshi wa Israel au walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi na ukanda wa Gaza.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,dpae,rtre.

Mhariri: Oummilkheir Hamidou.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com