1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSaudi Arabia

Assad akaribishwa katika Jumuiya ya nchi za Kiarabu

Daniel Gakuba
19 Mei 2023

Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2011, rais wa Syria Bashar al-Assad anashiriki katika mkutano wa kilele wa jumuiya ya nchi za Kiarabu unaofanyika Saudi Arabia. Rais Volodymyr Zelenskiy pia amealikwa katika mkutano huo.

https://p.dw.com/p/4RaUe
Gipfel der Arabischen Liga | Rückkehr Syriens in die Arabische Liga
Rais Bashar al-Assad (mwenye suti nyeusi) akikaribishwa na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia Arabia, Mwanamfalme Mohammed Bin Salman mjini JeddahPicha: Al Ekhbariya Tv/REUTERS

Wakati viongozi wakuu wa mataifa ya kiarabu walipokuwa wakiingia katika ukumbi wa mkutano mchana huu, Rais Bashar al-Assad alionekana akizungumza na Rais wa Misri Abdel Fattah-al Sisi, na katika hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo wa kilele, waziri mkuu wa Algeria Ayman Benebderrahmane amesema, kwa sauti kubwa anamkaribisha Rais Assad miongoni mwa ndugu zake.

Soma zaidi:  Assad wa Syria kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Kiarabu

Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, mwanamfalme Mohammed bin Salman pia amesema amefurahishwa na kushiriki kwa Rais Assad katika mkutano huo wa kilele, na kuongeza kuwa anayo matumaini kuwa hatua hiyo italeta utengamano nchini Syria.

Barabara za mitaa ya mji wa Jeddah unakofanyika mkutano huo wa kilele zinapepea bendera za mataifa wanachama, ya Syria ikiwemo, na gazeti la al-Riyadh limebashiri kuwa huu utakuwa mama wa mikutano yote ya kilele.

Ägypten «Vollwertiges Mitglied»: Assad-Regierung zurück in Arabischer Liga
Hii ni mara ya kwanza tangu mwaka 2011 kwa bendera ya Syria kupepea katika mkutano wa Jumuiya ya Mataifa ya KiarabuPicha: Ahmed Gomaa/Xinhua/picture alliance

Mitazamo mseto miongoni mwa wananchi wa Kiarabu

Maoni ya wananchi wa kawaida juu ya kukaribishwa tena kwa Syria yamechanganyika, baadhi wakikosoa, na wengine kama Naim Ibrahim mbaye ni mfanyakazi raia wa Syrua, wakiiona hatua hiyo kama yenye kuleta matumaini.

''Kimsingi nadhani ni mkutano wa kilele kati ya Syria na Saudi Arabia. Nchi mbili zina historia ndefu na ushawishi wa kisiasa na kidiplomasia, na uwezo wa kushawishi matukio katika ulimwengu wa kiarabu na wa kimataifa,'' amesema Ibrahi na kuongeza kuwa ndio sababu anafurahia mkutano huu kati ya viongozi wa kiarabu, kwa matumaini kuwa utakuwa wenye tija kwa ulimwengu wa kiarabu, na kwa Syria kwa hali ya kipekee.''

Soma zaidi: Rais wa Syria aalikwa katika mikutano mikuu miwili

Mkutano huu unafanyika wakati Saudi Arabia ikiwa katika juhudi kubwa za kidiplomasia, zilizoanza na makubaliano ya kurejesha uhusiano na hasimu wake kikanda, Iran kufuatia upatanishi wa China. Mbali na Iran na Syria, Saudi Arabia ambayo siku za nyuma ilikuwa kwa sehemu kubwa ikifuata maelekezo ya Marekani, inahusika pia katika mipango ya kutafuta amani nchini Sudan.

Saudi-Arabien | Ankunft Wolodymyr Selenskyj in Dschidda
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy pia amekaribishwa katika mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Mataifa ya KiarabuPicha: Saudi Press Agency/REUTERS

Qatar bado haijaikumbatia Syria

Hata hivyo, sio mataifa yote ya Kiarabu yamemkaribisha Rais Bashar al-Assad kwa mikono miwili, Qatar kwa mfano ilitangaza mwezi huu kuwa haitorejesha mahusiano ya kibalozi na Syria, lakini ikaweka bayana kuwa hilo halingezuia kurejeshwa kwa nchi hiyo katika jumuiya ya mataifa ya Kiarabu. Hata hivyo, kulingana na vyombo vya habari vya Syria, Rais Assad alipeana mkono na kuongea na kiongozi mkuu wa Qatar  Sheikh Tamim bin Hamad Al-Thani kabla ya wote wawili kuingia katika ukumbi wa mikutano.

Soma zaidi: Ujerumani haioni sababu ya kurejesha uhusiano na Syria

Mkutano huo wa kilele wa jumuiya ya nchi za Kiarabu umemshirikisha pia rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy, ambaye katika hotuba yake amezikosoa nchi wanachama wa Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu ambazo bado hatijalaani uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, na kuzitaka kufikiria kwa makini kinachoendelea katika vita hivyo.

Vyanzo: afpe, dpae