1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Hukumu ya kifo yapungua ulimwenguni

Lilian Mtono
21 Aprili 2021

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limesema kwenye ripoti yake kwamba idadi ya hukumu za kifo kwa mwaka 2020 ilipungua, ingawa baadhi ya mataifa yaliiendeleza.

https://p.dw.com/p/3sKoW
USA Todesstrafe Virginia
Picha: Steve Helber/AP Photo/picture alliance

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limesema kwenye ripoti yake kwamba idadi ya hukumu za kifo kwa mwaka 2020 ilipungua. Hata hivyo baadhi ya mataifa yaliendelea kutekeleza hukumu hiyo kwa wingi licha ya janga la virusi vya corona. 

Ripoti hiyo iliyochapishwa Jumatano na shirika la Amnesty International imeonyesha kupungua kwa hukumu za vifo kwa mwaka 2020. Ingawa shirika hilo limesema bado baadhi ya mataifa yaliendelea kutoa hukumu hiyo na hata idadi yake iliongezeka.

Soma Zaidi: 2015 yavunja rekodi kwa adhabu za vifo zilizotekelezwa 

Katibu mkuu wa shirika hilo Agnes Callamard amenukuliwa akisema licha ya mataifa hayo kuendelea kutoa hukumu ya kifo, bado jumla kuu ya mwaka 2020 ilikuwa ni ya kuridhisha. Amesema idadi ya hukumu za vifo zilizorekodiwa iliendelea kupungua, na kufanya ulimwengu kukaribia kuachana na adhabu hiyo ya kikatili na isiyo ya kibinaadamu.

Idadi imeshuka zaidi katika muongo mmoja.

Takriban hukumu 483 za kifo zilitolewa kote ulimwenguni kwa mwaka 2020, hii ikiwa ni kulingana na ripoti hiyo, ambayo ni ya chini kabisa kurekodiwa na Amnesty International kwa karibu miaka 10. Kwa kipindi kama hicho, hata hivyo hukumu hiyo iliongezeka mara tatu nchini Misri, India, Oman, Qatar na Taiwan, liyorejesha hukumu hiyo.

Utawala wa zamani wa Donald Trump nchini Marekani pia ulitekeleza hukumu ya kifo kwenye majimbo baada ya kusimamishwa kwa miaka 17, huku watu 10 wakihukumu kifo katika kipindi cha miezi sita.

Hukumu ya kifo nchini Saudi Arabia ilipungua kwa asilimia 85, kutoka 184 mwaka 2019 hadi 27 mwaka 2020 na nchini Iraq pia hukumu hiyo ilipungua kwa zaidi ya nusu kutoka 100 mwaka 2019 hadi 45 mwaka jana. Hakukurekodiwa adhabu yoyote ya kifo nchini Bahrain, Belarus, Japan, Pakistan, Singapore na Sudan ambazo kwa pamoja zilikuwa zikitoa hukumu hiyo mwaka 2019.

Symbolbild I Justiz I Todesstrafe
Polisi nchini Marekani wakijiandaa kuwaondoa wanaharakati waliokuwa wakipinga adhabu ya kifo, mnamo waka 2017.Picha: Brendan Smialowski /AFP/Getty Images

China "mhalifu" mkubwa.

China, Korea Kaskazini, Syria na Vietnam zinaiweka adhabu ya kifo kama taarifa ya siri ya taifa, na kwa maana hiyo idadi kamili kuhusiana na hukumu hiyo haijulikani.

China inaaminika kuwaua maelfu ya watu kila mwaka, na kulifanya kuwa taifa linalokabiliwa na uhalifu mkubwa, shirika hilo la Amnesty International limesema.

Soma Zaidi: China yaoongoza katika utoaji hukumu ya kifo duniani

Iran inashika nafasi ya pili kwa zaidi ya hukumu 246, ikifuatiwa na Misri iliyokuwa na hukumu zaidi ya 107, Iraq zaidi ya 45 na Saudi Arabia iliyowahukumu kifo zaidi ya watu 27.

Jumla ya hukumu zilizotolewa kwenye mataifa hayo ya Iran, Misri, Iraq na Saudi Arabia zilifanya asilimia 88 ya hukumu zote za vifo kwa mwaka 2020. 

Ripoti hiyo aidha imesema kwamba mataifa ya eneo la Asia Pacific yaliendelea kukiuka sheria na viwango vya kimataifa ambayo hutoa ushauri dhidi ya kutolewa adhabu ya kifo kwa makosa ya uhalifu zaidi ya mauaji ya kukusudia.

Takriban mataifa 108 yameikomesha adhabu ya kifo na 144 yameitoa kwenye sheria zake. Mwaka jana, Chad iliiondoa adhabu hiyo wakati Kazakhstzan na Barbados zikifanyia mageuzi sheria zake ili kuikomesha hukumu hiyo.

Chanzo: DW