1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
6 Aprili 2018

Magazeti ya Ujerumani yamezingatia kifo cha mpigania uhuru mashuhuri siyo tu nchini Afrika Kusini bali barani Afrika kote,Winnie Madikizela Mandela aliyeaga dunia mapema wiki hii akiwa na umri wa miaka 81.

https://p.dw.com/p/2vdD2
Südafrika Winnie Mandela
Picha: Imago/Gallo Images

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linasema Winnie Madikizela, aliyekuwa mshirika mkubwa na pia mke wa Nelson Mandela, aliwakilisha ndoto za baadhi ya watu wa nchini Afrika Kusini kutokana na  mchango mkubwa alioutoa katika harakati za ukombozi dhidi ya utawala wa  kibaguzi. Hata hivyo  gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kwamba Mama Winnie, kama jinsi alivyoitwa kwa upendo na wafuasi wake, alikuwa na pande mbili tatanishi katika haiba yake. Gazeti  hilo linasema katika upande mmoja Winnie Madikizela Mandela alibeba kifuani moyo  wa kimapinduzi, lakini katika upande mwingine alikabiliwa na tuhuma za kukiuka haki za binadamu. 

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia juu ya mapambano makali ya kugombea ardhi. Gazeti hilo linasema idadi ya wakulima weupe wanaouawa inazidi kuongezeka nchini Afrika Kusini. Na wakati huo huo serikali ya nchi hiyo inatafakari kuitaifisha ardhi bila ya kulipa fidia. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linaeleza kwamba Mikasa ya watu kuvamiwa kwenye sehemu za mashambani na hasa watu weupe, imeongezeka nchini Afrika Kusini. Kati ya mwezi Aprili mwaka 2016 na mwezi Machi mwaka 2017 mikasa hiyo ilongezeka kwa asilimia 22.9 na idadi ya watu waliouawa iliongezeka kwa asilimia 27.5. Mnamo mwaka huu matukio ya watu kuvamiwa yalikuwa 638 ambapo wakulima 74 waliuliwa.

Takwimu za polisi

Kwa mujibu wa takwimu za polisi zilizonukuliwa na gazeti la Frankfurter Allgemeine kati ya mwaka wa 1996 na  2017 wakulima 1700 waliuawa nchini Afrika Kusini na idadi kubwa walikuwa wakulima wa kizungu. Gazeti hilo pia linatilia maanani kuwa rais Cyril Ramaphosa anatafakari kutekeleza ajenda ya watu wenye siasa kali za mrengo wa shoto ya kutaifisha ardhi inayomilikiwa na watu weupe bila ya kulipa fidia.

Suala la kuleta mageuzi katika sera ya ardhi ni nyeti nchini Afrika Kusini. Hata hivyo gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine limeyanukulu matokeo ya utafiti uliofanywa na mtaalamu wa masuala ya siasa James Gibson, unaoonyesha kuwa idadi kubwa ya watu weusi nchini Afrika Kusini wanataka ardhi inayomilikiwa na wazungu itaifishwe. Kwa mujibu wa gazeti la Frankfurter Allgemeine mtaalamu huyo aliwahoji watu 3700, na asilimia 85 walimwambia, kuwa lazima ardhi irudishwe kwa watu weusi. Na sasa kutoka Afrika kusini.

Die Zeit

Katika makala yake gazeti la Die Zeit linasema wasichojua watu barani Ulaya ni kwamba mji mkuu wa Rwanda, Kigali ni msafi kuliko Berlin na pia ni salama zaidi kuliko Vienna, mji mkuu wa Austria. Gazeti la Die Zeit limeyatilia hayo maanani katika muktadha wa kongamano la wataalamu na watafiti wa Afrika, waliokutana na wanasayansi wenzao kutoka sehemu nyingine za dunia. Gazeti hilo linatufahamisha kwamba wataalamu hao walikutana kwa muda wa siku tatu mjini Kigali hivi karibuni ili kutoa ujumbe kuwa bara la Afrika linao wanasayansi wanaotimiza viwango vya kimataifa.

Gazeti la Die Zeit linasema lengo la wanasayansi wa Afrika waliokutana mjini Kigali, ni kusimama kwenye kilele cha maendeleo ya sayansi duniani na siyo tu kuwa maafisa wa miradi ya maendeleo. Die Zeit linatilia maanani kuwa siyo jambo la kushangaza kwamba wataalamu, wanasayansi na watafiti wa Afrika wamekutana katika mji wa Kigali wenye sifa za usafi na usalama ambazo watu barani Ulaya hawazioni katika vyombo vyao vya habari. 

Frankfurter Allgemeine

Shirika la ndege la Ufaransa "Air France" limebainisha kwamba kuna mustakabali mzuri barani Afrika. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine limeripoti kwamba shirika la ndege la Ufaransa linarejea barani Afrika baada ya kuondoka miaka 18 iliyopita. Gazeti hilo linasema wakati nchini Ufaransa kwenyewe migomo inaendelea, ndege za shirika la  "Air France" zitaanza kutua tena kwenye uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA)  jijini Nairobi, Kenya.

Mwandishi:Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Josephat Charo