Afrika katika Magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 15.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani

Janga la ugonjwa hatari wa Ebola latawala kurasa za magazeti ya Ujerumani wiki hii. Hujuma za Boko Haram nchini Nigeria, kiisho cha ugaidi Kenya na wimbi la wakimbizi Uhispania ni miongoni mwa mambo yaliripotiwa pia.

Janga la ugonjwa hatari wa Ebola ambalo lilihanikiza katika magazeti ya Ujerumani wiki hii. "Afya Taabani" limeandika gazeti la Frankfurter Allgemeine na kusema shirika la afya duniani, WHO limetumia mamlaka yake kuutangaza ugonjwa huo kama janga la kiafya la kimataifa. Hii ina maana shirika hilo lina haki kupata na kusambaza taarifa na data kuhusu kuenea kwa ugonjwa, kuyapa fursa kadhaa mashirika ya misaada, kuweka watu karantini, kutangaza mipango ya dharura ya kitaifa, kufutilia mbali kwa uangalifu haki za uhuru wa watu, biashara na kutafuta njia salama za usafiri kwa lengo la kuyalinda maisha ya binadamu.

Kuhusu Ebola gazeti la Süddeutsche Zeitung liliripoti juu ya hatua ya shirika la WHO kuridhia dawa ya majaribio dhidi ya ugonjwa huo, iitwayo ZMapp, kutumika barani Afrika. Mhariri amesema dawa hiyo "Ni majaribio kwa Afrika Magharibi" lakini haijajulikana kama matumzi yake yatakuwa na matokeo gani. Liberia, Sierra Leone na Guinea zimeathiriwa sana na ugonjwa huo huku zaidi ya watu 900 wakiwa wamekufa. Tanzania imethibitisha kisa kimoja cha maambukizi ya Ebola, huku Uganda na Rwanda zikiripoti kisa kimoja cha watu walioshukiwa kuwa na dalili za ugonjwa huo.

Harakati za Boko Haram Nigeria

Gazeti la Neues Deutschland liliripoti kuhusu hujuma za kundi la wanaitikadi kali za kiislamu la Boko Haram nchini Nigeria. Gazeti hilo lilisema katika taarifa yake kwamba kundi hilo haliko peke yake na linapata msaada kutoka ndani na nje ya nchi. Zaidi ya siku 100 tangu kutekwa nyara wasichana zaidi ya 200 wa shule na kundi hilo, bado hakujapatikana ufanisi wowote katika juhudi za kuwakomboa. Bado hawajasaulika, lakini bado matumaini ya wasichana hao kuwa huru ni madogo.

Nigeria Protest Boko Haram Entführung 26.5.2014

Maandamano yalifanyika kutaka wasichana hao waachiwe huru

Gazeti limeendelea kusema kundi hilo linapata msaada kutoka kwa magavana wa baadhi ya majimbo ya Nigeria, ima kwa kutoza fedha kwa ajili ya ulinzi au kupandisha kodi. Kwa upande mmoja Boko Haram inapata pia msaada kwa kitengo cha mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda katika eneo la Maghreb, AQIM, kundi la al Shabaab kutoka Somalia na makundi mengine kama vile Ansar Dine au Vuguvugu la Umoja wa Jihad katika eneo la Afrika Magharibi, MUJAO. Boko Haram pia inapatiwa msaada na wakfu kutoka Qatar na Saudi Arabia zinazopata fedha zake kutokana na biashara ya silaha, dawa za kulevya na biashara ya kuuza binadamu.

Wake wa wanajeshi waandamana Nigeria

Nalo gazeti la Neue Zürcher liliripoti kuhusu maandamanao ya wake wa wanajeshi wa Nigeria kaskazini mwa nchi hiyo kupinga utawala mzima wa jeshi hilo. Wanawake hao walianza kukusanyika Jumatatu wiki hii katika kambi ya jeshi mjini Maiduguri, mji ambao umeshuhudia mashambulizi mengi ya Boko Haram kaskazini mwa Nigeria.

Gazeti hilo limesema kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Nigeria waandamanaji hao waliyazingira malango ya kambi hiyo kuwazuia wanajeshi wasitoke kwenda kushiriki operesheni ya kuukomboa mji wa Gwoza, kiasi kilometa 100 kusini mashariki mwa Maiduguri unaodhibitiwa na wanamgambo wa Boko Haram. Boko Haram iliuteka mji huo ulio karibu na mpaka wa Cameroon, wiki moja iliyopita. Wake hao wa wanajeshi wanalalamika wanajeshi hawana silaha nzuri za kisasa kuliko adui wao na harakati hiyo iliyopangwa yumkini ikawatia waume zao katika hatari ya kupoteza maisha.

Utalii mashakani katika pwani ya Kenya

Mada nyingine iliyoripotiwa katika magazeti ya Ujerumani ni ugaidi katika pwani ya Kenya, ambako watalii wengi wa kigeni hupenda kwenda likizo. Gazeti la Tageszeitung lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema "Mustakabali wa eneo la utalii uko mashakani." Tangu mwezi Juni mwaka huu matukio ya kigaidi yamekuwa yakishuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya pwani, hususan katika kaunti ya Lamu ambako zaidi ya watu 100 wameuwawa. Kundi la al Shabaab lilidadi kuhusika na mauaji hayo, lakini serikali ikawabebesha dhamana wanasiasa wa eneo hilo.

Mpeketoni Kenia Anschlag Massaker

Shambulizi la kigaidi Mpeketoni, kaunti ya Lamu

Mhariri wa Tageszeitung amesema kuna uwezekano sababu zote mbili zina ukweli. kundi la Al Sahabaab lina kitengo chake nchini Kenya kinachojulikana kama al Hijra na kimekuwa kikiwasajili vijana wa Kenya wenye asili ya kisomali, waislamu wa eneo la pwani na vijana kutoka maeneo masikini, kwa miaka kadhaa sasa. Vijana huenda kupigana Somalia na kisha kurejea Kenya wakiwa na silaha hatari na ujuzi wa kupigana vita.

Gazeti hilo limemnukuu Gabriel Dolan, padri wa Ireland na mwanaharakti wa haki za binadamu ambaye amekuwa akiishi Kenya kwa zaidi ya miaka 30, akisema anahofia mashambulizi yatazidi kuongezeka ilimradi serikali haichukui hatua zozote madhubuti kulitatua tatizo la adhi katika pwani ya Kenya, hasa Lamu, au kwingineko.

Wimbi la wakimbizi laweka rekodi Uhispania

Flüchtlinge Gibraltar Cadiz

Wakimbizi katika mlango bahari wa Gibraltar

Gazeti la Frankfurter Allgemeine liliripoti juu ya wimbi kubwa la wakimbizi kusini mwa uhispania. Tangu mwanzo wa wiki hii zaidi ya wakimbizi 2,000 wamevuka mlango bahari wa Gilbraltar bila vibali na kufaulu kuingia Ulaya. Sehemu kubwa walifika pwani ya kusini mwa Uhispania kwa kutumia boti ndogo.

Nalo gazeti la Neue Zürcher kuhusu mada hii lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema "Wengi kuliko ulivyoshuhudiwa kabla" - Mhariri alisema nchini Italia hali ya wasiwasi inaongezeka kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Afrika kaskazini. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu zaidi ya wakimbizi 100,000 wamefaulu kufika Italia. Idadi hii imevunja rekodi na serikali ya Italia imeomba msaada kutoka kwa Umoja wa Ulaya na imetaka sera na sheria za uhamiaji zifanyiwe mageuzi.

Mwandishi: Josephat Charo/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Saumu Yusuf