1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zeleskny amfuta kazi mkuu wa usalama, mwendesha mashitaka

18 Julai 2022

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amewafuta kazi mwendesha mashitaka mkuu na mkuu wa shirika la ujasusi. akiwalaumu kwa kile anachosema ni idadi kubwa ya maafisa wanaoshirikiana na Urusi dhidi ya Ukraine.

https://p.dw.com/p/4EGrD
Ukraine | Wolodymyr Selenskyj in Dnipro
Picha: Ukrainian Presidential Press Office/AP/dpa/picture alliance

Akizungumza kwenye hotuba yake kwa taifa usiku wa kuamkia Jumatatu (18 Julai 2022), Zelensky alisema aliamuwa kuwafuta kazi Mwendesha Mashitaka Mkuu, Iryna Venediktova, na Mkuu wa Usalama wa Taifa, Ivan Bakanov, kwani kumekuwa na kiwango kikubwa cha kesi za uhaini miongoni mwa maafisa usalama wa Ukraine. 

Venediktova alikuwa anaongoza uchunguzi wa Ukraine juu ya tuhuma za matendo ya uhalifu wa kivita na ukatili yaliyotendwa na majeshi ya Urusi katika mji wa Bucha, ulio kando kidogo ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv. 

Katika hali iliyowashangaza wengi, Zelensky aliliambia taifa kuwa ameamuwa kuwavua majukumu yao wawili hao kwa maslahi ya usalama wa nchi. "Kufikia hivi leo, kuna kesi 651 za uhalifu zimeshafunguliwa zinazohusiana na uhaini dhidi ya nchi na shughuli za usaliti zinazofanywa na waajiriwa wa ofisi ya mwendesha mashitaka, taasisi za uchunguzi majimboni, na vyombo vyengine vya dola. Kwenye kesi 198 katika hizo, watu wanaohusika walitajwa kwa shutuma." Alisema kiongozi huyo.

Kiwango cha juu cha uhaini?

Kwa mujibu wa Zelensky, kuna kesi nyengine 60 ambapo maafisa wa usalama wamesalia kwenye majimbo yaliyotwaliwa na Urusi, ambako wanashirikiana na Urusi dhidi ya Ukraine.

Kiongozi huyo alisema kuwa idadi kubwa kama hiyo ya makosa ya uhalifu dhidi ya misingi ya usalama wa taifa na kwamba mashirikiano yaliyoanzishwa baina ya maafisa hao wa vyombo vya usalama vya Ukraine na shirika la ujasusi la Urusi yanazuwa masuali makubwa dhidi ya wakuu wa vyombo hivyo, ambayo lazima wayajibu.

Ukraine Iryna Venediktova und Ivan Bakanov in Kiew
Mkuu wa Ujasusi wa Ukraine Ivan Bakanov (kushoto) na Mwendesha Mashitaka Mkuu Iryna Venediktova kabla ya kufutwa kazi na Rais Volodymyr Zelensky.Picha: Photoshot/picture alliance

Hayo yakijiri, mkuu wa sera za nje za Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, alionya siku ya Jumatatu kwamba hatua za Urusi kuendelea kuzuwia huduma za usafirishaji katika bandari za Ukraine inatishia kupelekea vifo vya mamilioni ya watu kwa njaa ulimwenguni, na hivyo lazima zikomeshwe mara moja.

"Ni suala la kufa na kupona kwa wanaadamu wengi duniani. Na Urusi lazima iongowe mzingiro wake dhidi ya bandari hizo na kuruhusu ngano ya Ukraine kusafirishwa." Borrell aliwaambia waandishi wa habari mjini Brussels.

Wapatanishi kutoka Urusi na Ukraine walitarajiwa kukutana na wajumbe wa Umoja wa Mataifa na Uturuki mjini Istanbul siku Jumatano 20 Julai), kujadiliana juu ya uwezekano wa kukomesha mzingiro wa miezi mitano kwenye bandari za Ukraine.

Tangu Urusi kuivamia Ukraine mwezi Februari, imetwaa baadhi ya bandari za Bahari Nyeusina kuziharibu nyengine kwa mabomu, ikiwemo ya bandari kuu ya ngano ya mji wa Odessa.