Yoweri Museveni aapishwa kwa muhula wa saba
12 Mei 2026
Rais wa Uganda Yoweri Museveni anaanza muhula wa saba madarakani hii leo Jumanne (12.05.2026) huku mjadala mkubwa ukihusu sio lini ataondoka madarakani, bali ni nani atakayemrithi. Macho ya wengi sasa yanaelekezwa kwa mwanawe, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mkuu wa jeshi la Uganda. Muhoozi ndiye aliyesimamia mazoezi ya gwaride la kijeshi kwa ajili ya kuapishwa kwa Museveni mjini Kampala, hatua ambayo wengi wanaiona kama ishara ya kuendelea kuimarika kwa ushawishi wake ndani ya nchi.
Sherehe ya kumuapisha rais Yoweri Museveni inafanyika mjini Kampala lakini wachambuzi wa siasa Uganda wanasema mabadiliko ya uongozi tayari yanaonekana kutokea taratibu ndani ya mfumo wa serikali na jeshi.
Kadri Museveni anavyozeeka, viongozi wengi serikalini wameanza kuonyesha utii wao kwa Muhoozi, jambo linaloonyesha jinsi alivyoanza kuonekana kama mtu mwenye nguvu kubwa kisiasa na kijeshi nchini Uganda.
Mrithi wa Museveni?
Muhoozi Kainerugaba, mwanawe rais Museveni amewahi kusema wazi kuwa ana nia ya kuwa rais wa Uganda siku zijazo. Hata hivyo, safari yake kuelekea urais inaweza kuwa na njia mbili. Njia ya kwanza ni kupitia mabadiliko ya kisiasa yanayoweza kufanyika ndani ya chama tawala cha NRM, ambacho kina viti vingi bungeni. Njia ya pili ni kupitia ushawishi mkubwa wa jeshi katika kipindi cha mpito wa uongozi.
Lakini changamoto kubwa kwa Muhoozi inaweza kuwa uchaguzi wa moja kwa moja dhidi ya viongozi wa upinzani, hasa Bobi Wine, mwanamuziki maarufu na kiongozi wa upinzani ambaye bado anaungwa mkono na vijana wengi nchini humo. Spika wa Bunge la Uganda, Anita Among, tayari ameonyesha wazi kumuunga mkono Muhoozi, akisema wabunge watafanya kila linalowezekana kuhakikisha anafanikisha ndoto yake ya kuwa rais.
Muhoozi mwenye umri wa miaka 52 aliingia rasmi jeshini mwishoni mwa miaka ya tisini na kupanda haraka hadi kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa majeshi ya Uganda. Wakosoaji wa serikali wamekuwa wakiita hatua hiyo kuwa ni mpango wa muda mrefu wa kumwandaa kurithi urais.
Demokrasia ya uongozi
Kwa muda mrefu Museveni na mwanawe walikuwa wakikanusha madai hayo, lakini katika miaka ya hivi karibuni dalili zimeongezeka kuwa familia hiyo inaweza kutaka kuendelea kubaki madarakani hata baada ya Museveni kuondoka. Tofauti na baba yake ambaye alikuwa akijulikana kwa uwezo wa kujadiliana kisiasa na kuvutia wananchi kwa lugha ya kawaida, Muhoozi anaonekana kuwa mkali zaidi, hasa kupitia ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii ambao wakati mwingine huzua mabishano makubwa.
Museveni aliingia madarakani mwaka 1986 baada ya vita vya msituni, akiahidi kuleta demokrasia na kuondoa viongozi wanaokaa madarakani kwa muda mrefu. Lakini sasa wakosoaji wake wanasema Uganda imekuwa na mwelekeo wa utawala wa kiimla, huku ukomo wa mihula na umri wa rais ukiondolewa kikatiba.
Serikali ya Uganda pia imepitisha sheria mpya inayodhibiti ufadhili wa mashirika kutoka nje ya nchi, hatua ambayo upinzani unasema inalenga kuwanyamazisha wakosoaji wa serikali pamoja na mashirika ya kiraia. Chama cha Bobi Wine, National Unity Platform, NUP, kimeielezea sheria hiyo kuwa ni ya kibaguzi na yenye lengo la kuendelea kuwabana wale wenye maoni tofauti na serikali.