Yemen: Vikosi vya serikali vyadhibiti jimbo la Hadramout
5 Januari 2026
Mji huo wa Mukalla ni mji mkuu wa jimbo la Hadramout, sasa umeingia tena mikononi mwa serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa baada ya siku kadhaa za mashambulizi ya anga ya Saudi Arabia. Wanajeshi wasiopungua 80 wa Baraza la Mpito la Kusini mwa Yemen (STC) wameuawa katika mapigano na mashambulizi ya vikosi vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia.
Wakazi wa miji ya al-Qatn na Seiyun, katika jimbo hilo la Hadramout wameliambia shirika la Habari la Associated Press kwamba vikosi vya waasi wa Baraza la Mpito la Kusini, STC linalotaka kujitenga na linaloungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu vimeondoka kutoka kwenye kambi za kijeshi katika eneo hilo.
Vikosi vya serikali ya Yemen vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia tayari vimedhibiti maeneo muhimu huko Hadramout, jimbo kubwa lenye sehemu za jangwa kando ya mpaka wan chi hiyo na Saudi Arabia.
Yemen, iligawika kwa muda wa muongo mmoja kati ya maeneo yanayopingana, ni nchi iliyo katika eneo la kimkakati sana baina ya Saudi Arabia inayouza mafuta kwa wingi duniani na eneo la Bab al-Mandab ambalo ni njia muhimu ya baharini kati ya Ulaya na bara Asia.
Mgogoro huo ulianza mapema mwezi uliopita wakati vikosi vya Baraza la Mpito la Kusini, STC vilipoyateka maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na jimbo la Hadramout, ambapo viliweka udhibiti imara kwenye eneo lote la jimbo hilo la zamani la kusini mwa Yemen lililoungana na eneo la kaskazini mnamo mwaka 1990.
Katika wiki za hivi karibuni, Saudi Arabia ilishambulia maeneo ya STC na ilishambulia pia kile inachosema kuwa shehena ya silaha za Umoja wa Falme wa Kiarabu. Baada ya shinikizo la Saudi Arabia na kauli kali kutoka kwa vikosi vinavyowapinga WaHouthi manmo siku ya Jumamosi Umoja wa Falme za Kiarabu ulitangaza kuwa umeviondoa vikosi vyake kutoka nchini Yemen.
Mvutano nchini Yemen ulizidi kuathiri uhusiano kati ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu majirani wanaoshindana kuhusu masuala ya kiuchumi na siasa za kikanda, hasa katika eneo la Bahari Nyekundu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imesema itakuwa mwenyeji wa mkutano utakaofanyika mjini Riyadh wa kuyakutanisha makundi yote ya kusini mwa Yemen ili kujadili njia zitakazoleta suluhisho la haki kwa pande zote za kusini mwa Yemen.