1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wahitaji ushirikiano wa Marekani kuikoa WTO

Saumu Mwasimba
27 Septemba 2021

Umoja wa Ulaya wasema uko tayari kushirikiana na Marekani kulifanyia mageuzi shirika la biashara duniani liwe na nguvu mpya badala ya kulitelekeza

https://p.dw.com/p/40vyK
Schweiz Genf | WTO Hauptquartier
Picha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Mkuu wa masuala ya biashara katika umoja wa Ulaya  Valdmis Dombrovski amesema Marekani inahitaji kushirikiana na Umoja wa Ulaya kuleta mageuzi katika shirika la biashara duniani WTO kuliko kuliacha shirika hilo kuzorota kwa kulitelekeza. Makamu huyo wa rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya ameweka wazi kwamba mageuzi yanahitajika na wala sio kuliangamiza shirika hilo. Matamshi yake ameyatowa wakati akihutubia  katika chuo kikuu cha John Hopkins mwanzoni mwa wiki ya mazungumzo na wenzake wa Marekani mjini Washington.

Dombrovski amesisitiza kwamba kuliacha shirika la biashara duniani WTO liporomoke itakuwa ni kukipoteza moja ya chombo muhimu katika suala la maendeleo na biashara ya usawa. Lakini pia amesema ni suala la kuamua kati ya kufuata  utaratibu wa  sheria inayoeleweka  au sheria ya mwenye nguvu mpishe. Marekani inaendeleza sera za rais aliyetangulia Donald Trump ya kuzuia teuzi za bozi ya maamuzi ya shirika hilo la biashashara duniani na hatua hiyo inamaanisha kwamba shirika hilo haliwezi kuwa na nguvu za kuingilia kati na kuitatua migogoro ya kibiashara duniani.

Valdis Dombrovski Lettland EU
Waziri Mkuu wa Latvia Valdis DombrovskisPicha: Reuters

Dombrovski anasema Umoja wa Ulaya unautambua wasiwasi wa Marekani kuhusu kuwa na shirika la WTO linalofanya kazi na haja ya kushughulikiwa kwa dharura suala linalohusu tabia ya kutokuwepo usawa kama vile  suala la kutolewa ruzuku kubwa kwa viwanda, ulazimishaji wa kuhamisha teknolojia, ruzuku na  kujiingiza kwa kiasi kikubwa wa serikali  katika masuala ya uchumi.

 

Shirika la WTO haliwezi kuzishughulikia changamoto hizi likiwa kama lilivyo hivi sasa kwa mujibu wa kamishna wa Umoja wa Ulaya akitilia mkazo kwamba mchakato wa mageuzi unahitajika kuanzia katika mkutano wa ngazi ya mawaziri wanachama wa shirika hilo mnamo mwezi Novemba 30 hadi Desemba 3.

Dombrovski amesema Umoja wa Ulaya uko tayari kufanya kazi na Marekani kufikia makubaliana kuhusiana na ruzuku kwenye sekta ya uvuvi, afya, kilimo na maendeleo endelevu pamoja na kuanza mazungumzo ya dhati  kuhusu mageuzi ya kitaasisi.  Dombrovski ameongeza kuweka wazi kwamba anaamini ukiwepo ushirikiano imara na uongozi wa pamoja hapana shaka shirika hilo la WTO litapata nguvu mpya.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/rtre

Mhariri: Daniel Gakuba