1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wanane wauawa kwa kupigwa risasi Marekani

Grace Kabogo
16 Aprili 2021

Takriban watu wanane wameuawa baada ya kupigwa risasi kwenye mji wa Indianapolis nchini Marekani na mtu mwenye silaha anayeaminika pia kujiua.

https://p.dw.com/p/3s7Cw
Schießerei in Indianapolis in den USA
Picha: WRTV/AP/picture alliance

Msemaji wa polisi wa Indianapolis, Genae Cook amesema watu wote hao walikutwa katika ghala la kampuni ya kusafirisha mizigo ya Marekani, Fedex karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa ambako mauaji hayo yalifanyika jana usiku. Cook amewaambia waandishi habari kwamba watu wengine kadhaa wamepelekwa hospitalini.

''Tumefahamishwa kuhusu watu wengine kadhaa waliojeruhiwa ambao wamepelekwa hospitali. Tuna uhakika watu wanne walipelekwa na magari ya kubebea wagonjwa, mmoja akiwa mahututi baada ya kupata majeraha ya risasi. Watu wengine walienda wenyewe katika hospitali tofauti zilizoko kwenye eneo hili,'' alifafanua Cook.

Hata hivyo, afisa huyo wa polisi amesema hakuna tena kitisho kwa usalama wa umma. Msemaji wa Fedex amethibitisha kwamba mauaji hayo yametokea kwenye eneo la kampuni yake na wanashirikiana na maafisa wa polisi. Amesema usalama ndiyo kupaumbele chao cha kwanza na wako pamoja na wote walioathiriwa na mauaji hayo. Inaripotiwa kuwa kampuni hiyo ina zaidi ya wafanyakazi 4,000.

USA 13-jährige Adam Toledo hält seine Hände einen Sekundenbruchteil hoch, bevor er von der Polizei erschossen wurde
Adam Toledo, 13 akinyanyua mikono juu saa chache kabla ya kuuawa kwa kupigwa risasiPicha: Civilian Office of Police Accountability/REUTERS

Wakati huo huo, maafisa wa mjini Chicago wameonyesha picha za video za askari polisi akimuua kwa kumpiga risasi kijana wa Kilatino mwenye umri wa miaka 13 mwezi uliopita. Picha hizo zilinaswa kwa kutumia kamera za mwilini za polisi. Video hiyo ya kutisha inamuonesha mvulana huyo, Adam Toledo akiwakimbia polisi Machi 29 na kisha kupigwa risasi moja kifuani wakati akisimama na kunyoosha juu mikono yake.

Waendesha mashtaka wamesema mvulana huyo alikuwa amejihami kwa silaha, ingawa hakuna silaha yoyote inayoonekana kwenye mikono yake katika video hiyo wakati anapigwa risasi.

Amani na utulivu vitawale

Meya wa Chicago, Lori Lightfoot ametoa wito wa kuwepo utulivu. Akizungumza na waandishi habari jana kabla ya kutolewa kwa video hiyo, Lightfoot alitoa wito wa kuwepo amani huku akiielezea video hiyo kama ''isiyofaa kutazamwa.'' Kundi dogo la watu lilikusanyika jana mjini Chicago kwa maandamano ya amani kutokana na kifo hicho baada ya video hiyo kuoneshwa.

Mauaji hayo yamefanyika wiki hiyo hiyo ambapo polisi walimuua kwa kumpiga risasi mwanaume Mweusi, Daunte Wright mwenye umri wa miaka 20 asiyekuwa na silaha hatua iliyozusha maandamano kwenye kitongoji cha Minneapolis na Marekani kote.

Mvutano kuhusu ubaguzi wa rangi na mauaji yanayofanywa na polisi uko juu nchini Marekani, wakati ambapo jimbo jirani la Minneapolis likiendelea na kesi ya askari polisi Mzungu aliyeshtakiwa kwa kumuua Mmarekani Mweusi George Floyd. Takriban watu 30 wameuawa katika matukio ya ufyatuaji wa risasi nchini Marekani ndani ya kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

(AFP, AP, Reuters)