1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu kumi wauawa katika shambulizi la risasi Ohio

Bruce Amani
4 Agosti 2019

Watu kumi jimboni Ohio nchini Marekani wameuawa katika tukio la pili la shambulizi la risasi nchini Marekani katika kipindi cha saa 24. Polisi imesema mshukiwa wa shambulizi hilo pia ameuawa

https://p.dw.com/p/3NJcy
USA Schießerei in Dayton, Ohio
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Minchillo

Polisi ya mji wa Dayton imeandika kwenye mtandao wa Twitter kuwa tukio hilo lilianza katika Wilaya ya Oregon mwendo wa saa saba mchana lakini polisi waliokuwa karibu waliweza kulikabili haraka. Luteni Kanali Matt Carper amesema katika kikao cha waandishi wa habari kuwa mshukiwa alipigwa risasi na kuuliwa na polisi waliofika katika eneo hilo.

Karibu watu 16 wengine wamelazwa katika hospitali za eneo hilo wakiwa na majeraha. Hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu waathiriwa.

Polisi wanaamini kuwa shambulizi hilo lilifanywa na mtu mmoja pekee, na hawajamtambua mshukiwa huyo wala chanzo cha tukio hilo.

Shambulizi la El Paso

USA | Schießerei in El Paso, Texas
Shambulizi la El Paso lilisababisha vifo vya watu 20Picha: Getty Images/AFP/J. A. Juarez

Shambulizi la Ohio limekuja saa chache baada ya kijana mmoja kufyatua risasi kiholea katika umati watu waliokuwa wamejaa kwenye eneo la manunuzi mjini El Paso, jimboni Texas na kusababisha vifo vya watu 20 na madezeni kadhaa kupata majeraha.

Siku chache tu kabla, mnamo Julai 28, kijana mmoja mwenye umri wa miaka 19 aliwafyatulia risasi na kuwaua watu watatu, wakiwemo watoto wawili katika tamasha moja la chakula kaskazini mwa California. Shambulizi la El Paso ni la 21 la mauaji ya watu wengi kwa kupigwa risasi nchini Marekani mwaka wa 2019, kwa mujibu wa takwimu rasmi. Matukio ya kwanza 20 ya ufyatuaji risasi nchini Marekani 2019 yalisababisha vifo vya watu 96.

Wabunge wa Democratic wametoa wito wa kuwekwa masharti makali ya ununuzi wa silaha na kupigwa marufuku aina Fulani ya bunduki ambazo zimekuwa zikitumiwa mara kwa mara katika mauaji ya watu wengi.

USA Texas | Schießerei in El Paso - Patrick Crusius
Mshukiwa wa shambulizi la El Paso ametiwa mbaroniPicha: AFP/KTSM 9 News Channel

Lakini wabunge wa Republican wanapinga juhudi za udhibiti wa bunduki wakisema zinakiuka haki za kikatiba na kuhoji kuwa washambuliaji wanaweza kuzuiwa haraka kama Wamarekani zaidi watakuwa na bunduki.

Papa awaombea wahanga

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis amefanya maombi kwa ajili ya waliouawa na kujeruhiwa katika mashambulizi matatu ya risasi nchini Marekani iliyosababisha vifo vya watu wengi wiki hii.

Francis ameuambia umati uliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kwa ajili ya Baraka za kila Jumapili kuwa roho yake ipo karibu na wahanga wa machafuko yaliyosababisha umwagaji damu Texas, California na Ohio nchini Marekani, yaliyofanywa dhidi ya watu ambao hawangeweza kujilinda.