1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiAfrika

Watafiti wa kodi barani Afrika wakutana Tanzania

29 Agosti 2023

Watafiti wa masuala ya kodi na wanachama wa jukwaa la kodi, kutoka zaidi ya nchi 40 barani Afrika wamekutana Tanzania kujadili tafiti za kitaalamu zinazolenga kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato barani Afrika.

https://p.dw.com/p/4VicR
Washiriki wa kongamano la Jukwaa la Kodi Afrika (ATAF) mjini Dar es Salaam Tanzania tarehe 29.08.2023
Washiriki wa kongamano la Jukwaa la Kodi Afrika (ATAF) mjini Dar es Salaam Tanzania tarehe 29.08.2023Picha: Florence Majani/DW

Kongamano hilo lililobebwa na kauli mbiu, isemayo ‘masuala ya kisasa katika kodi barani Afrika' limejumuisha wadau wa masuala ya kodi, watafiti, taasisi za elimu ya juu za kodi, makamishna wa kodi, makatibu wakuu wa wizara na taasisi za kodi katika nchi za Afrika.

Akizungumza katika kongamano hilo linalotarajiwa kufanyika kwa siku tatu hapa nchini, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, (TRA), Richard Kayombo amesema kongamano hilo litaleta tija barani Afrika kwani linaratajia kutoa suluhisho la namna ya kuzuia upotevu wa mapato yatokanayo na kodi.

Akizungumzia ukusanyaji wa mapato, Kayombo amesema tafiti zinabainisha kuwa upotevu wa mapato barani Afrika unasababishwa na sekta isiyo rasmi ambapo serikali nyingi zinashindwa kufikia kundi hilo na hivyo kuruhusu upotevu huo.

Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, Profesa Adolf Mkenda amesema anatarajia kongamano hilo litakuja na suluhu za namna ya kumaliza usafirishaji wa fedha haramu, wizi wa fedha kwa njia ya mtandao na namna ya kutumia teknolojia kumaliza changamoto za ukwepaji wa kodi Afrika.

Profesa Mkenda amesema "Tunahitaji kutumia teknolojia ili kupata njia bora ambayo italeta ufumbuzi katika masuala ya usimamizi wa kodi, kuongeza ubunifu katika matumizi ya  vifaa vya teknolojia ya mawasiliano".

Caroline Mutayabarwa, ni Meneja Mafunzo wa Mtandao wa  Tafiti za Kodi Afrika(ATRN) ameiambia DW kuwa, Mtandao huo umepokea tafiti mbalimbali ikiwamo namna gani nchi za Afrika zitanufaika na makusanyo ya kodi kupitia sekta ya madini, gesi na namna gani kodi itakusanywa kupitia uchafuzi wa mazingira, ambapo kodi hutozwa kutokana na uharibifu wa mazingira.

Tanzania ni mwenyeji wa kongamano hili linalofanyika kwa mara ya nane tangu kuanzishwa kwake na limejumuisha nchi zaidi ya 40 wanachama wa Jukwaa la kodi Afrika,

Florence Majani. DW, Dar es Salaam.