1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Urusi kulinda amani Nargono Karabakh

Saumu Mwasimba
11 Novemba 2020

Urusi imepeleka wanajeshi wake 2000 wa kulinda amani katika jimbo la Nargono Karabakh baada ya Armenia na Azerbaijan kufikia makubaliano ya amani.

https://p.dw.com/p/3l8nu
Russische Friedenstruppen reisen nach Berg-Karabach in Uljanowsk
Picha: Russian Defence Ministry/REUTERS

Urusi tangu jana jumanne ilianza kupeleka wanajeshi wake 2000 wa kulinda amani katika jimbo la Nargono Karabakh baada ya Armenia na Azerbaijan kufikia makubaliano ya amani ya kumaliza vita vya wiki kadhaa katika jimbo hilo wanalolizozania. 

Makubaliani yaliyosimamiwa na Urusi yalifikiwa baada ya ushindi wa mara kadhaa wa Azerbaijan katika mapigano ya kulikomboa jimbo la Nargorno Karabakh lililoko chini ya Armenia.

Makubaliano hayo yaliibua shangwe nchini Azerbaijan lakini hayakufurahiwa nchini Armenia ambako waandamanaji waliingia mitaani kuwashutumu na kuwalaani viongozi wao kwa kulipoteza jimbo hilo lililojitenga na Azerbaijan katika vita vilivyoshuhudiwa mwanzoni mwa miaka ya 1990. Soma zaidi Armenia, Azerbaijan, Urusi zakubaliana kumaliza vita vya Karabakh

Waziri mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan,rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev na rais wa Urusi Vladmir Putin walitangaza makubaliano hayo mapema hapo jana,ambapo Pashinyan akiyataja makubaliano hayo kama hatua ya maumivu makubwa yasiyoelezeka kwake na kwa wananchi wake,wakati kwa upande wake rais Aliyev wa Azerbaijan akisema ni makubaliano yaliyonesha kwamba Armenia imeridhia kuachana na uhasama.

Azerbaijan imeshinda katika mgogogo

Reaktionen auf die neu vereinbarte Waffenruhe in Berg-Karabach
Watu wakisherehekea ushindi wa mzozo wa Nagorno Karabakh wakiwa wamebeba bendera ya AzerbaijanPicha: Gavriil Grigorov/ITAR-TASS/imago images

Makubaliano hayo yameonesha wazi kabisa ushindi wa Azerbaijan katika mgogoro huu.

Vikosi vya nchi hiyo vitayadhibiti maeneo waliyoyanyakua katika mapigano ikiwemo mji muhimu wa Shusha wakati Armenia ikikubaliana na ratiba iliyotolewa ya kuondowa wanajeshi wake katika sehemu kubwa za Nagorno Karabakh. Chini ya mpango huu pia wanajeshi 1,960 wa Urusi na magari 90 ya kijeshi,watalinda amani katika eneo hilo kwa kipindi cha miaka mitano ambacho kinaweza kurefushwa.

Lakini pia rais wa Azerbaijan,Aliyev amesema mshirika wake muhimu Uturuki kadhalika itahusika katika juhudi hizo za kuweka amani katika eneo hilo. Rais Recep Tayyip Erdogan ameweka wazi kwamba serikali yake na Urusi kwa pamoja zitasimamia usitishwaji mapigano katika kituo cha pamoja kitakachowekwa na Azerbaijan kwenye ardhi yake iliyokombolewa kutoka himaya ya Armenia. Soma Zaidi Makubaliano mapya yatangazwa Nagorno-Karabakh

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameelezea matarajio yake kwamba makubaliano hayo yatazingatia maslahi ya Waarmenia na pia akaitaka Uturuki iache uchochezi katika mgogoro huo.

Kwa upande wake rais, Erdogan ameyataja makubaliano yaliyofikiwa kuwa ni hatua stahiki katika kuelekea suluhisho la kudumu.''

Zaidi ya watu 1,400 wamethibitika kuuwawa ikiwemo raia lakini idadi hiyo ya vifo inaaminika kuwa huenda ikawa ni zaidi ya iliyotajwa.