1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati wa Uganda waikosoa Google

Admin.WagnerD16 Desemba 2020

Wanaharakati na watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Uganda wameikosoa namna Google ilivyoshughulikia barua ya serikali ya kuyafungia majukwaa yanayorusha moja kwa moja kampeni za mgombea urais Robert Kyagulanyi.

https://p.dw.com/p/3moOV
Symbolbild Google
Picha: Ralph Peters/imago images

Wanaharakati, wasomi na watumiaji wa mitandao ya kijamii wameikosoa kampuni ya Google kwa mwitikio wake kwa barua ya serikali ya Uganda kuhusu suala la kuyafungia majukwa kijamii yanayorusha moja kwa moja kampeni za mgombea urais Robert Kyagulanyi.

Google imeijibu tume ya mawasiliano ya Uganda kwamba itahitaji agizo la mahakama kuchukua hatua ya kuifungia mitandao 17 hivi ambayo iliorodheshwa na tume hiyo kwamba inasambaza taarifa za chuki zinazoweza kusababisha ghasia na machafuko katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu. 

Serikali ya Uganda kupitia kwa tume ya mawasiliano UCC imeitaka Google iziifungie idhaa 17 zenye jumla ya hadhira ya watu laki tatu na imetazamwa mara milioni 59. Hii ni kwa mujibu wa takwimu za YouTube kufikia tarehe 15 mwezi huu. Tume ya UCC inadai kuwa idhaa hizo zimendelea kusambaza taarifa za chuki za kisiasa dhidi ya serikali ya Uganda na kwa hiyo kuchochea ghasia na vurugu.

Katika barua yake ikijibu ombi la tume ya mawasiliano  ya Uganda UCC, mkuu wa masuala ya mawasiliano na umma kanda ya Afrika katika kampuni ya Google Dorothy Ooko ametaja kuwa ni vigumu kwa idhaa au jukwaa lolote kufungiwa kutokana na ombi la serikali.

Amefahamisha kuwa ili kutekeleza ombi hilo serikali ya Uganda inatakiwa kuwasilisha agizo la mahakama.

Uganda Festnahme Robert Kyagulanyi aka Bobi Wine
Robert Kyagulanyi, mgombea wa urais anayekabiliwa na changamoto kubwa katika harakati zakePicha: REUTERS

Hata hivyo, wanaharakati wa haki za binadamu, wasomi na watumiaji kadhaa wa mitandao ya kijamii wanatahadharisha Google kwamba suala hilo ni la kisiasa na haifai kuitikia kwa vyovyote ombi la serikali ya Uganda bila kuzingatia masuala nyeti ya uhuru wa kujieleza, uhuru wa vyombo vya habari na kadhalika. Wana mtazamo kuwa baada ya wagombea urais hasa Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine kuzuiliwa kuwasiliana na wapiga kura kupitia idhaa za redio na televisheni.

Wanashauri kuwa Google lazima ifanye uchunguzi wa kina kuthibitisha kama wahusika wamevunja sheria za nchi na kimataifa. 

Kulingana na tume ya UCC, mienendo ya majukwaa hayo kuonyesha maiti na damu za watu wanaojeruhiwa katika makabiliano kati ya wafuasi wa upinzani na polisi na majeshi inasababisha ulimwengu kudhani kuwa hakuna amani na utulivu Uganda na kuwatia hofu wananchi ilihali hivyo ni vitendo vya watu wanaokiuka maagizo yaliyowekwa ya kuendesha kampeni.

Lakini mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu Nicholas Opiyo ana mtazamo kuwa UCC inajaribu kuzuia matumizi ya majukwaa hayo ambayo ndiyo mbadala kwa wanasiasa walionyimwa fursa kutumia idhaa na vyombo vya habari nchini Uganda.

Rais wa mtandao wa idhaa za mtandaoni nchini Uganda Andrew Irumba ametaja hatua ya serikali kuwa ya kisiasa akiongezea kuwa hata kuna idhaa zinazotangaza habari za chama tawala ambazo zinasambaza taarifa za chuki lakini hazikuorodheshwa.

Mapema mwaka huu tume ya mawasiliano ya Uganda, iliagiza majukwaa yote ya mitandao ya kijamii yasajiliwe rasmi kwa mujibu wa sheria za nchi. Lakini mkuu wa masuala ya kisheria wa tume hiyo Abdul Salam Waiswa ameelezea kuwa hadi sasa majukwaa mengi ambayo yameorodheshwa kukiuka sheria za kuepusha kusambaza chuki na uhasama hayajasajiliwa. Kwa ajili ya hili pia wanataka ushirikiano wa Google kuyafungia.

Lubega Emmanuel DW Kampala.