1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Waganda wamemchoka Museveni lakini hawawezi kumuondoa

Daniel Gakuba
23 Novemba 2020

Ghasia zilizotokea nchini Uganda na nguvu za ziada zilizotumiwa na vyombo vya usalama kuzizima ghasia hizo, ni ishara kuwa Waganda wamemchoka Rais Yoweri Museveni. Maoni ya Daniel Gakuba wa DW Kiswahili.

https://p.dw.com/p/3ljY3
Uganda Festnahme Robert Kyagulanyi aka Bobi Wine
Picha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za polisi ya Uganda, watu 50 waliuawa katika vurugu hizo zilizofuatia kukamatwa na kuwekwa rumande kwa Robert Kyagulanyi, mwanamuziki aliyegeuka mwanasiasa, akijulikana zaidi kwa jina lake la usanii la Bobi Wine.

Soma zaidi: HRW: Uganda inatumia suala la COVID-19 kukandamiza upinzani

Wengi wa wahanga hao walikufa kwa kupigwa risasi za moto na maaskari waliovalia sare na wengine wakivaa nguo za kiraia, katika kile kinachotazamwa na wafuasi wa Bobi Wine kama mkakati wa chama tawala wa kulikandamiza vuguvugu lao la upinzani linalokua kwa kasi.

Bobi Wine ni mgombea wa urais kupitia chama chake cha Jukwaa la Umoja wa Kitaifa-UNP, anayeonekana kuwa kitisho kikubwa dhidi ya utawala wa muda mrefu wa Rais Museveni mwenye umri wa miaka 76, ambaye yeye anawania muhula wa sita mamlakani.

Kommentarbild PROVISORISCH | DW Kiswahili | Daniel Gakuba
Daniel Gakuba, mhariri katika Idhaa ya Kiswahili ya DW

Sababu ya kukamatwa kwa Bobi Wine Mashariki mwa Uganda akifanya kampeni wiki iliyopita, ilielezwa na polisi kuwa ilitokana na kukiuka masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Soma zaidi:Uganda: Idadi ya waliopoteza maisha yafikia watu 30

Kushikiliwa kwake rumande kwa siku mbili kulizusha ghadhabu kubwa nchini kote Uganda, nje kabisa ya mji mkuu Kampala ambao kawaida ni ngome ya upinzani. Hasira hizo zinatosha kuwapa onyo Museveni na wafuasi wake, kwamba hatimaye raia huchoshwa na hila zote zinazotumiwa na utawala wa kiimla, na husimama kidete kupigania haki zao.

Museveni azima moto kwa kuumwagia mafuta

Katika nyakati kama hizi za misukosuko ya kitaifa, Museveni angeonekana mstaarabu kama angejikeza na kuwapa pole waliofiwa, kukemea ukandamizaji wa polisi, na kutoa rai ya maridhiano ya kitaifa.

Badala yake, hulka ya rais huyo ambaye zamani aliongoza kundi la waasi, yumkini ilimfanya adhani kuonyesha moyo wa kujali kunaweza kumuonyesha kama mtu dhaifu.

Alichokifanya wakati wa kampeni yake baada ya ghasia hizo, ni kutishia kuwavunjavunja wale aliosema wanawatisha wafuasi wa chama chake cha NRM, na wanaotumia lugha ya matusi kumlenga yeye.

Museveni alisema wamejidanganya sana kuingia katika uwanja wa mapigano, ambao amesema ni eneo analolimudu vyema.

Majibu yake hayo yanadhihirisha yale aliyowahi kuyasema katika mkutano wa chama chake, kwamba yeye sio mtumishi wa Waganda, na kuongeza kuwa anayoyafanya yote ni kwa maslahi yake binafsi.

Bildkombo Yoweri Museveni und Bobi Wine
Bobi Wine (kulia) anampa Tumbo joto Yoweri Museveni katika uchaguzi wa Januari mwaka ujao

Alipoingia madarakani kwa mtutu wa bunduki mwaka 1986, Museveni alisema na tatizo la Afrika na la Uganda sio watu wake, bali viongozi wasiotaka kuachia madaraka. Naamini kuwa hata yeye mwenyewe, wakati huo asingeamini kwamba miaka 34 baadaye, angekuwa bado anatumia bunduki kuwanyamazisha vijana waliozaliwa akiwa rais, ambalo kosa lao kubwa ni kutaka mabadiliko kupitia njia za kidemokrasia.

Vyombo vya usalama vinaona makosa ya upande mmoja

Ki kweli kwamba baadhi ya makundi ya wahuni yaliitumia hali hii kufanya uporaji na kuwashambulia raia na maafisa wa usalama, na yanapaswa kulaaniwa pia. Lakini, kwa sehemu kubwa mripuko wa maasi ya upinzani ulitokea bila kupangwa, na ulitokana na kukata tamaa kwa sababu vyombo vya usalama wa taifa vilitumiwa kumlenga tu mgombea wao.

Soma zaidi: Vurugu zatokea Uganda baada ya kukamatwa Bobi Wine

Kushindwa kwa polisi ya Uganda kuyadhibiti maasi madogo tu ya umma bila umwagaji wa damu, kunadhihirisha kuwa taasisi hiyo haina mafunzo yanayostahili. Na kuwaandama wagombea wa upinzani kwa kisingizio cha kuhakikisha masharti ya kujikinga na COVID-19 yanafuatwa, huku wagombea wa chama tawala wakifumbiwa macho wanapoyakiuka masharti hayo, yanaanika kweupe ukweli kwamba uchaguzi ujao ya tarehe 14 Januari 2021, tayari unazo kasoro.

Lakini kwa wale wanaofuatilia siasa za Uganda chini ya uongozi wa zaidi ya miongo mitatu wa Museveni, ambaye amebadilisha katiba mara mbili kujisafishia njia ya kusalia madarakani, yanayotokea sasa hayashangazi.

Mwaka 2001 Rais huyo alijilinganisha na kotapini kwenye pedali ya baskeli, ambayo huingizwa kwa nyundo, na kutolewa kwa nyundo. Maana yake, ameingia kwa mtutu wa bunduki, na anaweza tu kutolewa kwa bunduki. Kufikiria kuwa anaweza kutoka madarakani kwa sababu ameshindwa katika uchaguzi, ni kujidanganya sana.