Wakimbizi wa Ethiopia wapewa hifadhi Marsabit | Matukio ya Afrika | DW | 07.10.2022
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Wakimbizi wa Ethiopia wapewa hifadhi Marsabit

Familia zisizopungua 400 kutoka nchini Ethiopia zinahifadhiwa na wakaazi wa eneo la Uran jimboni Marsabit nchini Kenya, baada ya kukimbilia eneo hilo la mpakani kutokana na makali ya ukame.

Huku makali ya kiangazi na ukame yakiendelea kuripotiwa katika maeneo mbalimbali ya  Pembe ya afrika, idadi ya wahamiaji wanaotafuta chakula inaendelea kuongezeka katika eneo la Uran mpakani mwa Kenya na Ethiopia.

Familia zipatazo mia nne kutoka Ethiopia tayari zimevuka na kuingia upande wa kenya na kwa sasa zinahifadhiwa na wakaazi wa eneo la Uran.  Asili mia themanini ya wahamiaji hao ni akina mama na watoto ambao wamekuwa waathiriwa wakubwa wa baa la njaa.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa mkutano wa wadau wa kupambana na majanga jimboni Marsabit,mratibu katika shirika la World Vision Jarso James Galgallo ,amesema kuwa,kuna haja kwa serikali na wadau wengine kushikana mkono kuwasaidia wahamiaji hao ambao kwa sasa wanaishi katika mazingira duni.

"Kati ya familia mia tatu hamsini na mia nne wametoroka kwa sababu wameathirika na njaa.Mifugo waliokuwa nao wamekufa na sasa katika ile hali ya kujiokoa,wamekuja upande huu.”

''Mifugo wetu huelekea eneo la Ethiopia''

Afisa huyo amesema kuwa,kuna haja ya mashirika ya kijamii kuwapa wahamiaji hao msaada, ikiwemo malazi na vyandarua vya kujikinga.

Serikali ya kaunti ya Marsabit imekiri kuwa na ufahamu kuhusu wahamiaji hao eneo la uran na kwamba imekuwa ikitoa msaada wa chakula japo hautoshi kwa wakaazi wenyewe.

Katibu wa serikali ya kaunti Ibrahim Adan Sora amesema wafugaji wamekuwa wakihamahama kutafuta malisho kwa mifugo wakati ambapo malisho yamepungua kutokana na hali mbaya ya ukame.

"Kwa sasa,tuna watu wengi eneo la Uran na hili ni kutokana na uhaba wa lishe na chakula.Hata sisi,mifugo wetu huelekea eneo la Ethiopia …”

Serikali ya kaunti aidha,imeeleza kuwa,maafisa kutoka shirika la kimataifa la kuwashugukikia wahamiaji IOM wanatarajiwa kuzuru eneo la Uran wanakohifadhiwa wahamiaji hao kabla ya kuchukua hatua zaidi.

Marsabit imeendelea kuripoti hali mbaya ya ukame huku maelfu ya wafugaji wakiendelea kuhamia katika majimbo Jirani kuokoa Maisha ya mifugo yao wakati huu.