1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Wahamiaji wa Afrika wadiriki safari hatari Visiwa vya Canary

10 Februari 2026

Safari ya kuvuka kati ya Afrika na Visiwa vya Canary inatajwa kuwa njia hatari zaidi ya uhamiaji duniani. Takriban watu 2,000 walifia humo mwaka 2025. Mara kwa mara pia hutokea matukio ya vurugu ndani ya mashua hizo.

https://p.dw.com/p/58T82
Wahamiaji wawasili Visiwa vya Canary
Ingawa Visiwa vya Canary vimeripoti idadi ndogo ya wahamiaji wanaowasili ikilinganishwa na miaka ya awali, ripoti za vurugu ndani ya mashua zimeongezeka.Picha: IMAGO/ABACAPRESS

Mahali fulani kati ya kusini mwa Morocco na kisiwa cha Uhispania cha Teneriffa, jinamizi lilianza kwa Ismael Ouattara. Ndani ya saa 24, binti yake wa mwaka mmoja na mke wake walifariki. Wakati huo, mashua yao ilikuwa tayari imekuwa ikielea bila uwezo wa kujiendesha kwenye Bahari ya Atlantiki kwa siku kadhaa.

"Binti yangu alifariki mikononi mwangu. Asubuhi iliyofuata mke wangu hakuamka tena. Nafikiri ni kwa sababu ya mshtuko wa kifo hicho,” anakumbuka kijana huyo.

Kama makumi ya maelfu ya wengine, Ouattara alikuwa ameondoka Ivory Coast pamoja na familia yake ili kutafuta kazi yenye malipo bora barani Ulaya. Hakuwa hata mara moja amewahi kufikiria kwamba safari hiyo ingeweza kugeuka kuwa janga kama hilo.

"Maiti zilitupwa tu baharini mara moja,” anakumbuka raia huyo wa Ivory Coast. "Wengine hawaombi ruhusa kwa muda mrefu.”

"Wanafikiri wakiwa baharini wanaweza kufanya lolote”

Tukio hilo lilitokea miaka minne iliyopita, lakini hadi leo Ouattara huumia kuona jinsi abiria wengine walivyoshughulikia miili ya wapendwa wake bila heshima. Hata hivyo, hakukuwa na milipuko ya vurugu miongoni mwa manusura wa mashua hiyo, anasema. Kwa sababu hali kama hizo kali si jambo la ajabu kuzua vurugu.

Wahamiaji 532 kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara wafika El Hierro — Huduma za afya zatoa msaada baada ya kuwasili kwa boti katika T-532
Wahamiaji wengi wanaofika Visiwa vya Canary wameokoka hali za kutisha bahariniPicha: IMAGO/ABACAPRESS

Mohammed Manga ameshuhudia hilo. "Kulikuwa na vurugu nyingi kwenye mashua yetu,” anakumbuka kijana huyo kutoka Gambia aliyewasili Visiwa vya Canary mwaka 2023. "Siku ya nne baharini baadhi waliingiwa na hofu na kuanza kushutumiana kuwa wachawi.”

Mchanganyiko wa hali ya hatari na imani katika nguvu za kichawi hufanya matukio hayo kuwa ya hatari sana, kulingana na abiria huyo wa zamani. Ingawa hakuna aliyefariki katika vurugu hizo, kulikuwa na majeruhi wengi, anasema Manga. Hakuna aliyewajibishwa — hata baadaye walipofika Canary.

"Ni vigumu sana kuchukua hatua yoyote baadaye. Ndiyo maana baadhi ya watu hufikiri wakiwa baharini wanaweza kufanya lolote.”

Abiria walitupwa baharini wakiwa hai

Hivi karibuni, safari kupitia njia ya Atlantiki kati ya Afrika na Visiwa vya Canary zimepungua. Mwaka 2024 zaidi ya wahamiaji 40,000 waliwasili visiwani humo, lakini mwaka uliofuata idadi ilishuka hadi karibu 18,000. Wataalamu wengi wanasema ni kutokana na ushirikiano mkubwa kati ya Ulaya na nchi za mpito kama Mauritania na Morocco, pamoja na udhibiti mkali wa mipaka.

Hata hivyo, kuna ongezeko la ripoti za vurugu kali na hata mauaji yanayodaiwa kutokea kwenye mashua.

Katikati ya 2024, Wasenegal watatu wanadaiwa kuwapiga vibaya watu kadhaa hadi baadhi wakapata ulemavu wa kudumu. Mwaka 2025, polisi ya Uhispania iliwakamata watu 19 baada ya takribani abiria 50 kufariki kati ya Senegal na Gran Canaria — tukio linaloshukiwa kuwa mauaji ya halaiki baharini.

Wahamiaji wafika Visiwa vya Canary
Matukio yanapotokea baharini, uchunguzi wa baadaye mara nyingi huwa karibu hauwezekani.Picha: IMAGO/ABACAPRESS

Walionusurika wanasema washukiwa waliwapiga makumi ya abiria hadi kufa na wengine kuwatupa baharini wakiwa bado hai. Haijulikani iwapo walikuwa wanachama wa mitandao ya usafirishaji haramu au abiria wa kawaida. Polisi wa taifa la Uhispania hawakutaka kutoa maoni.

Utata katika ushahidi

Wakili Loueila Sin Ahmed Ndiaye, anayefanya kazi Visiwa vya Canary, anasema kufuatilia kisheria matukio hayo ni vigumu sana. Uhalifu mara nyingi hutokea nje ya eneo la Uhispania na hauhusishi raia wa Uhispania.

Pia kuna matatizo makubwa ya ushahidi. "Ripoti za polisi zinaonyesha watu hupoteza hisia ya muda. Baridi, hofu, kutoona nchi, hali ya wasiwasi — yote haya huathiri afya ya akili,” anasema. Hivyo ushahidi huwa na utata.

Zaidi ya hayo, manusura wengi hukataa kushirikiana na mamlaka, hata kuwakataa mawakili wao. "Baada ya siku 10 hadi 14 baharini, wana hofu. Kitu cha mwisho wanachotaka ni kushiriki katika kesi ya mahakama.”

Waathirika wakuu mara nyingi ni makundi dhaifu: watoto, vijana wanaosafiri peke yao na wanawake. Mwishowe, kesi nyingi hufungwa bila wahusika kuwajibishwa na bila fidia kwa waathirika.

Wahamiaji 4 wamefariki, 29 wapotelea baharini nchini Uhispania

Hakuna mahali pa kuomboleza

Kwa Ismael Ouattara, aliyempoteza mke na binti, fidia ya kifedha si muhimu. Miaka minne baadaye ameanza maisha mapya Canary pamoja na binti yake mkubwa aliyenusurika.

Lakini hadi leo anakosa mahali pa kuomboleza.

"Nimebaki na kumbukumbu tu. Hakuna kaburi la kupeleka maua. Hilo ndilo linalofanya hali hii iwe ngumu zaidi kuvumilia.”