1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usafiri kati ya miji ya Bukavu na Uvira wasitishwa

11 Mei 2026

Safari kati ya Bukavu na Uvira zimesimamishwa kwa muda usiojulikana, huku mamlaka zikilenga kudhibiti harakati kati ya serikali na waasi wa AFC/M23.

https://p.dw.com/p/5DbLv
Gavana wa Kivu Kusini aliye mjini Uvira amesema usafiri utaendelea kusimamishwa hadi waasi hao watakapoondoka Bukavu
Gavana wa Kivu Kusini aliye mjini Uvira amesema usafiri utaendelea kusimamishwa hadi waasi hao watakapoondoka BukavuPicha: Janvier Barhahiga/AP Photo/picture alliance

Akizungumza mbele ya wanahabari mjini Uvira, Jean-Jacques Elakano amesema serikali inahofia kuwa waasi wa AFC/M23 wanatumia shughuli za biashara na safari za kifamilia kati ya Bukavu na Uvira kujipenyeza katika maeneo yanayodhibitiwa na jeshi la serikali.

"Sasa njia itafungwa. Cha huku hakiendi kule na cha kule hakiendi huku. Lengo letu ni kuhakikisha tunairejesha Bukavu”, alisema Elakano.

Hata hivyo, hatua hiyo imezua malalamiko makubwa kutoka kwa wakazi wa Bukavu na Uvira ambao kwa zaidi ya mwaka mmoja wameendelea kuathiriwa na vita na kuyumba kwa shughuli za kiuchumi. Wakazi wengi wanasema kufunguliwa tena kwa barabara hiyo mwezi Aprili kulirejesha matumaini ya biashara na usafiri, hasa kwa jamii zinazotegemeana kiuchumi katika bonde la Mto Ruzizi.

Serges mwagizaji wa viatu vya mitumba kutoka Burundi akiviuza katika baadhi ya vijiji vya bonde la Mto Ruzizi, anaelezea masikitiko yake.

"Vita ni chafu kweli! Wakiifunga ina maana wanataka kutuua sasa, viongozi watuelewe jinsi wanavyowaelewa watoto wao. Au Kinshasa tayari wametusahau? Hatupendezwi na ugomvi wao; watuache tufanye biashara kama ilivyokuwa awali."

"Wakiifunga ni raia ndio wataendelea kuteseka"

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uvira 2025 | Warundi waliokwama katika kivuko cha mpaka cha Kavimvira baada ya kufungwa
Mvutano wa kiusalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umechukua sura mpya baada ya mamlaka iliyo chini ya utawala wa Kinshasa kusimamisha tena usafiri kati ya miji ya Bukavu na Uvira kwa muda usiyojulikanaPicha: Jospin Mwisha/AFP/Getty Images

Kusimamishwa kwa usafiri kunakuja huku kukiwa na mvutano mkubwa wakiusalama Mashariki mwa Kongo. Mapigano ya mara kwa mara kati ya waasi wa AFC/M23 wanaodaiwa kusaidiwa na Rwanda na jeshi la Kongo linalosaidiwa na Wazalendo yamesababisha wakazi wa baadhi ya vijiji kuhama makazi yao na kuvuruga shughuli za kiuchumi katika maeneo kadhaa ya jimbo la Kivu kusini.

Mashirika ya kiraia pia yameitaka serikali kutafuta njia mbadala badala ya kufunga barabara hiyo. Mwanaharakati Pacifique Karauka amesema mamlaka zinaweza kuongeza vituo vya ukaguzi bila kusimamisha kabisa usafiri ambao unaathiri maisha ya raia.

"Waongeze vituo vya ukaguzi lakini wasifunge barabara maana wakiifunga ni raia ndio wataendelea kuteseka”, alisema Karauka.

Wakati huohuo, taarifa kutoka eneo la Uvira zinaeleza kuwa tangu Jumamosi kumekuwa na harakati za kujiondoa kwa wapiganaji wa AFC/M23 kutoka eneo la Sange pamoja na baadhi ya vijiji vya milimani kuelekea kaskazini mwa wilaya hiyo.

Video zilizosambaa mitandaoni zinaonesha wanajeshi wa serikali ya Kongo pamoja na makundi ya Wazalendo wakiingia katika kijiji cha Sange. Jeshi la Kongo pia limesema waasi hao wameondoka katika vijiji vya Nyakabere, Mutarule na Luberizi, madai ambayo hadi sasa hayajathibitishwa na AFC/M23.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi