1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa upinzani Katumbi na Bemba kurejea nyumbani

Sekione Kitojo
31 Julai 2018

Tajiri mkubwa na kigogo wa kisiasa Moise Katumbi alisema anatafuta ruhusa kurejea nyumbani Jamhuri ya Kidemokrasi ya  Congo wiki hii ili kujitupa katika kinyang'anyiro kuwania urais katika nchi tete kabisa barani Afrika.

https://p.dw.com/p/32Mjc
Kongo: Bildkombo Moise Katumbi und Jean-Pierre Bemba

Halikadhalika mbabe  wa  zamani  wa  kivita  Jean-Pierre Bemba  anatarajiwa  kuwasili   nchini  humo  kesho akiwa  na dhamira  ya  kuwania  pia  kiti  cha  urais  katika  uchaguzi  mkuu unaosubiriwa  kwa  hamu  kubwa  mwezi  Desemba mwaka  huu.

Ruanda Kigali Opposition Moise Katumbi
Moise Katumbi akizungumza na waandishi habariPicha: DW/E. Topona

Katumbi  amesema  katika mahojiano  kwa  njia  ya  simu  na  shirika la  habari  la  Ufaransa  AFP kwamba  yuko  mjini  Johannesburgh na  ameiandikia  mamlaka  ya  safari  za  anga  kuomba  ruhusa  kwa ndege  yake  ya  binafsi  kutua  siku  ya  Ijumaa  mjini  Lubumbashi , mji  mkuu  wa  jimbo  la  Katanga.

Katumbi mwenye  umri  wa  miaka  53, gavana  wa  zamani  wa jimbo  hilo  lenye  utajiri  mkubwa  wa  madini, amekuwa  akiishi uhamishoni  nchini  Ubelgiji  tangu Mei 2016  baada  ya  kutofautiana na  rais Joseph Kabila.

Ameapa  kurejea  kwa  ajili  ya  uchaguzi  ambao umecheleweshwa mno  hapo Desemba  23 licha  ya  kuhukumiwa  kifungo  cha  miaka mitatu jela  katika  kesi  ambayo  anadaiwa  kufanya  udanganyifu wa majumba.

Pia  amefunguliwa  mashitaka  kwa  kile  kinachoonekana  kuwa  ni kukodisha  mamluki  na  kuwa  na  hati  ya  kusafiria  ya  Italia, ambapo  sheria  ya  Congo  hairuhusu  kuwa  na  uraia pacha, wa mataifa  mawili.

Demokratische Republik Kongo Joseph Kabila
Rais Joseph Kabila ambaye muda wake umemalizika kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Desemba 2016.Picha: Getty Images/AFP/T. Nicolon

Kabila  ambaye  ni  mwanajeshi  wa  zamani , amekuwa  madarakani tangu  mwaka  2001, wakati  alipochukua  madaraka  kutoka  kwa baba  yake  aliyeuwawa. akiongoza serikali ambayo  imekosolewa kwa  kiasi  kikubwa  kwamba ametapakaa  rushwa  na isoyofanyakazi , alikuwa aondoke madarakani  Desemba  2016  kwa mujibu  wa  katiba  ya  nchi  hiyo  mwishoni  mwa  muhula  wake  wa pili.

Bemba  anarejea

Lakini  aliendelea  kubaki  madarakani  hadi  pale  mrithi  wake atakapochaguliwa, hatua  ambayo imechochea  maandamano mitaani  na kukandamizwa  kwa  nguvu  pamoja  na  mamia  ya  watu kuuwawa.

Demokratische Republik Kongo Proteste
Waandamanaji wakimnyanyua mwenzao katika maandamano ya kuipinga serikali katika DRCPicha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Hasimu  mwingine  mkubwa  wa  Kabila  ni  mbabe  wa  zamani wa kivita  na  makamu  wa  rais Jean-Pierre  Bemba, mwenye  umri  wa miaka  55, ambaye  mwezi  Juni  alifutiwa  mashitaka  ya  uhalifu  wa kivita katika  mahakama  ya  kimataifa  ya  uhalifu  mjini  The  Hague.

Chama  chake  hapo  mwanzo  kilisema  atawasili  katika  mji  wa Gemena, mji  ulioko  katika  ngome  yake  kuu upande  wa  kaskazini magharibi  mwa  nchi  hiyo  leo  Jumanne. Lakini  chama  hicho kilisema  jana  kuwa  hajapata  ruhusa  ya  ndege  yake  kutua katika  mji  huo. maelfu ya  watu  walikuwa  wakimsubiri mjini Gemena jana.

Belgien Jean-Pierre Bemba Gombo in Brüssel
Jean-Pierre Bemba baada ya mkutano na waandishi habari mjini Brussels Julai 24, 2018Picha: Reuters/F. Lenoir

Bemba  ameapa  kurejea  mjini  Kinshasa  kesho  Jumatano Agosti mosi  kutangaza  nia  yake  ya  kugombea katika  uchaguzi.  Jana gavana  wa  mji  wa  Kinshasa  amesema  atahakikisha  usalama  na kuamuru polisi  10 , kumlinda  Bemba wakati  atakaporejea, afisa  wa chama  cha  Bemba  cha  MLC  amesema.

Mwandishi:  Sekione Kitojo /afp

Mhariri: Iddi Ssessanga