1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya wampongeza Merkel

Sabine Faber23 Septemba 2013

Ushindi wa Kansela Angela Merkel kuiongoza Ujerumani kwa muhula wa tatu, umepongezwa na viongozi wa mataifa ya Ulaya ambao wanauona kuwa ni muhimu kwa mustakabali wa bara hilo.

https://p.dw.com/p/19mG9
Kansela wa Ujerumani Angela akizungumza na wafuasi wake baada ya kushinda uchaguzi mkuu.
Kansela wa Ujerumani Angela akizungumza na wafuasi wake baada ya kushinda uchaguzi mkuu.Picha: Reuters

Lakini uchaguzi huu ulitoa mshangao wa kihistoria kwa mshirika wa Merkel katika serikali iliyopita, chama cha Kiliberali cha FDP, ambacho hakitakuwa bungeni kwa miaka minne ijayo, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 1949, na sasa wadadisi wanahoji iwapo huu ndiyo mwisho wa enzi kwa chama hicho, ambacho kimekuwa madarakani kwa muda mrefu kuliko chama chochote nchini Ujerumani.

Ushindi muhimu kwa Ulaya
Rais wa Ufaransa Francoise Hollande, ambaye wakati mwingine amekuwa akitofautiana wazi na Merkel kuhusiana na sera zake za kubana matumizi kwa Ulaya, alikuwa kiongozi wa kwanza kumpigia simu, baada ya matokeo ya awali kumuonyesha akielekea ushindi wa wazi. Ofisi ya rais Hollande ilisema viongozi hao wawili walionyesha nia ya kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano, ili kutimiza malengo ya Umoja wa Ulaya. Hollande pia alimualika Merkel mjini Paris, pale atakapokamilisha kuunda serikali yake.

Merkel na mpinzani wake mkuu Peer Steinbrück kutoka chama cha SPD.
Merkel na mpinzani wake mkuu Peer Steinbrück kutoka chama cha SPD.Picha: Nigel Treblin/Getty Images

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron alitumia mtandao wa kijamii wa twitter kutuma salaamu zake. "Pongezi nyingi kwa Merkel, natizamia kuendelea kufanya naye kazi kwa karibu," aliandika waziri Mkuu Cameron.

Waziri mkuu wa Italia, Enrico Letta, ambaye nchi yake inapitia kipindi kigumu cha kubana matumizi, aliyaita matokea ya uchaguzi huo kuwa ni adhimu kwa Merkel, na pia alizungumzia umuhimu wake kwa Umoja wa Ulaya.

Katika kile kilichoonekana kama kukilenga chama kipya cha Alternative für Deutschland, au chama mbadala kwa Ujerumani AfD, Letta alisema kama matokeo hayo yatathibitisha kuwa chama hicho ambacho kinapinga sarafu ya euro hakipati uwakilishi bungeni, basi yatakuwa mazuri kwa Umoja wa Ulaya.

Chama cha AfD kilijaribu kutumia hasira juu ya mchango wa Ujerumani katika uokozi wa mataifa washirika yanayokabiliwa na migogoro ya kifedha, lakini matokeo ya mwisho yameonyesha kuwa chama hicho kilishindwa kuvuka kiunzi cha asilimia 5 ya kura, kinachotakiwa kwa chama kupata uwakilishi bungeni. Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy, alielezea imani kuwa Merkel, katika uongozi wa taifa kubwa zaidi kiuchumi barani Ulaya, ataendelea kufanya kazi kwa Ulaya yenye mafanikio.

Mshirika wa Merkel FDP yaangukia pua
Licha ya ushindi huo wa Merkel hata hivyo, analaazimika kutafuta mshirika mwingine wa kuunda naye serikali, baada ya chama chake CDU kutopata wingi wa kutosha kukiwezesha kuunda serikali peke yake. Mshirika wake katika serikali inayomaliza muda wake, chama cha kiliberali cha FDP, kilijikuta kikiangukia pua, katika kile mwenyekiti wa chama hicho wa jimbo la North-Rhine Westphalia, Chritian Lindner, alichokieleza kama maumivu yasiyo kifani, na wakati mgumu zaidi kwa chama hicho kinachotetea bishara huru. "Huu ndiyo wakati mchungu zaidi kwa FDP tangu mwaka 1949. Ni wazi kwamba matajario ya wapiga kura hatukuyatimiza katika ushiriki wetu serikalini."

Baadhi ya viongozi wa chama kilichoangushwa cha FDP, waziri wa mambo ya kigeni Guido Westerwelle, waziri wa ushirikiano wa kimaendeleo Dirk Niebel, na mjumbe wa chama hicho Christian Lindner.
Baadhi ya viongozi wa chama kilichoangushwa cha FDP, waziri wa mambo ya kigeni Guido Westerwelle, waziri wa ushirikiano wa kimaendeleo Dirk Niebel, na mjumbe wa chama hicho Christian Lindner.Picha: Reuters

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Profesa Dr. Ulrich von Alemann alisema FDP yapaswa kujilaumu kwa yaliyowakuta. "Hiyo ndiyo ilikuwa stakabadhi ya sera. Huwa kunakuwa na nukta tatu au nne kwa pamoja. Na FDP imefanya makosa katika sera yao, katika program yao, katika kampeni yao ya uchaguzi, na pia kwa viongozi wao", alisema Profesa Ulrich.

Lakini profesa Ulrich anasema bila ya kuwepo na chama cha Alternative für Deutscland, FDP inaweza kurudi bungeni. Lakini kwa miaka minne ijayo, chama hicho kitakuwa mtazamaji tu.


Mwandishi: Griebeler Monika/HGD deutsch/ Ssessanga Iddi Ismail/afpe
Mhariri: Daniel Gakuba