1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiMashariki ya Kati

Viongozi wa Palestina waituhumu Israel mbele ya ICJ

19 Februari 2024

Israel imekuwa ikikiuka kwa maksudi sheria ya kimataifa kwa miongo kadhaa, imehoji Mamlaka ya Wapalestina mbele ya mahakama ya kimataifa ya haki, ICJ, inayosikiliza kesi kuhusu sera za Israel katika eneo la Wapalestina.

https://p.dw.com/p/4caRR
Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ
Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ ikiwa katika uendeshaji wa shauriPicha: Robin van Lonkhuijsen/ANP/AFP/Getty Images

Viongozi wa Mamlaka ya Palestina wamezungumza hii leo mbele ya Mahakama ya Haki ya Kimataifa, ICJ, na wameituhumu Israel kuwa imekuwa ikikiuka kwa makusudi na kwa miongo kadhaa sheria za kimataifa iliponyakua na kukalia kwa mabavu maeneo ya Palestina mnamo mwaka 1967 .

Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyadh al-Maliki amesema ni lazima nguvu ya sheria itawale huku akilalamika kuwa Wapalestina wamekuwa wakiteseka na "ukoloni na ubaguzi wa rangi", na akiwataka majaji wa ICJ kuamuru mara moja na bila masharti kukomeshwa kwa ukaliaji wa Israel.

Soma pia:ICJ kujadili ukaliaji wa Israel kwenye maeneo ya Palestina

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliwasilisha ombi la kujadiliwa kwa uhalali wa Israel kuikalia kimabavu ardhi ya Palestina kwa muda wa miaka 57. Kuanzia leo na kwa muda wa siku 6, majaji 15 wa Mahakama hiyo watajadili ukaliaji wa kimabavu wa Israel katika maeneo ya Ukingo wa Magharibi, Gaza na Jerusalem Mashariki.