1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Waziri wa Wapalestina aishutumu Israel kwa ubaguzi wa rangi

John Juma
19 Februari 2024

Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Wapalestina ameishutumu Israel kwa ukoloni na ubaguzi wa rangi kwa kukalia ardhi inayodaiwa na Wapalestina kwa miaka 57.

https://p.dw.com/p/4cZlY
Mawakili wa upande wa mamlaka ya Wapalestina waiambia mahakama ya ICJ kwamba 'Israel imekiuka sheria kwa kunyakua sehemu kubwa ya ardhi yao'.
Mawakili wa upande wa mamlaka ya Wapalestina waiambia mahakama ya ICJ kwamba 'Israel imekiuka sheria kwa kunyakua sehemu kubwa ya ardhi yao'.Picha: Selman Aksunger/AA/picture alliance

Al-Malik ameihimiza mahakama ya juu ya haki ya Umoja wa Mataifa kuamua kwamba hatua ya Israel kuikalia ardhi inayodaiwa na Wapalestina ni kinyume cha sheria na ikome mara moja bila masharti yoyote.

Riyad al-Malik amesema hatua hiyo ndiyo itahakikisha matumaini ya uwepo wa mataifa mawili kama suluhisho la mgogoro wa Mashariki ya Kati. Ameyasema hayo mapema Jumatatu wakati wa kuanza kwa kesi ya kihistoria dhidi ya Israel kuhusu uhalali wake wa kukalia kwa miaka 57, ardhi inayotakiwa kuunda taifa la Wapalestina.

Al-Maliki aliiambia mahakama hiyo kuwa Wapalestina milioni 2.3 wa Gaza, nusu yao wakiwa watoto wamezingirwa humo, wanapigwa mabomu, wanauawa, wanajeruhiwa, wanakabiliwa na njaa na kuwa wakimbizi.

Soma pia: Mahakama ya UN yaitaka Israel kuepusha mauaji ya kimbari Gaza

''Umoja wa Mataifa uliweka wazi kwenye Mkataba wake, haki ya kujitawala na uliahidi kuondoa ukiukwaji mkubwa wa haki hii yaani ukoloni na ubaguzi wa rangi. Hata hivyo kwa miongo kadhaa, Wapalestina wamekuwa wakinyimwa haki hii na wamevumilia ukoloni na ubaguzi wa rangi,'' amesema al-Malik.

Vita vya Gaza vyahofiwa vitagubika vikao vya kesi dhidi ya makaazi ya Israel

Vikao hivyo vinafuatia ombi lililowasilishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa maoni ya ushauri yasiyofungamana na sera za Israeli katika maeneo yaliyochukuliwa.

Nembo ya mahakama ya kimataifa ya haki ICJ ikionekana karibu na waziri wa Mambo ya Nje ya mamlaka ya Wapalestina Riyad al-Malik na ujumbe wake katika mahakama hiyo mjini The hague Februari 19, 2024.
Nembo ya mahakama ya kimataifa ya haki ICJ ikionekana karibu na waziri wa Mambo ya Nje ya mamlaka ya Wapalestina Riyad al-Malik na ujumbe wake katika mahakama hiyo mjini The hague Februari 19, 2024.Picha: Robin van Lonkhuijsen/ANP/AFP/Getty Images

Kesi hiyo katika mahakama ya juu ya haki ya Umoja wa Mataifa, ICJ, mjini The Hague, inajiri wakati vita vya Israel na Hamas vikiendelea na kutishia kuwa kipaumbele cha vikao vya leo mahakamani.

Soma pia: Israel yatishia kushambulia Rafah wakati wa Ramadhan

Hii ni licha kwamba vikao hivyo vilikusudia kujikita kwenye suala la udhibiti wa wazi wa Israel juu ya Ukingo wa Magharibi, Ukanda wa Gaza na hatua ya kuichukua Jerusalem ya Mashariki.

Wanaharakati wanaounga mkono upande wa Wapalestina wamesema uamuzi utakuwa na uzito mkubwa sana linapokuja suala la mamlaka na maadili.

Baada ya Wapalestina kuwasilisha hoja zao, nchi nyingine 51 pia zitapewa na nafasi ikiwemo pia mashirika matatu ya kimataifa.

Israel haijaratibiwa kujitetea kwa kuzungumza mbele ya vikao hivyo lakini inaweza kuwasilisha taarifa.

Annalena ziarani Israel tena kusaka suluhisho la mgogoro

Wizara ya Afya Hamas: Idadi ya vifo Gaza yazidi 29,000

Kwingineko, wizara ya Afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, imesema idadi ya vifo ndani ya ukanda wa Gaza imefikia watu 29,000.

Vita dhidi ya Hamas, baada ya kundi hilo la wanamgambo kufanya shambulizi baya kusini mwa Israel na kuua takriban watu 1,200 na kushika wengine wapatao 250 mateka.

Soma pia: Wapalestina Rafah wahisi kukwama katikati mwa mashambulizi ya Israel

Israel, Marekani na Umoja wa ulaya miongoni mwa mataifa mengine yameliorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.

Israel imetishia kuushambulia mji wa Rafah wakati wa mwezi wa Ramadhan ikiwa mateka waliosalia mikononi mwa wanamgambo wa Palestina hawatakuwa wameachiliwa huru.

Vyanzo: APE, EBU,DPAE