1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina Rafah wahisi kukwama katikati mwa mashambulizi

15 Februari 2024

Operesheni ya kijeshi ya Israel inayotarajiwa kwenye mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah inaawacha Wapalestina milioni 1 waliokwama kwenye eneo hilo na swali kubwa moja, wapi wanaweza kukimbilia kunusuru maisha yao.

https://p.dw.com/p/4cRx3
Wakimbizi wa Gaza walitafuta hifadhi Rafah baada ya mashambulizi ya Israel kaskazini.
Zaidi ya Wapalestina milioni moja wamekwama mjini Rafh wakati IDF ikijiandaa kufanya operesheni huko.Picha: Yasser Qudih/Xinhua News Agency/picture alliance

Wakiwa taabani baada ya vita vya miezi kadhaa, Wapalestina kwenye mji wa Rafah kwa mara nyingine wanakabiliwa na mazingira ya kutakiwa wafanye uamuzi usiowezekana. Idadi kubwa ya watu wamesongamana kwenye mji huo wa kusini kabisa mwa Ukanda wa Gaza unaopakana na mpaka wenye ulinzi mkali wa Misri.

Wameduwaa ni wapi wanaweza kwenda katika wakati Israel imesema operesheni ya kijeshi ya ardhini ni lazima ifanyike kwenye eneo hilo.

"Sote tunahofia maisha yetu," anasema Iman Abu Musa, binti wa kipalestina aliyewasiliana na DW kwa njia ya mtandao wa Whatsapp. Iman mwenye umri wa miaka 22 alikimbilia Rafah kutoka mjini jirani wa Khan Younis, ambako mapambano ya ardhini kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo wa Hamas yamewalazimisha maelfu ya watu kuukimbia kwenda kutafuta hifadhi kusini na magharibi mwa Gaza.

Msichana huyo anasema kwa sasa kile kilichobakia pekee ni kuomba "manusura kutoka kwa Mwenyezi Mungu".

Watoto wa Gaza wakiandamana kupinga vita
Imetosha na mauaji, unasema ujumbe kwenye mabango yaliobebwa na watoto hawa wa Gaza.Picha: Ahmad Hasaballah/Getty Images

Hakuna mahala salama Gaza

Mnamo Ijumaa iliyopita waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema "ni vigumu kutimiza malengo ya kulitokomeza kundi la Hamas kwa kuziacha bataliani 4" za kundi hilo kwenye mji wa Rafah.

Na kisha akawaelekeza viongozi wakuu wa jeshi na masuala ya ulinzi kuandaa mkakati wa pamoja wa kuwaondoa raia kwenye mji huo na kuzitokomeza bataliani hizo za Hamas.

Soma pia: Mataifa matatu zaidi yajiunga kuonya operesheni ya Rafah

Ingawa Bw. Netanyahu amesisitiza raia wataondolewa kupitia njia salama hadi sasa hajaweka wazi ni wapi umma huo wa Wapalestina utapelekwa.

Msimamo wake wa kutaka lazima operesheni ya kijeshi ifanyike Rafah mara moja uliigutua jumuiya ya kimaita. Miito ya hadhari na tahadhari ilitolewa tangu Washington, Berlin, Paris na hata kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini New York na Geneva.

Kabla ya kuelekea Israel jana Jumatano, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock alisema, operesheni yoyote ya jeshi la Israel kwenye mji wa Rafah itahatarisha zaidi hali ya kibinaadamu akitumia maneno kwamba umati wa watu uliojihifadhi kwenye eneo hilo "hauwezi kuondoka tu kimiujiza".

Ni watu wangapi walioko Rafah?

Kabla ya vita, mji wa Rafah, unaokutikana kwenye mpaka wa Ukanda wa Gaza na Misri, ulikuwa nyumbani kwa wakaazi wapatao 300,000. Hivi sasa lakini Umoja wa Mataifa unakadiria zaidi ya nusu ya idadi jumla ya watu 2.3 waishio Gaza wamekimbilia kwenye mji huo. Majengo ya shule, hospitali na mahema yasiyo na ubora ndivyo vinatmika kuwahifadhi. Na wengine wanalala nje kabisa bila miundombinu ya kujikinga na jua au baridi.

Ukanda wa Gaza, Rafah | makaazi ya dharura
Zaidi ya Wapalestina milioni moja wamekimbilia Rafah kutoka maeneo mengine ya Ukanda wa Gaza.Picha: Abed Zagout/Anadolu(picture alliance

Afisa mmoja mwandamizi anayefanya kazi ya kutoa msaada wa kiutu ambaye aliitembelea Rafah hivi karibuni ameiambia DW mzozo wa kibinadaamu kwenye mji umepindukia mwingine wowote aliowahi kuushuhudia katika miongo kadhaa aliyofanya kazi.

Watu waliofurika Rafah ni wale waliokimbia kutoka kaskazini mwa Gaza baada ya kuamriwa kufanya hivyo na vikosi vya Israel miezi kadhaa iliyopita. Wengi walihamia mji wa Khan Younis kusini mwa Gaza. Wiki chache baadaye vikosi vya Israel vikaanza kuushambulia pia mji huo na kuwataka watu wakimbilia kusini zaidi mwa Gaza. Na sasa inaonesha mji wa Rafah ndiyo eneo la mwisho na hakuna kwengine kwa kwenda.

Choka kabisaa

Sahar Abu Zeid ni miongoni mwa wale walioukimbia mji wa Khan Younis na kuhamia Rafah anasema anatumai uvamizi kwenye mji huo utaepushwa na suluhisho la haraka litapatika. Ameiambia DW kuwa fikra tu kwamba watalazimika kuuhamia pia mji huo inaleta msongo wa mawazo. Amesema hilo limeathiri sana utulivu wa akili ya familia yake na sasa wanachofanya ni kufanya maombi tu madhila yawaepuke.

Soma pia:WHO yaonya kuhusu mashambulizi mapya ya Israel huko Rafah 

Wengine kwenye mji huo tayari wameukimbia mji huo. Walikusanya na kufungasha vitu vichache walivyo navyo. Miongoni mwao ni Basem Al-Mahmoud ambaye sasa amekimbia kwenye kambi ya wakimbizi katikati mwa Gaza.

Anasema amechukua hatua ya mapema kuepuka kuwa miongoni mwa mamia kwa maelfu wengine watakapoteza maakaazi kwenye mji wa Rafah. Lakini amesisitiza ulimwengu lazima ufahamu kwamba hakuna mahali popote salama hivi sasa ndani ya Gaza.