1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO yaonya kuhusu mashambulizi mapya Rafah

14 Februari 2024

Wakati hofu ya mashambulizi zaidi huko Rafah ikitanda miongoni mwa Wapalestina, Shirika la Afya Duniani, WHO, limeonya kwamba shambulio dhidi ya Rafah litakuwa "janga lisiloweza kuelezeka."

https://p.dw.com/p/4cOem
Mfanyakazi wa WHO
Mfanyakazi wa Shirika la Afya Duniani WHOPicha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Hofu imeongezeka miongoni mwa Wapalestina kwamba Israel huenda ikaanzisha mashambulizi mapya kwenye mji wa kusini mwa Ukanda wa Gaza wa Rafah. Mwakilishi wa WHO katika eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu Rik Peeperkorn amesema:

"Operesheni za kijeshi katika eneo hilo lenye watu wengi, zitasababisha bila shaka maafa makubwa  yasiyo kifani, na ambayo yangezidisha zaidi maafa ya kibinadamu. Wimbi jipya la watu kuhama, lingeongeza pia majeraha ya ziada na kiwewe kutokana na mashambulizi ya kijeshi. Pia itaongeza mzigo katika mfumo wa afya ambao tayari umelemewa na wenye uwezo mdogo. Hii itapelekea mfumo wa afya kuwa kwenye ukingo wa kusambaratika."

Ukanda wa Gaza | Mashambulizi huko Rafah
Mtoto wa Kipalestina akishuhudia uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Israel huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza: 12.02.2024Picha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameonya pia kwamba mashambulizi huko Rafah yatazidi kuzorotesha hali ya kibinadamu eneo hilo.

Soma pia: Mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza 'yafika pazuri'

Israel inadai kuwa itachukua hatua za kupunguza maafa kwa raia huku ikiwashutumu wapiganaji wa Hamas kwa kujificha miongoni mwa raia, hasa katika hospitali na maeneo ya makazi. Tuhuma hizo zimekanushwa vikali na kundi hilo.

Aidha Peeperkorn amesema Israel imeidhinisha chini ya nusu tu ya uwezo wake wa kupeleka misaada huko Gaza, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea na usambazaji wa vifaa muhimu kwa  hospitali za Gaza  ambazo amesema zinafanya kazi katika mazingira magumu mno.

Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas imesema watu wapatao 103 wameuawa huko Gaza ndani ya saa 24 zilizopita na hivyo kupelekea idadi ya vifo tangu kuanza kwa mzozo huo Oktoba 7 mwaka jana, kufikia watu 28.576.

Mazungumzo ya kutafutia suluhu mzozo huo yaendelea Misri

Marekani | Maandamano ya kuiunga mkono Palestina mjini New York
Maandamano ya kudhihirisha mshikamano na Palestina yaliyofanyika mjini New York Marekani: 12.02.2024Picha: Michael M. Santiago/Getty Images

Mazungumzo kati ya Israel na kundi la Hamas huko mjini Cairo yakiendelea ili kufikia angalau makubaliano ya usitishwaji mapigano.

Wapatanishi kutoka Israel, Qatar, Marekani na Misri wanaendelea leo hii kujadiliana ili kufikia makubaliano ya kusitisha vita huko Gaza na kuwezesha mpango wa kubadilishana mateka na wafungwa.

Soma pia: Baerbock ahofia mpango wa Israel kuushambulia mji wa Rafah

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa operesheni ya Israel huko Gaza, amefanya ziara yake ya kwanza nchini Misri tangu mwaka 2012 na kukutana kwa mazungumzo na Rais Abdel Fattah al-Sissi juu ya mzozo huo wa Mashariki ya Kati.

Wapatanishi wanaharakisha kufikiwa kwa makubaliano hayo kabla ya Israel kuendelea na mashambulizi yake ya ardhinikwenye mji wa kusini mwa Gaza, Rafah,  ambako sasa ni kimbilio la Wapalestina zaidi ya milioni 1.4.

(Vyanzo: Mashirika)