1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo vya COVID-19 vyapindukia milioni 5 duniani

Sylvia Mwehozi
1 Novemba 2021

Idadi ya vifo vilivyotokana na janga la Covid-19 vimepindukia milioni 5 duniani kote, ikiwa ni chini ya miaka miwili tangu mgogoro huo uanze ambao sio tu umeyatingisha mataifa maskini lakini pia mataifa tajiri

https://p.dw.com/p/42Qam
Argentinien Corona-Pandemie | Intensivstation in Firmat
Picha: Patricio Murphy/ZUMAPRESS/picture alliance

Idadi ya vifo vilivyotokana na janga la Covid-19 vimepindukia milioni 5 duniani kote, ikiwa ni chini ya miaka miwili tangu mgogoro huo uanze ambao sio tu umeyatingisha mataifa maskini lakini pia mataifa tajiri ambayo yana viwango bora vya mfumo wa afya.

Marekani, Umoja wa Ulaya , Uingereza na Brazil ndizo zenye karibu nusu ya vifo ambavyo vimeripotiwa. Marekani pekee imekwisha rekodi vifo 740,000 ikiwa ndio kiwango cha juu kuliko taifa jingine.

Hivi sasa virusi hivyo vinasambaa kwa kasi Urusi, Ukraine na baadhi ya maeneo ya mashariki mwa Ulaya ambako habari za uongo na kukosa imani katika serikali vimekwamisha juhudi za utoaji chanjo.

UK London | Impftraining
Nesi akimpatia chanjo mwananchi huko LondonPicha: Yui Mok/AFP

India ambayo ilikuwa na maambukizi mengi mapema mwezi Mei, hivi sasa ina kiwango cha chini cha maambukizi ya kila siku.

Mataifa tajiri yamekuwa na jukumu kubwa katika kampeni ya utoaji chanjo, huku mataifa hayo yakilaumiwa kwa kujitwalia chanjo za kutosha.

Marekani kwa mfano na nchi nyinginezo zimeanza kutoa chanjo ya nyongeza wakati mamilioni barani Afrika hawajapata hata chanjo ya kwanza.

Afrika imesalia ndio eneo ambalo limetoa chanjo kwa kiwango cha chini, ni asilimia 15 pekee ya wakaazi wake bilioni 1.3 waliochanjwa kikamilifu.