Venezuela na Brexit magazetini | Magazetini | DW | 03.04.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Venezuela na Brexit magazetini

 Wahariri leo hii wanatoa maoni yao juu ya mgogoro wa Venezuela na pia wanazungumzia juu ya watu wanaotaka Uingereza iadhibiwe kutokana na kuamua kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya.

Mhariri wa gazeti la ``RHEINISCHE POST`` anatoa maoni yake juu ya mgogoro wa nchini Venezuela baada ya mahakama kuu ya nchi hiyo kujaribu kulizima bunge linalodhibitiwa na upinzani.  Mhariri wa gazeti hilo la ``RHEINISCHE POST`` anasema kwa sasa jaribio la rais Nicolas Maduro la kulinyang'anya bunge mamlaka limeshindikana.  Hata hivyo Maduro anatayarisha njia ya kuielekeza nchi yake kwenye udikteta wa mrengo wa kushoto kwa sababu njia hiyo pekee ndiyo itakayo mfanya aendelee kuwamo madarakani.  Kutokana na hali mbaya ya maisha ya wananchi wake rais Maduro anahofia kufanyika uchaguzi huru nchini Venezuela.  Iwapo Venezuela itaepuka machafuko hayo haijulikani ila yote hayo yataonekana katika siku za usoni. Hata hivyo pana hatari kubwa kwamba watu wa Venezuela hawataendelea daima kuliwazwa katika kuusubiri mustakabali mzuri.

Naye mhariri wa gazeti la ``FRANKFURTER ALLGEMEINE`` anasema Rais Maduro ambaye yumo katika hali ya wasiwasi hana mpango wowote wa kuleta matumaini kwa watu wake.  Mhariri huyo anaeleza Maduro anafanya kila analoliweza ili kuendelea kuwamo madarakani ndiyo sababu mtu hapaswi kuamini kwamba Rais huyo hatajaribu tena kufanya mbinu ili kulinyang'anya mamlaka bunge ambalo kwa sasa linadhibitiwa na wapinzani.  Mbinu hizo zinaweza kusababisha hali ya machafuko nchini Venezuela inayoweza kufanana na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Gazeti la ``DER TAGESSPIEGEL`` linaeleza kwamba kuna watu wanaotoa kauli kutaka Uingereza iadhibiwe kwa sababu ya kuamua kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya lakini mhariri wa gazeti hilo hakubaliani na kauli hizo na anasema. Wazo juu ya kuiadhibu Uingereza kwa sababu ya uamuzi wake wa kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya sio sahihi asilani! Kwa sababu wazo hilo ni la hatari. Mhariri anaeleza kizazi chote kijacho kinaweza kuathirika, ikiwa vijana wa Uingereza wakati wote watasikia kwamba nchi yao inaadhibiwa na Umoja wa Ulaya. Kwa vyovyote vile mhariri anasema Uingereza itaendelea kuwamo barani Ulaya.

Nalo gazeti la ``DIE WELT`` linamlaumu waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel juu ya msimamo wake kuhusu bajeti ya ulinzi ya NATO. Gazeti hilo linasema bwana Gabriel anaufwata msimamo huo katika jitihada za kufanya kampeni ya uchaguzi mkuu ujao. Gazeti hilo linafafanua. Ujerumani ikiwa ni nchi yenye nguvu kubwa kabisa barani Ulaya, Asilani! Sio jambo la kuwajibika kwa nchi hii katika kutoa asilimia 1.2 tu kwa ajili ya ulinzi. Hata hivyo waziri Gabriel yuko sahihi anapohoji kwamba misaada ya maendeleo pia ni sera ya ulinzi ila ni vyema kutilia maani kwamba hata katika hilo Ujerumani haitimizi ahadi yake. Wakati Ujerumani imeahidi kutenga asilimia 0.7 ya pato jumla kwa ajili ya misaada ya maendeleo nchi hii hadi sasa inatoa asilimia 0.4 tu kwa ajili wa kusaidia miradi ya maendeleo duniani

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com