1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki kutuma vikosi vya jeshi nchini Libya

26 Desemba 2019

Rais wa Uturuki Reccip Tayyip Erdogan amesema serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Libya imeiomba nchi yake kupeleka vikosi vya jeshi kuulinda mji mkuu Tripoli dhidi ya mashambulizi ya vikosi hasimu.

https://p.dw.com/p/3VLNe
Schweiz UNHCR-Flüchtlingsforum in Genf | Recep Tayyip Erdogan, Präsident Türkei
Rais Recep Tayyip Erdogan wa UturukiPicha: picture-alliance/AP Photos/Pool Presidential Press Service

Erdogan amesema bunge la Uturuki litajadili na kupiga kura katika muda wa hadi wiki inayokuja kuamua kuhusu ombi hilo na kuongeza serikali yake itawasilisha muswada wa kupeleka vikosi Uturuki nchini Libya.

Akizungumza na maafisa wa chama tawala, Erdogan amesema serikali ya mjini Tripoli inayoongozwa na waziri mkuu  Fayez Sarraj imeikaribisha Uturuki kutuma vikosi vyake chini ya makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi yaliyotiwa saini hivi karibuni na pande hizo mbili.

Uturuki na Libya pia zilitiliana saini mkataba kuhusu eneo la bahari ya Mediterrania ambayo yote pamoja na ule wa ushrikiano wa kijeshi ilikabiliwa na ukosoaji kutoka kanda hiyo na pande nyingine za ulimwengu.

Utawala wa waziri mkuu Sarraj umekabiliwa na uchokozi tangu mnamo mwezi April kutoka serikali hasimu ya upande wa mashariki na vikosi vinavyoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar, ambaye anajaribu kuchukua udhibiti wa mji mkuu, Tripoli.

Erdogan: Tutapeleka vikosi Libya

Türkei Istanbul | Libyens Premierminister al-Sarraj trifft Erdogan
Rais Erdogan na waziri mkuu wa LIbya Fayez al SarrajPicha: picture-alliance/AP Photo/Turkish Presidency

"Tutakwenda maeneo tuliyokaribishwa na hatutokwenda kwenye maeneo ambayo hatualikwa" amesema Erdogan na kuongeza kwa kuwa Libya imetoa mwaliko hu, Uturuki itauridhia na kutuma vikosi vyake.

Erdogan amesema nchi yake itatoa msaada unaohitajika kwa seirkali ya Tripoli dhidi ya kile alichokiita kuwa kitisho cha jenereali Haftar anayelenga kufanya mapinduzi ya kijeshi akiungwa mkono na mataifa kadhaa ya Ulaya na kiarabu.

"Tuko upande wa serikali halali ya Libya" ameongeza kusema rais Erdogan.

Kiongozi huyo amesema muswada wa sheria kuidhinisha hatua hiyo utaweza kupelekwa bungeni baina ya Januari 8 au 9 baada ya wabunge kurejea kutoka mapumziko ya mwisho wa mwaka.

Ni wazi muswada huo utaidhinishwa na Bunge

Türkei Parlament
Bunge la UturukiPicha: picture-alliance/AA/H. Aktas

Chama cha rais Erdogan kina idadi kubwa ya wabunge, hali inayoashiria kuwa muswada huo utaidhinishwa na bunge bila pingamizi.

Libya imegawika kati ya serikali mbili, ile ya waziri mkuu Sarraj ya mjini Tripoli na nyingine yenye makao yake mashariki ya nchi hiyo, kila serikali inaungwa mkono na mkundi kadhaa ya wapiganaji wenye silaha na mataifa ya kigeni.

Mapigano kuwania mji wa Tripoli yameongezeka wiki za karibuni baada ya Haftar kutangaza operesheni ya mwisho na ya aina yake ya kuukamata mji huo mkuu. Haftar anaungwa mkono na Muungano wa Falme za Kiarabu, Misri, Ufaransa na Urusi huku serikali ya mjini Tripoli inapokea msaada kutoka Uturuki, Qatar na Italia.

Mapigano ya kuwania udhibiti wa Tripoli yanatishia kuitumbukiza Libya kwenye awamu nyingine ya machafuko yanayofanana na yale ya mwaka 2011 yaliyomuondoa madaraka na kumuua kiongozi wa muda mrefu Muammar Ghaddafi