1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utumiaji holela wa P2 kwa wasichana na hatari inayowakabili

22 Septemba 2021

Ni njia wanaoitazama kuwa rahisi na salama zaidi kwao katika kupanga uzazi, lakini matumizi yaliokithiri ya vidonde vya kuzuwia mimba kwa wasichana wengi mkoani Tabora inaweza kuwa hatari kwa afya zao, watalaam wanaonya.

https://p.dw.com/p/40f7q
Tansania Übermäßige Verwendung von P2-Tabletten
Picha: Hawa Bihoga/DW

"Nimejiwekea utaratibu, kila ikifika usiku nameza vidonge vyangu, nalala,” anasema Khanifa Adam (22), Mkazi wa Mtaa wa Ghana Mjini Tabora, akiwa ni mtumiaji mkubwa wa tembe za P2 .

Anasema amekuwa akitumia tembe hizo mfululizo kwa kipindi cha miaka mitano sasa ikiwa ndiyo mbinu yake kuu ya kudhibiti ujauzito baada ya kupokea habari kutoka kwa dada yake kuwa kuna haja ya kutumia njia za uzazi wa mpango kuepuka mimba zisizotarajiwa.

Anasema tembe hizo kwake anaona ni rahisi mno kupatikana, maduka ya dawa baridi tofauti na njia nyingine ambapo lazima aende katika kituo cha kutolea huduma za afya kuketi na mtaalamu.

"Niliamua mwenyewe kutumia, zinasaidia huwezi kupata mimba za utotoni, zisizotarajiwa kwa sababu nilianza mahusiano ya kingono nikiwa bado mwanafunzi,” Kanifa aliiambia DW.

Anasimulia kwamba tembe hizo huzinunua kwenye maduka ya dawa baridi kwa kiasi cha Tsh. 5,000 fedha ambayo hupatiwa na mwenza wake.

Soma pia: Kondomu feki zaondolewa sokoni Tanzania

Anasema katika familia hakuna mtu mwingine anayefahamu kuhusu uamuzi wake huo wa kutumia tembe hizo, isipokuwa dada yake pekee ambaye alimshauri awali juu ya njia hiyo.

Dada yake amekuwa akifahamu changamoto anayoipitia ambayo ni kutoka hedhi nyingi kuliko kawaida na zikiwa haziko katika mpangilio.

"Tangu nilipoanza matumizi ya tembe hizi kalenda yangu ilivurugika, kuna wakati niliwahi na kuna kipindi kingine nilichelewa mpaka kupatwa wasiwasi na zinapokuja zinakuwa nyingi sana,” anasimulia.

Anasema licha ya kushuhudia hilo hajawahi kwenda kituo cha afya kuchunguza hali yake na ameendelea kukaa hivyo hivyo huku dada yake akihisi mdogo wake anasumbuliwa na tumbo la chango.

Tansania Übermäßige Verwendung von P2-Tabletten
Mwandishi wa DW HAwa Bihoga akizungumza na mama mjamzito, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Busondo, wilaya ya Nzega mkoani Tabora.Picha: Hawa Bihoga/DW

Tembe hizi P2 ni nini?

Kimombo hujulikana ‘Emmergency Contraceptive Pills' ni vidonge maalum vinavyotengenezwa kwa lengo la kutumika kwa dharura kuzuwia mimba isiyotarajiwa.

Mara nyingi daktari humwandikia mtu ambaye ana shaka na kupata ujauzito asiyoutarajia baada ya tendo kwa mfano ikiwa amebakwa na inatakiwa kutumika ndani ya saa 48 hadi 72 kupata matokeo.

Kutumika kwa njia hii hakumzuii mtumiaji kutokupata magonjwa ya zinaa.

Wataalamu wa afya wanasisitiza tembe hizo hazipaswi kumezwa mara kwa mara kwani vichocheo vilivyotumika kuitengeneza huweza kuathiri mwili wa mtumiaji.

Juma Ramadhani ni Mtoa Huduma ya Afya ya Uzazi, kituo cha Afya Busondo. Anasema kinachotokea baada ya kumeza tembe hiyo huenda kupunguza kasi ya yai kutembea kuelekea kwenye mirija ya uzazi hadi kufikia mji wa mimba.

Soma pia: Uzazi wa mpango: Rwanda yaonyesha njia Afrika

Ramadhani ambaye pia ni muuguzi na mkunga wa kituo hicho, anasema zipo athari za muda mfupi na muda mrefu endapo tembe hizi zitatumika tofauti, ikiwamo kubadilisha mzunguko wa kalenda na kumuathiri mtumiaji kisaikolojia.

"Akawa anatumia isivyo zaidi, endapo atatumia mara kwa mara inaweza ikasababisha akachukua muda mrefu kuja kupata mimba, kwa sababu hizi njia za vichocheo zinapunguza ukomavu wa yai.

Wanawake Venezuela wakosa huduma ya uzazi wa mpango

"Akitumia (tembe hizi) mara kwa mara inaweza kusababisha yai likawa teke au lisikomae kwa wakati na hata kumpelekea asipate kabisa mimba (utasa),” anasema Ramadhani.

Anasisitiza kwamba tembe hizo hazipaswi kutumika zaidi ya mara nne kwa mwezi.

Kwanini mbinu hii ni kimbilio la wasichana?

DW ilizingumza na watumishi wa maduka ya dawa baridi yasiyopungua matano, mawili yakiwa katika Mkoa wa Tabora na Matatu Mkoa wa Dar es Salaam. Wanasema njia hii ni rahisi na hata wasichana inawawia rahisi kuficha vidonge hivyo.

Wanasema vidonge hivyo wanaviuza mno kwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 32, rika ambalo wengi kati yao wapo kwenye mikono ya wazazi na walezi na bado wapo kwenye mfumo rasmi wa elimu.

"Huwa tunawauliza kwanini wanajiingiza kwenye matumizi ya tembe hizi, wengi huwa hawataki kujieleza na wakati mwingine huja wavulana kuchukua badala ya wasichana, zinauzika sana,” anasema mmoja wa wauzaji ambaye hakupenda jina lake linukuliwe mtandaoni.

Anaongeza, "ni kweli dawa hizi zinahitaji cheti cha daktari lakini tunawaonea huruma na sisi tunataka pesa, tena wananunua zaidi ya dozi moja, tunawauzia.

Tansania Übermäßige Verwendung von P2-Tabletten
Wataalamu wanaonya kuwa matumizi ya holela ya vidonge vya P2 yanaweza kuvuruga mfumo wa uzazi na hata kusababisha ugumba.Picha: Hawa Bihoga/DW

Namna wanavyoshawishiana kutumia

Wasichana ambao wamezitumia dawa hizi na kuzigeuza njia zao za kudumu katika kuzuia mimba, wamekuwa na ushawishi mkubwa kwa wenzao kuingia katika uraibu huo.

"Mimba inataka maandalizi, mtoto anataka maandalizi, sasa ukijiachia tu bila kujiandaa inaweza kuwa tatizo, ni kheri kutumia P2,” anasema Husna Nassoro Mkazi wa Tabora Mjini.

Anasema msichana akipata mimba tena akiwa bado yupo nyumbani kwa wazazi wake jamii humtizama kama muhuni na kufikia hatua hata wazazi wengine kuwakataza mabinti zao kukaribiana na wewe.

Soma pia: Namna ya kumlinda mtoto na Ukimwi

"Ukichukua kijana ambaye haeleweki, atakukataa, atakukimbia kwa hiyo mtu anaona bora ajikinge asipate hiyo kitu (mimba), anaona bora atumie hizo njia, ajiepushe, kuonekana tofauti mtaani hata kwenye familia,” anasema.

Wanasema wanapenda kutumia njia nyingine za muda mrefu zinazoshauriwa kama vile sindano, njiti, kitanzi na nyinginezo lakini wanahofia kufika kwenye vituo vya afya kujua zaidi kutokana na mtizamo hasi uliopo kwa wazazi na jamii.

"Kwanza wazazi wenyewe hawataki tutumie na jamii ikikuona msichana umeenda kituo cha afya kuulizia kuhusu masuala ya afya ya uzazi na njia za uzazi wa mpango, wengi hutafsiri tofauti, wanakuona muhuni,” anasema Edina Eminael.

Wataalamu wanasema nini?

Kila dawa ina utaratibu wake wa matumizi, mtumiaji anapozidisha lazima zitamletea changamoto za muda mfupi na muda mrefu.

Kwa vile dawa hizi zinaenda kufanya kazi moja kwa moja kwenye vichocheo vya mwili, wataalamu wanaonya matumizi holela na ya muda mrefu huathiri mwili, huweza pia kusababisha saratani mbalimbali ikiwemo ya matiti.

"Wameigeuza kama mbinu ya kujikinga na ujauzito lakini si kitu sahihi, tunajua hili ni kundi maalum ambalo pia lina uwoga wa kutumia njia za uzazi wa mpango, anasema Dk. Gloria Shirima, mMshauri wa uzazi wa mpango katika. mradi wa USAID, Boresha Afya, kanda ya Kati na Kaskazini, unaotekelezwa na shirika la EGPAF na Engenderhealth.

Tansania Übermäßige Verwendung von P2-Tabletten
Vidonge vya P2.Picha: Hawa Bihoga/DW

"P2 kwa kawaida inatakiwa kumezwa katika zile siku za hatari kuweza kuzuia ujauzito, tunaona sasa hivi upatikanaji wake katika maduka ya dawa baridi (makubwa) ni rahisi, wananunua, hakuna kupanga foleni," anasema Dk. Shirima.

"Wanaona aibu kwenda vituo vya afya kwa sababu kule wanaweza kukutana na ndugu zao na hata wazazi wao, hivyo wakawa katika ile taharuki ya kujulikana kwamba wameanza kutumia njia za uzazi wa mpango.”

Dk. Shirima anasema tembe za P2 zimewekwa kiwango kikubwa cha vichocheo kuliko zile njia nyingine za kawaida za uzazi wa mpango.

"Mara nyingi anayetumia njia hizi mfululizo anaweza kupata mvurugano wa hedhi, ikakata au akapata mfululizo na hata kuchukua muda mrefu kushika mimba pale atakapohitaji kwa sababu ya ule mvurugano wa kalenda,” anabainisha. Dk. Shirima anasema katika mkoa wa Tabora zimeanzishwa program maalum za kusaidia vijana.

Soma pia: Melinda:Wezesha wanawake kuisaidia Afrika

"Tunashirikiana na Serikali, watoa huduma za afya wa vituoni pamoja na wale wa ngazi ya jamii (CHWs), tumetengeneza mazingira kwa ajili ya vijana ili waweze kufika kwenye vituo vya afya, elimu sahihi kuhusu afya ya uzazi inafikishwa pia mashuleni,” anasema Dk Shirima.

"Vijana wanafika kwenye vituo wanatoa huduma za uzazi wa mpango hadi siku ya Jumamosi na Jumapili hata muda wa ziada baada ya saa za kazi za kawaida wanapata huduma."