1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uzazi wa mpango: Rwanda yaonyesha njia Afrika

Admin.WagnerD11 Julai 2012

Rwanda ni nchi ya kwanza Afrika kuanzisha sera ya taifa ya uzazi wa mpango. Kwa kipindi cha miaka mitano sasa, serikali ya Rwanda imekuwa ikiwahamasisha wananchi wake kuwa na watoto wasiozidi watatu.

https://p.dw.com/p/15V9z
Watoto wa Rwanda.
Watoto wa Rwanda.Picha: AP

Miaka mitano baada ya kuanzishwa kwa sera hiyo, serikali ya Rwanda imesema sera hiyo imezaa matunda kutokana na kupungua kwa idadi ya watoto wanaozaliwa nchini humo. Pamoja na mafanikio hayo lakini bado kuna changamoto.

Rwanda ni moja ya nchi ndogo yenye watu wengi zaidi katika bara la Afrika, ikiwa na zaidi ya wakaazi mia nne katika kila kilomita moja ya mraba. Mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yalisababisha nchi hiyo kuwa katika dimbwi kubwa la umaskini na kuathiri sekta zote muhimu. Hata hivyo ongezeko la watu, kukosekana kwa huduma za afya na baadhi ya watu kukosa mawazo ya kufikiri ni moja ya vikwazo kwa maendeleo endelevu ya nchi hiyo.

Familia ya wakimbizi nchini Rwanda.
Familia ya wakimbizi nchini Rwanda.Picha: picture-alliance/dpa

Katika kudhibiti ongezeko la idadi ya watu ambalo lilionekana kuwa ni changamoto kubwa, serikali ilianza juhudi za kuwahamasisha wananchi wake kuzaa watoto wasiozidi watatu. Serikali hiyo sasa inasema kuwa juhudi hizo zimekuwa na manufaa. Arthur Asiimwe, ambaye ni mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya huduma za afya kwenye Wizara ya Afya nchini Rwanda anasema matokeo ya utafiti kuhusu masuala ya afya yanaonyesha kuwa kwa wastani, mwanamke mmoja wa Rwanda alikuwa na watoto zaidi ya sita.

"Huo ni utafiti uliofanyika miaka mitano iliyopita, lakini sasa kwa matokeo ya mwaka 2010 kwa wastani mama mmoja ana watoto wanne," alisema na kuongeza, "hii inaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kampeni iliyofanyika kuhamasisha familia kuhusu uzazi wa mpango zimezaa matunda kwa watu kuwa makini kuhusu uzazi wa mpango."

Kila kijiji na wataalamu wa uzazi wa mpango
Asiimwe anasema kila kijiji nchini Rwanda kimepatiwa wataalamu wawili wa masuala ya afya kwa ajili ya kuwahamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya njia za kawaida na za kisasa za uzazi wa mpango. Katika baadhi ya maeneo, njia mpya  za uzazi wa mpango kwa wanaume zimeanzishwa.

Uwimana Gadi  ni baba ambaye amekwishaanza kutumia njia za kiume za uzazi wa mpango: "Nina watoto sita, mimi na mama yao hatuna kipato cha kukidhi mahitaji yetu, tunaishi kwa kutegemea vibarua kwa majirani zetu. Nimelazimika kutumia njia ya uzazi wa mpango kwa wanaume ili kujizuia kuwa na watoto wengine zaidi. Imekuwa vigumu kwangu kuwatunza watoto wangu, kwa nini niendelee kuongeza wengine?"

Mauaji ya kimbari yalipunguza familia
Hata hivyo kuna taarifa za hofu kuwa sera ya uzazi wa mpango Rwanda inaweza kushusha hadhi ya taifa hilo, ambalo linaonekana kubadilika katika kipindi cha miaka mitano. Historia ya mauaji ya kimbari pia ilipelekea watu kuamini katika familia kubwa, kama anavyosema Joyce Uwera.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
Rais wa Rwanda, Paul Kagame.Picha: picture-alliance/dpa

"Mimi na mume wangu ni yatima wa mauaji ya kimbari, mume wangu hana familia nyingine kama ilivyo kwangu. Tunataka kuwa na watoto wengi iwezekenavyo ili kufidia familia tulizozipoteza. Nashindwa kuelewa ninapoaambiwa nizae mtoto mmoja tu. Haiwezekani."

Kwa mujibu wa serikali ya Rwanda, sera hiyo ya kila familia kutokuwa na zaidi ya watoto watatu, haiwezi kupitishwa kuwa sheria kwa sasa, ingawa tayari kuna mabadiliko mengi tangu kuanzishwa kwake, na wataalamu wanaamini kuwa wananchi wataendelea kukubaliana na ukweli kwamba ongezeko la watu lazima lidhibitiwe.

Mafanikio yake, kama vile kupungua kwa vifo vya watoto na kupungua kwa umasikini, ambayo hupelekea elimu bora kwa wote, yanaweza kuwa kigezo chema kwa nchi nyengine duniani kufuata.

Mwandishi: Sylivanus Karemera/Flora Nzema
Mhariri: Mohammed Khelef