Urusi yashutumu mataifa ya Magharibi | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Urusi yashutumu mataifa ya Magharibi

Urusi imeyashutumu mataifa ya Magharibi kwa kuwasaidia waasi nchini Syria, baada ya mkutano na Iran na Uturuki kwenye awamu ya mazungumzo mapya ya kujaribu kutafuta ufumbuzi wa mzozo unaoendelea nchini humo.

Mawaziri wa mambo nje wa Urusi, Iran, Uturuki walikutana katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana, wakiangazia suala la Ghouta Mashariki ambayo ni ngome ya upinzani iliyoko nje ya mji wa Damascus, iliyoanza kushambuliwa mwezi mmoja uliopita na utawala wa rais Syria Bashar al-Assad.

Mkutano wa Astana ulilenga kuweka msingi wa kikoa cha marais wa mataifa hayo matatu kitakaochofanyika mjini Istanbul Aprili 4. Akiongea baada ya mazungumzo hayo waziri wa masuala ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov ameyalaumu Mataifa ya Magharibi kwa kuwakingia kifua waasi na hata kuimarisha uwezo wao wa kivita.

Mataifa ya Urusi na Iran yanamuunga mkono rais Assad, lakini Uturuki imetaka kusitishwa kwa mashambulizi Ghouta Mashariki ambapo takriban watu 1,260 wameuawa wengi wao wakiwa watoto tangu lianze kushambuliwa mwezi Februari tarehe 18.

Syrien Luftangriffe auf Ost-Ghuta (picture-alliance/abaca/AA/M. Taim)

Syria yashambulia eneo la Ghouta Mashariki

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelielezea janga la kibinadamu katika eneo hilo ambalo halina chakula, maji na mahitaji mengine ya kimsingi kuwa jehenamu ya duniani.

Lavrov ayakosoa mataifa ya Magharibi

Lakini  Lavrov alisema kuwa mtazamo wa mataifa ya Magharibi ni wa upande mmoja na kuwashutumu wenzao kwa kujaribu kuwalinda waasi, akitoa mfano wa kundi la Hayat Tahrir al-Sham ambalo limeundwa na waliokuwa wapiganaji wa kundi la Al-Qaeda ambalo liko Ghouta Mashariki. Amesema kuwa kundi hilo linafuata maelekezo kutoka kwa mataifa ya Magharibi. Lavrov pia ameonya dhidi ya kitisho cha Marekani kuushambulia mji mkuu wa Syria Damascus haitakubalika.

Lavrov amesema, "tunapenda kukumbusha kwamba matumizi ya nguvu dhidi ya Damascus kwa visingizio hayakubaliki. Vitisho vilivyotolewa hivi karibuni na Marekani kuhusu mashambulizi ya upande mmoja dhidi ya Syria ikiwemo Damascus - kama tuhuma zisizo na msingi mwezi Aprili mwaka uliopita kuhusiana na matumizi ya silaha za kemikali na serikali ya Syria - hazikubaliki na hazitovumiliwa."

Urusi, Iran na Uturuki zaafikiana

Katika mwafaka uliotiwa saini na Lavrov, Mohammad Javad Zarif wa Iran na Mevlut Cavusoglu wa Uturuki- na kutolewa na wizara ya mambo ya nje ya Kazakhstan, mwishoni mwa mazungumzo, mataifa hayo matatu yaliamua kuvunja nguvu za makundi yanayohusishwa na Al-Qaeda.

Ghouta Mashariki ilistahili kulindwa na kuwa salama. Lakini utawala wa Syria na Urusi wametumia kisingizio cha waasi katika eneo hilo kutekeleza mashambulizi.  

Wakati hayo yakiarifiwa shirika la uangalizi wa haki za biadamu nchini Syria linasema mashambulio ya angani ya Urusi na serikali ya Syria Ghouta Mashariki yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 46 katika muda wa masaa 24.

Türkei beginnt Offensive Operation Afrin in Syrien (picture alliance/AA/O. Coban )

Eneo la Afrin lashambuliwa na utawala wa Syria

Ripoti ya kundi hilo inasema kuwa mji wa Kafr Batna ulishambuliwa na vilipuzi hii leo. Vikosi vya serikali  vinaelekea katika ngome za waasi hali ambayo imechangia raia wengi kuhama.

Kwingineko katika mji wa Afrin ulioko kaskazini mwa Syria takriban raia 20 wameuawa, miongoni mwao kina mama na watoto huku wengine 30 wakijeruhiwa.

Picha zilizotumwa na wanaharakati wa Kikurdi zilionyesha watoto wakilia huku wakitokwa damu walipokuwa wakipelekwa katika hospitali ya Afrin kutibiwa.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Ap, Afp, dpa

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com