1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yapuuza ombi la Ukraine la mazungumzo

Bruce Amani
12 Aprili 2021

Hali mashariki mwa Ukraine inaendelea kuwa tete, baada ya wanajeshi wawili wa nchi hiyo kuuawa katika makabiliano na wapiganaji wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi. Urusi haujajibu ombi la Ukraine la mazungumzo

https://p.dw.com/p/3rtYb
BG Spannungen an der russisch-ukrainischen Grenze
Picha: AFP

Makabiliano yamezuka kila mara mashariki mwa Ukraine katika wiki za karibuni, hali inayohujumu mpango wa usitishaji mapigano uliofikiwa mwaka jana na ambao ulikuwa umeongeza matumaini ya kuumaliza mzozo uliozuka mwaka wa 2o14 baada ya Urusi kuinyakua rasi ya Crimea.

Msemaji wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Urusi sasa ina wanajeshi 41,000 kwenye mpaka wa mashariki wa Ukraine na wanajeshi 42,000 katika rasi ya Crimea.

Soma pia: Urusi yajitetea kujiimarisha kijeshi kwenye mpaka na Ukraine

Msemaji Yulia Mendel pia amesema rais Zelensky mwishoni mwa Machi alituma ombi kwa serikali ya Urusi la kufanya mazungumzo na Rais Vladmir Putin kuhusu kuongezeka kwa mvutano, lakini bado hajapata jibu

Puitn und Selenskyj mit Macron in Paris
Picha ya maktaba ikiwaonyesha marais Zelensky, Macron na PutinPicha: Imago Images/ITAR-TASS/Russian Presidential Press and Information Office/A. Nikolsky

Msemaji wa Ikulu ya Urusi Dmitry Peskov amesema hajaona ombi lolote la aina hiyo la mazungumzo katika siku za karibuni, na hana habari kama kulitolewa ombi lolote katika siku za karibuni. Urusi, ambayo haijakanusha kupeleka vikosi mpakani, imesema haitaki kuanzisha vita na Ukraine kama anavyoeleza Peskov. "Hakuna atakayekubali uwezekano wa vita ya wenyewe kwa wenyewe Ukraine. Urusi haikuwahi kuwa sehemu ya mzozo huu. Lakini Urusi aghalabu inasema haitaacha kuchukua hatua za kuwalinda wakaazi wanaozungumza Kirusi, ambao wanaishi kusini mashariki mwa Ukraine." Ameema Peskov.

Soma pia: Merkel, Putin wahimiza kutulizwa mivutano mashariki Ukraine

Mgogoro huo, ambao umewauwa Zaidi ya watu 13,000, umesababisha vifo vya wanajeshi 28 wa Ukraine tangu mwanzo wa mwaka huu ikilinganishwa na 50 katika mwaka mzima wa 2020.

Mendel amesema Rais Zelensky anatarajiwa kuelekea Paris kwa mazungumzo na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron baadaye wiki hii.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine Dymtro Kuleba atazuru makao makuu ya NATO kukutana kesho na Katibu Mkuu wa muungano huo wa kijeshi Jens Stoltenberg wakati pia waziri wa mambo ya kigeni wa Masrekani Antony Blinken akielekea Brussels kwa mazungumzo.

AFP/Rueters