Urithi wa Obama wakabiliwa na kitisho | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.01.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Marekani

Urithi wa Obama wakabiliwa na kitisho

Urithi wa Barack Obama kutokana na yale aliyoyafanya unakabiliwa na changamoto kubwa, kutokana na wasiwasi kwamba yote hayo yanaweza kupanguliwa na rais ajaye nchini humo Donald Trump, kutokana na msimam tofauti

Rais wa Marekani Barack Obama aliapishwa mwaka 2009. Miaka minane baadae wengi wanaoangalia kutokea wakati alipochukua madaraka, ni kama ulimwengu umepagawa. Mwandishi wa DW Michael Knigge anasema kwa kuangazia alikoanzia Obama na serikali yake haitakuwa sawa kutathmini rekodi yake tu, kwani ni wazi kwamba mazingira ya kidunia aliyokutana nayo katika awamu yake ya kwanza ya uongozi yalikuwa tofauti katika maeneo mengi, na hayawezi kufananishwa na yale atakayokutana nayo anayechukua nafasi hiyo atakapoapishwa baadae mwezi huu. 

Inawezekana Obama aliingia madarakani wakati wa kipindi kigumu zaidi ikilinganishwa na marais wengine tangu enzi ya Rais Franklin D. Roosevelt, anasema Profesa wa masomo kuhusu masuala ya Marekani katika taasisi ya University College London, Iwan Morgan. "Marekani ilikuwa ikikabiliwa na hali mbaya zaidi ya kiuchumi tangu kutokea kwa mdororo mkubwa wa kiuchumi Marekani na Ulaya, na ilijihusisha na vita viwili vya nje. Roosevelt alipata wakati mgumu alipochukua madaraka", amesema Morgan.

Kwa kuziunganisha changamoto alizokutana nazo, Obama pia alitakiwa kukabiliana na changamoto kubwa ya misimamo ya kisiasa iliyokuwa imefikia kilele wakati akichukua madaraka, na kuchukua muda wake kufanya kazi na wapinzani wa chama cha Republican ambao lengo lao kuu kisiasa lilikuwa ni rahisi tu, kumzuia ama kumuondoa madarakani.

USA Präsident Donald Trump (Getty Images/AFP/D. Emmert)

Donald Trump rais mteule anayetarajiwa kufanyia marekebisho ama kufuta kabisa aliyoyafanya mtangulizi wake Barack Obama

Kiuchumi, Obama amefanikiwa kuiepusha Marekani kuangukia kwenye mdororo mwingine wa kiuchumi kufuatia mgogoro wa kifedha mnamo mwaka 2008, ni miongoni mwa rekodi zake, kama leo atatathminiwa kwa kuzingatia mafaniko yake, anasema mwalimu wa masomo yahusuyo utawala wa Marekani kwenye chuo Kikuu cha Oxford, Desmond King. 

Katika kukabiliana na madhara ya haraka ya mgogoro wa kifedha, Obama alifanikiwa sio tu kupitishwa katika bunge la Marekani, mpango mkubwa kwa ajili ya kuchochea ukuaji sekta ya fedha katika historia ya Marekani, bali pia alisaini kanuni za kifedha katika sheria ya mageuzi na kuwalinda watumiaji, ya Dod-Frank, ili kuzuia majanga kama hayo kutokea kwa siku za usoni.

Obama amejiwekea historia isiyobadilika ya kuwa Rais wa kwanza mweusi wa Marekani.

Wakati mafanikio haya ya Obama yanakabiliwa na kitisho cha kutenguliwa na rais ajaye Donald Trump, "kile alichokifanya Obama na ambacho kitasalia palepale ni namna alivyoweza kuiweka Marekani mbali na majanga", ameandika Profesa wa mahusiano ya kimataifa katika Graduate Institute ya Geneva, David Sylvan kupitia barua pepe. Miongoni mwa majanga hayo ni kutetereka kwa uchumi na mafanikio ya Obama katika kuiimarisha tena Marekani kiuchumi baada ya mdororo wa uchumi wa mwaka 2007-08.

Kuhusu sera za ndani, Obama alifanikisha sera ya afya, maarufu kama ObamaCare. Hii ni alama ya urithi wa Obama amesema King. Alifanikiwa kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa mamilioni ya Wamarekani waliokosa huduma hiyo hapo awali. Ni programu mpya na muhimu zaidi kuanzishwa tangu miaka ya 1960, amesema Morgan. Iliwashinda marais watatu ama wanne waliomtangulia.

Na kuhusiana na sera za nje, wachambuzi wanasema wakati mkataba wa nyuklia na Iran ukichukuliwa na wasomi kwamba ni mkataba muhimu zaidi kwenye sera za nje uliofanikiwa chini ya Obama, lakini pia makubaliano hayo yanakabiliwa na kitisho cha kuvurugwa na utawala wa Trump. Na ndio maana Sylvan anasema hatua ya Obama ya kukataa kujiingiza kijeshi kwenye vita vya Syria kunasalia kama miongoni mwa mafanikio yake mawili makubwa, na ni sifa ambayo hata utawala mpya wa Trump hautaweza kuifuta. 

Jingine ambalo Obama anatajwa kufanikiwa ni mahusiano ya kijamiii. Bila kujali ni nini ambacho Trump na wafuasi wake wa Republican wanataka kufanya dhidi ya urithi wa sera zake, Obama tayari amenyakua nafasi muhimu kwenye historia yake kama rais wa kwanza Mmarekani mweusi wa Marekani. Hilo tu, lilikuwa ni muhimu, anasema King na lisingeweza kutokea bila ya mabadiliko yaliyofikiwa kupitia harakati za haki za kiraia za miaka ya 1960.  

Kwa maoni yangu, aina ya uoga wa kitamaduni wanaohisi Wamarekani weupe kutokana na Rais mweusi katika Ikulu ya White House ilijumuisha matatizo yaliyomkumba Hillary Clinton. Rais wa kwanza mweusi, kumuachia madaraka rais wa kwanza mwanamke ni kitu ambacho Wamarekani wengi walikipinga na kuamua kumpigia kura Trump.

Mwandishi: Lilian Mtono
Mhariri: Grace Patricia Kabogo 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com