Unicef: Ndoa za utotoni zimepungua duniani | Afya na masuala ya kijamii | DW | 06.03.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Afya na masuala ya kijamii

Unicef: Ndoa za utotoni zimepungua duniani

Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa, Unicef limesema ndoa za utotoni zimepungua kwa kiwango kikubwa duniani, hususan katika nchi za Asia Kusini. Hata hivyo bado tatizo hilo ni kubwa Afrika ya Kusini mwa Sahara.

Bildergalerie Kinderheirat in Südasien (Getty Images/AFP/Str)

Tatizo la ndoa za utotoni India limepungua kwa kiasi kikubwa

Ripoti hiyo ya Unicef iliyochapishwa Jumanne, inaonyesha kuwepo upungufu wa ndoa za utotoni zipatazo milioni 25 duniani tangu mwaka 2008, kutokana na kampeni ya kupinga ndoa hizo. Kulingana na ripoti hiyo, nchi za Kusini mwa Asia zilipiga hatua kubwa zaidi kivitendo.

Wanaharakati dhidi ya ndoa za utotoni na maafisa wa taasisi zinazohusika katika kampeni hiyo wanasema mafanikio yamepatikana kutokana na kuongezeka kwa elimu, pamoja na uhamasishaji wa umma kuelewa madhara yatokanayo ndoa hizo.

Pamoja na hayo lakini Unicef imeonya kwamba hadi mwaka 2030, wasichana wapatao milioni 150 wanakabiliwa na hatari ya kuozwa kabla ya kutimiza miaka 18, ikiwa juhudi zaidi hazitachukuliwa. Malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo endelevu, yanaazimia kumaliza kabisa ndoa za utotoni ifikapo mwaka huo wa 2030.

Tatizo lahama kutoka India hadi Afrika

Maendeleo makubwa yamepatikana India ambako idadi ya wasichana wanaoozwa wakiwa wadogo imepungua kwa takriban asilimia 50. Mkuu wa Unicef nchini India Javier Aguilar amesema kuwa kwa sasa ni asilimia 27 ya wasichana wa India wanaoolewa kabla ya kufika umri wa utu uzima, ikilinganishwa na asilimia 47 muongo mmoja uliopita.

Kinderehe Child marriage Chad Tschad (picture alliance/dpa/O.Cicek )

Mmoja kati ya watoto watatu walioolewa duniani yuko Afrika

Ripoti ya Unicef inaonyesha kwamba matatizo ya ndoa za utotoni yamehama kutoka Ukanda wa Asia Kusini na kuelekea katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Imeelezwa kuwa mmoja kati ya wasichana wanaoolewa wakiwa watoto, anatoka katika nchi hizo za Afrika. Hii inadhihirisha kuwa nchi hizo zimebaki nyuma, kwani miaka 10 iliyopita kiwango hicho kilikuwa msichana mmoja kati ya watano.

Mfano mwema barani Afrika umetajwa kuwa Ethiopia ambayo imepunguza sana ndoa za utotoni, na kuondoka katika nchi tano zinazoongoza kwa kuwa na ndoa za aina hiyo.

Madhara ya muda mrefu

Kwa mujibu Unicef, wanawake milioni 650 duniani kote waliolewa wakiwa watoto. Makadirio ya shirika hilo ni kuwa kwa wakati huu, wasichana milioni 12 huolewa mwaka duniani kote kabla ya kutimiza miaka 18.

Mshauri mkuu kuhusu masuala ya jinsia katika shirika la Unicef Anju Malhotra amesema msichana akilazimishwa kuolewa akiwa mdogo, anakabiliwa na athari za hapo hapo na za muda mrefu. Uwezekano wake wa kupata elimu unapungua, huku hatari za kunyanyaswa na mmewe na kupata matatizo wakati wa ujauzito na kujifungua zikiongezeka. Aidha, afisa huyo ameongeza kuwa jamii nzima hupoteza kutokana na ndoa hizo, kwa sababu ni chanzo cha mzunguko wa umasikini.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, dpae, dw

Mhariri: Josephat Charo

Sauti na Vidio Kuhusu Mada

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com